Kila la kheri mkutano wa WEF Afrika
Maoni ya katuni
Mkutano wa Kiuchumi wa Dunia kuhusu Bara la Afrika (WEF), unatarajia kuanza kesho jijini Dar es Salaam na kuwashirikisha wakuu wa nchi na serikali kadhaa barani. Tayari maandalizi ya mkutano huo yamekamilika kwa sehemu kubwa, ikiwa ni pamoja na kuanza kuwasili kwa wajumbe wakiwemo maofisa waandamizi na viongozi.
Mkutano huo ni mkubwa kwa kuzingatia kwamba unawashirikisha wajumbe 1,000, idadi ambayo ni kubwa.
Kwa bahati nzuri, Tanzania imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo muhimu ambao utajadili mambo mengi muhimu, yakiwemo ya uchumi kwa ujumla na utawala bora barani Afrika.
Mkutano huo wa kwanza kufanyika katika ukanda wa Afrika Mashariki tangu ulipoanza miaka 20 iliyopita, utawahusisha Marais Armando Emilio Guebuza (Msumbiji), Paul Kagame (Rwanda) na Ali-Bongo Ondimba (Gabon). Wengine ni Hifikepunye Pohamba (Namibia), Boni Yayi (Benin), Jacob Zuma (Afrika Kusini) na mwenyeji wao, Jakaya Kikwete (Tanzania).
Mbali na marais hao, atakuwepo pia Makamu wa Rais Dk. Ali Mohammed Shein na Mawaziri Wakuu, Morgan Tsvangirai (Zimbabwe), Raila Odinga (Kenya), Meles Zenawi (Ethiopia) na Mizengo Kayanza Pinda (Tanzania).
Mkurugenzi wa WEF katika Afrika, Katherine Tweedie, alisema katika mkutano huo, pia wadau wengine katika uchumi na maendeleo ya jamii watakuwepo kujadili dhima inayosema `kurejerea mkakati wa ukuaji Afrika.
Alisema viongozi hao na washiriki wa WEF, pia watajadili masuala ya kijamii yatakayochagiza kupata msingi bora wa Afrika ya baadaye kwa mtazamo wa kidunia.Baadhi ya mada zitakazojadiliwa ni elimu ya juu, kurejerea ushindani barani Afrika, Waafrika bilioni moja ni fursa ama hatari?
Nyingine ni muingiliano wa kikanda, hali ya rasilimali za asili ifikapo 2030, vikwazo dhidi ya ukuaji wa fursa za Afrika, ushirikiano wa India na Afrika, vita, amani na haki ya ulinzi. Ratiba ya WEF inaonyesha kuwa Rais Zuma ataelezea kuhusu ujenzi wa Afrika Kusini wakati na baada ya mashindano ya Kombe ya Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Aidha, kutakuwepo na mada kuhusu Zimbabwe, ambayo pamoja na mambo mengine, itagusa hali ya baadaye kiuchumi, hususan baada ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa. Mjadala huo pia utachangiwa na Waziri wake Mkuu, Tsvangirai.
Rais Kikwete atashiriki mijadala kuhusu dira mpya ya kilimo barani Afrika na kufungua fursa za ukuaji uchumi barani.
Rais Guebuza wa Msumbiji atafungua warsha kuhusu mfumo mpya wa ushirikiano kwa maendeleo ya kiuchumi barani, wakati Odinga atashiriki kujadili sayansi na teknolojia dhidi ya uendelevu, ukuaji na maendeleo.
Pia Marais Zuma, Kikwete na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Makazi Duniani (UN-Habitat), Anna Tibaijuka, ni miongoni mwa watakaojadili mada ya ubunifu wa wajibu wa Afrika katika uchumi mpya wa dunia.
Mada muhimu ya demokrasia ya baadaye barani Afrika, itajadiliwa pia Raisi wa Bunge la Pan-African kutoka Afrika Kusini, Idirsaa Moussa.
Kimsingi, mkutano huo unawakutanisha viongozi wa kisiasa na watu wengine mashuhuri katika bara hili na hiyo inaleta matumaini kwamba mataifa ya Afrika sasa yamefikia mahali na kuona umuhimu wa kujadili masuala muhimu kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa watu wao kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Tunasema hivyo kutokana na miaka ya nyuma viongozi wa nchi na serikali za Afrika kukutana na kujadili kuhusu utatuzi wa migogoro iliyokuwa inatokana na vita.Tunawashauri wajumbe wa mkutano huo kuyajadili masuala yaliyopangwa kwa kina na kwa uwazi ili changamoto zitakazobainika ziweze kurekebishwa.
Baadhi ya nchi zinafahamika kwamba zinakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa utawala bora hivyo tunawashauri wawakilishi wake katika mkutano huo kupokea ushauri watakaopewa na kuufanyia kazi.
Nchi itakayokataa kupokea changamoto hizo, itakuwa inajidanganya kwa kuwa dunia ya leo ya utandawazi nchi yoyote haiwezi kupata maendeleo ya kiuchumi ikiwa itakaidi kuheshimu misingi ya demokrasia na utawala bora.
Matumaini yetu ni kwamba yatakayojadiliwa na kukubaliwa yatakuwa ni msimamo wa pamoja wa mataifa hayo. Tunawakaribisha wajumbe na tunautakia mkutano huo mafanikio.
CHANZO: NIPASHE