Yaliyojiri katika Siasa 2012

ndiyomkuusana

JF-Expert Member
Aug 2, 2012
666
421
Hamad Rashid atimuliwa CUF
Januari 5

CHAMA cha Wananchi (CUF) kilimtimua na kumvua uanachama Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, ndani ya chama hicho, hivyo kumfanya apoteze sifa ya kuwa mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (bara), Julius Mtatiro, alitangaza kutimuliwa kwa mbunge huyo na baadaye aliamua kukimbilia mahakamani ili kupata hati ya zuio la mkutano huo.
Mbunge Regia Mtema afariki
Januari 14

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kilipata pigo kwa mbunge wake wa viti maalumu mkoa wa Morogoro, Regia Mtema, kufariki baada ya gari alilokuwa akiliendesha kupinduka mara tatu katika eneo la Ruvu JKT, Mlandizi, wilayani Kibaha, mkoani Pwani.
Mbunge wa Arumeru Jeremia Sumari (CCM) afariki
Januari 19

MBUNGE wa Arumeru Mashariki, Jeremia Solomon Sumari (CCM), alifariki katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Sumari ambaye pia aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha, alifariki zikiwa zimepita siku tano tu tangu kitokee kifo cha Mbunge wa Viti Maalum, Regia Mtema (CHADEMA), ambaye alizikwa nyumbani kwao Ifakara.
CHADEMA wambana JK mchakato wa Katiba
Januari 23

LICHA ya Rais Jakaya Kikwete, kukutana mara mbili na ujumbe mahususi wa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Ikulu jijini Dar es Salaam kujadili masuala mbalimbali ikiwamo mchakato wa uundwaji wa Katiba mpya, bado pande hizo mbili zilionekana kutoafikiana juu ya marekebisho yanayotakiwa.
Mjadala wa posho za wabunge
Februari mosi

RAIS Jakaya Kikwete na Spika wa Bunge, Anna Makinda, walijiweka pabaya kwa kutoa kauli zinazopingana kuhusu posho mpya za kikao kwa wabunge.
Huku Makinda akisema Rais Kikwete ndiye aliyebariki posho hizo za shilingi 200,000 kwa siku, Kurugenzi ya Mawasiliano ilisema kwamba Rais hahusiki.
Mgogoro wa madaktari watinga bungeni
Februari 2

MGOMO wa madaktari ulilitikisa Bunge ambalo lilitishia kutoendelea na shughuli zake endapo serikali isingelitoa hatima ya mgomo huo.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema alishangazwa na ukimya wa serikali kwani ilikuwa imeahidi kutolea kauli, lakini hadi siku hiyo ilikuwa haijasema chochote huku mgomo huo ukiendelea kushika kasi na hali za wagonjwa zikizidi kuwa mbaya
Kampeni zashamiri Arumeru
Machi mosi

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, alipata mapokezi ya kifalme mkoani Arusha, yakianzia Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) mpaka eneo la Tengeru kwa Pole.
Dk. Slaa aliwasili Arusha kwa ajili ya kumfanyia kampeni mgombea ubunge wa jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, akitokea mkoani Mwanza.
Kada wa CHADEMA amwagiwa tindikali
Machi 30

KADA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zabron Yusuf, alimwagiwa tindikali na watu wanaoaminika kutumwa na chama kimoja cha siasa usiku wakati akijaribu kumwokoa mwanachama mwenzake aliyekuwa ametekwa na watu hao.
CCM yaanguka Arumeru uchaguzi mdogo
Aprili 2

KULIKUWA na uchaguzi mgumu kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) lakini kilifanikiwa kushinda kiasi cha Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi(CCM) kukiri kupigwa. Jimbo hili lilinyakuliwa na kijana mdogo Joshua Nassari, licha ya uchaguzi huo kugubikwa na hila.
CHADEMA yamnasa Millya wa Lowassa
Aprili 16

MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UV CCM), mkoa wa Arusha, James Millya, alijitoa kwenye chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Mawaziri wang’oka
Aprili 20

Mawaziri saba kati ya nane wakiwemo waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma za ubadhirifu, waliandika barua za kujiuzulu kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kukinusuru Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mawaziri hao ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika; Waziri wa Uchukuzi Omari Nundu; Waziri wa Afya, Dk. Haji Mponda; Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja; Naibu Waziri wa Afya, Lucy Nkya na Naibu Waziri wa Viwanda, Lazaro Nyarandu.
Mwenyekiti wa CHADEMA auawa
Aprili 27

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kata ya Usa River, wilayani Arumeru, Msafiri Mbwambo (38), aliuawa kwa kukatwa shingoni na kitu chenye ncha kali.
Mahakama yamnyang’anya ubunge Hayeshi
Mei Mosi

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kilipata pigo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga kutengua matokeo ya ubunge wa jimbo la Sumbawanga mjini yaliyompa ushindi mgombea wake Hayeshi Hilalm, baada ya kubaini dosari wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31, 2010.
JK amteua Mbatia wa NCCR kuwa mbunge
Mei 3

RAIS Jakaya Kikwete alimteua Mwenyekiti wa NCCR mageuzi James Mbatia kuwa mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mawaziri wang’olewa
Mei 4

