Wenje achangiwa samani za ofisi

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
WANANCHI wa Jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza juzi walichanga sh 179, 690 kwa ajili ya kununua samani za Ofisi ya Mbunge wa
Jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Ezekia Wenje.Fedha hizo zilichangwa wakati mbunge huyo alipokuwa akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Sahara jijini hapa kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa kumchagua.

Wananchi hao waliamua kuchanga fedha hizo baada ya mbunge huyo kueleza kuwa ofisi yake haina meza wala kiti na kwamba analazimika kuwahudumia wananchi akiwa amesimama kutokana na samani ambazo zikuwa katika ofisi hiyo kuchukuliwa na Mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Bw. Lawrence Masha kwa madai kuwa alinunua samani hizo kwa fedha zake.

Siku chache baada ya Bw. Masha kuachia madaraka hayo, iliyokuwa ofisi yake ilikuwa haina samani muhimu, ikiwamo picha ya Rais Jakaya Kikwete, simu ya mezani ilikatwa waya na kichwa chake kubebwa; vitasa, zulia, mafaili yenye nyaraka za maendeleo ya jimbo na mapazia.

Kutokana na hali hiyo, Bw. Wenje alikaririwa akisema: Niliwabana viongozi ngazi ya wilaya na mkoa wanieleze vimeenda wapi hivi vitu… niliambiwa eti vilinunuliwa na mtu binafsi na havikuwa vya serikali.Akihutubia mkutano huo juzi Bw. Wenje alisema kuwa Bw. Masha hakuwa na sababu ya kuchukua samani hizo kwa vile serikali kila mwaka ilikuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kuendesha ofisi hiyo na kuhoji kwamba kama alinunua kwa fedha zake, zile za serikali zilienda wapi kwa kipindi cha miaka mitano.

Akiwashukuru wananchi, Bw. Wenje alisema kuwa yeye amekuwa mbunge kwa sababu wananchi walikubali kupigwa mabomu na hata kupoteza maisha yao siku ya kutangaza matokeo, na si kwa sababu alipigiwa kura nyingi au nchi ni ya demokrasia.

Aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika Ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza siku ya kuwachagua Meya na Naibu Meya wa Jiji hilo ili washangilie ushindi, kwa vile chama chao kina wajumbe wengi wa kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi huo ambao wanakihakikishia ushindi wa kutwaa viti hivyo na kuongoza halmashauri hiyo.

"Sisi tuna wajumbe 17 ukiweka na diwani mmoja wa Chama cha Civic United Front (CUF) tunakuwa jumla 18 wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kina wajumbe 13 pekee, hivyo hatuna sababu ya kushindwa kupata kiti cha umeya na naibu meya," alisema Bw. Wenje.

Bw. Wenje alisema kuwa endapo Halmashauri ya Jiji la Mwanza itahitaji kuwaondoa wamachinga katika maeneo wanayofanyia biashara, inatakiwa kufanya nao mazungumzo badala ya kuwaondoa kwa nguvu, hali ambayo inaweza kusababisha kero kwa wafanyabiashara hao na wananchi wengine kwa ujumla.Alisema kuwa yeye amechaguliwa na maskini, hivyo ni lazima asimame mstari wa mbele kuwatetea wanyonge ambao ndio wapiga kura wake, ili wafanye shughuli zao za kujiletea maendeleo pamoja na familia zao bila usumbufu wowote.

Katika hatua nyingine, Mwandishi Wetu Rehema Mohamed anaripoti kuwa chama hicho kimesema kuwa hakuna mgawanyiko ndani ya chama hicho unaosababisha wanachama wake kutambuana kwa uvaaji wa sare za chama hicho kuwa wafuasi wa kiongozi fulani.

Akizungumza na gazeti hili, Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Bw. Erasto Tumbo alisema hoja hizo hazina mashiko kwa kuwa suala la mavazi linatokana na mapendekezo ya mtu mwenyewe.Bw. Tumbo alisema mtu anayeongozwa kwa mavazi ni yule aliyefilisika kifikra na anahitaji msaada kuondokana na hilo.

"Hoja hiyo haina mashiko yoyote, uvaaji wa fomu ni kutokana na mtu anavyopenda kuvaa, binadamu mwenye akili timamu hawezi kuongoza fikira zake kimavazi, mimi nina sare zote za mikono mirefu na mifupi, je, ni mfuasi wa nani kati ya hao?, alihoji Bw. Tumbo

Akizungumzia madai ya kuwepo kwa udini ndani ya chama hicho, alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kuwa anayepaswa kulisemea ni Bw. Zitto aliyedaiwa kulitamka.Kwamujibu wa taarifa iliyochapishwa katika baadhi ya vyombo vya habari jana ilibainishwa kuwa kuna mvutano wa uongozi ndani ya CHADEMA na kusababisha mgawanyiko wa wanachama kulingana na uvaaji wa sare za chama hicho.

Ilibainishwa kuwa wanachama wanaovaa sare za mikono mifupi ni wafuasi wa Naibu Katibu Mkuu, Bw. Zitto Kabwe na wale wanaovaa kombati za mikono mifupi ni wafuasi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Freeman Mbowe.

Lakini pia madai hayo yamekanushwa na Bw. Kabwe kwenye mtandao wake wa Wordpress.com kuwa habari hizo ni za kutunga zenye lengo la kugawa uongozi wa CHADEMA na kuleta mgogoro."Kumekuwa na habari kwenye magazeti kitambo sasa zenye kuonyesha mgogoro ndani ya CHADEMA. Napenda kuwajulisha marafiki zangu kuwa hakuna mgogoro wowote. Sihami wala sifukuzwi CHADEMA," alisema Bw. Kabwe.

Aliongeza kuwa, "Tuna kazi moja tu, nayo ni kuimarisha chama kuelekea 2015 wakati tukipigania mabadiliko ya katiba. Tusiyumbishwe!"
 
Back
Top Bottom