RAIS Jakaya Kikwete alitangaza baraza lake la mawaziri na kuwatupa nje mawaziri waandamizi akiwemo Mustafa Mkulo, huku akiweka wazi kuwa atawashukia makatibu wakuu na wakurugenzi wote ambao wizara na idara zao zilihusishwa na tuhuma za ufisadi.
Alimtupa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Maliasiri na Utalii, Ezekiel Maige; Omari Nundu aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi; na Dk. Cyril Chami aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara ambaye amerithiwa na waziri mpya, Abdallah Kigoda.
Wakuu wa wilaya 51 wafyekwa
Mei 9

RAIS Jakaya Kikwete aliwafyeka wakuu wa wilaya 51 kwa sababu mbalimbali, zikiwamo za kinidhamu, katika uteuzi mpya uliotangazwa na kuwaingiza wana habari saba kuwa miongoni mwa wakuu wapya wa wilaya.
Mnyika aachiwa ubunge wake
Mei 24

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilimtangaza Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), kuwa ndiye mbunge halali wa jimbo hilo na matokeo ya uchaguzi ya jimbo hilo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Novemba mwaka 2010, yalikidhi matakwa ya kisheria.
Mbunge wa CCM atimuliwa bungeni
Julai 13

MBUNGE wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile (CCM), alifukuzwa bungeni na kutakiwa kutohudhuria vikao vitatu, kutokana na kugoma kufuta kauli yake ya kuwatuhumu madiwani wanne wa jimboni kwake kuwa walihongwa na Waziri wa Ardhi ili kuunga mkono ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni.
Zitto na kauli ya urais
Julai 26

HARAKATI za kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2015 zilianza kuwatesa viongozi wa vyama vya siasa ambapo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) bara, Zitto Kabwe, alisema kama akiandikiwa kuwa Rais hakuna wa kumzuia.
Bunge lanuka rushwa
Julai 28

Bunge liliwaka moto baada ya baadhi ya wabunge kuwanyooshea vidole wenzao kwa madai ya kupokea rushwa kwa lengo la kuwapigia debe mafisadi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wanaowafilisi Watanzania.
Wabunge hao walidaiwa kuwaunga mkono mafisadi ili Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakimu Maswi, waonekane hawafai.
Tuko tayari kwa vita
Agosti 8

KAMATI ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, ilisema majeshi ya Tanzania yalikuwa tayari kiakili na kivifaa ikibidi kuingia vitani kutokana na mzozo wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi.
Kauli hiyo ilitolewa mjini Dodoma na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Edward Lowassa, alipozungumza na waandishi na habari.
Zitto ataka walioweka fedha nje kutajwa
Agosti 15

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), aliitaka Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA), kufanya uchunguzi wa manunuzi ya mafuta ya kuzalisha umeme ambayo yanagharimu sh bilioni 42 za serikali kila mwezi.
CHADEMA yailiza CCM Igunga
Agosti 21

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kilipata pigo jingine baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kumvua ubunge, Dk. Peter Kafumu, aliyekuwa Mbunge wa Igunga, baada ya mahakama kuthibitisha kwamba taratibu za uchaguzi mdogo uliomwingiza madarakani zilikiukwa.
Dk. Kigwangala, Bashe watishiana bastola Nzega
Agosti 31

KUWEPO kwa makundi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), yaliyoanza kujiimarisha katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho kwa kuwepo mwendelezo wa visasi ndani ya chama hicho kumesababisha kukesekana kwa uelewano katika jimbo la Nzega, mkoani Tabora hadi kufikia Mbunge wa sasa, Dk. Hamis Kigwangala, na kada aliyeenguliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa, Hussein Bashe, kutishiana bastola.
Sophia Simba ambwaga Anne Kilango
Oktoba 20

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), Sophia Simba, alifanikiwa kutetea kiti chake baada ya kuibuka mshindi na kumbwaga mpinzani wake, Anne Kilango Malecela, katika uchaguzi uliofanyika Dodoma na kutawaliwa na vituko vingi, vikiwamo vijembe, kashfa na kugubikwa na tuhuma za rushwa.
Zitto ataka umri wa kugombea urais uwe miaka 35
Novemba 3

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), alitaka umri wa kugombea urais ushushwe kutoka miaka 40 hadi kufikia 35.
Familia ya JK yamuokoa Membe
Novemba 12

LICHA ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, kuwaeleza wajumbe wa Mkutano Mkuu kuwa haungi mkono kundi lolote ndani ya chama katika mbio za urais 2015, mkewe Salma Kikwete na mwanaye Ridhiwan, walitajwa kuongoza kampeni za kumnusuru Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe.
Mbunge Makweta afariki
Novemba 17

MBUNGE wa Njombe wa muda mrefu na mwanasiasa wa siku nyingi nchini, Jackson Myangila Makweta, alifariki Dar es Salaam kutokana na na matatizo ya moyo yaliyokuwa yakimsumbua.
Lema kulamba mil. 20
Desemba 24

BUNGE lilisema Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, atalipwa mafao yake yote ya mshahara na posho kwa kipindi chote cha siku 260 alizokuwa nje ya Bunge.
Lema alivuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha mnamo Aprili 5, mwaka huu, baada ya Jaji Gabriel Rwakibarila kuridhika na ushahidi wa wanachama watatu wa CCM, Musa Mkanga, Agnes Mollel na Happy Kivuyo.
 
Back
Top Bottom