Waziri wa TAMISEMI, hili nalo liangalie kwa makini

Voice of wise

Member
Jul 2, 2023
14
9
Katika wizara ambazo zinakaba nchi kwenda mbele ni pamoja na hii ya TAMISEMI. Wizara hii ndiyo imekamata majukumu makuu ya kiuchumi kuanzia chini kabisa ngazi ya wananchi wazalishaji vijijini, miji midogo, miji ya wilaya, hadi miji ya mikoa. Ni wizara nyeti sana kwa maendeleo na ustawi wa wananchi. Imeshika sehemu kubwa sana ya mstakabari wa nchi.

Lakini shida yake kuu ni aina ya baadhi ya watumishi ilionao. Kama vile hawajitambui au wamejitoa ufahamu au hawana sifa ya kufanyakazi serikalini. Utendaji wao hauridhishi kabisa.

Kwa leo nizungumzie tu suala la utawala bora; niachane kwanza na suala la huduma kwa wateja ambalo nalo ni balaa zaidi. Eneo la maafisa utumishi limulikwe vizuri. Watu hawa wanaroho mbaya kama ya wanyama wala nyama.

Kero yangu hapa kwenye eneo hili kwa leo ni kuhusu ukiritimba wa uhamisho wa watumishi, hususan waalimu. Moja ya haki za mtumishi ni kuhamishiwa eneo aliloomba kwa ajili ya kutatua matatizo yake ya kifamilia, ili mradi yawe ya ukweli na uhakika. Lakini mwalimu anaweza akaomba uhamisho leo akiwa na umuhimu wa kuhamia alikoomba kwenda kwa haraka. Tena anaomba kuhama kwa gharama zake binafsi. Kwa utaratibu wa zamani, anapitisha barua zake vizuri huku kwenye ngazi ya shule, wilayani hadi halmashauri anayokwenda bila matatizo yoyote. Kisha anaikabidhi mkoani ili ipelekwe wizara ya TAMISEMI kwa uamuzi wa mwisho.

Ngoma ndiyo inaanzia hapa TAMISEMI. Mwombaji atakaa anasubiri kwa matumaini wee hata miaka 10 inaweza kupita hapati barua ng'oo. Hakuna cha feedback kwamba barua imepokelewa inafanyiwakazi na utapewa majibu ndani ya kipindi fulani, wala kwamba ombi lako halijakubaliwa kwa sababu Fulani. Atakaa anasubiri hajielewi yuko upande gani na hata kiongozi wake atabaki njiapanda katika kumpangia majukumu. Huko TAMISEMI haya wala hayawaumizi kichwa. Wanajifanya hayawahusu kabisa.

Inasemekana, hali hii inawafaidisha hao wahusika na maamuzi ya mwisho, ndiyo maana hawazipitishi kwa wakati. Ni mazingira ya rushwa yametengenezwa ili waombaji wajipeleke huko wizarani kwa ajili ya "kunyolewa". Hapo ndiyo unakuta walioomba nyuma na wakajipeleka kwa kinyozi wanafanikiwa kuhama na kuwaacha wanaojifanya wazalendo wakibaki kusubiri kudra za mwenyezi Mungu. Wakijaribu kuulizia wataambiwa, vumilia awamu ijayo unaweza kupata. Awamu ijayo ikifika wanaambiwa walipitishiwa wale wa kubadilishana tu au faili lako lilisahaulika n.k.

Hapa ndipo mimi ninapojiuliza maswali mengi yasiyo na majibu:

-Hivi watanzania mbona tunaroho mbaya namna hii? Hata hatuthaminiani. Inapendwa pesa kuliko utu na maendeleo ya nchi
-Ni nani aliyeturoga? Mbona hatujitambui hata kidogo?
-Ni lini tutarudi kwenye mstari ili nchi iweze kupiga hatua kwa haraka?
-Ni nani wakutukomboa kutoka katika mkwamo huu?
-Hivi mtumishi anayefanyiwa hivi atakuwaje na moyo wa kuipenda kazi yake? Alikuwa anamatatizo yake yakifamilia kuanzia alipoandika barua sasa kwa nini acheleweshwe kwa miaka mingi?
-Hivi wanaofanya hivi wanaijua dhamana waliyonayo kwa wananchi?
-Hivi hawana hata hofu ya Mungu? Unachukuaje rushwa kwenye haki ya mtu jamani.
-Hivi makatibu wakuu wanawalindaje? Au na wao ni sehemu ya syndicate hii?
-Kama watumishi muhimu wanafanyiwa hivi je hao wakulima inakuwaje?

Hapa ndipo ninapomlilia waziri mh. Mchengerwa ambaye anaonekana yuko serious na mambo ya nchi. Na anaitafsri vizuri falsafa ya mh. Rais mama yetu mpendwa. Namuomba afanye jambo la maana hapa. Najua ni tatizo ambalo makatibu wakuu wangekuwa serious wangelitatua haraka tu. Lakini wameshindwa kufanya hivyo kwa sababu wanazozijua wao. Kwa hiyo mh. Waziri inabidi aingilie kati. Lakini naomba asikurupuke ila afanye utafiti mdogo tu. Asiende wizarani maana atadanganywa, aende mashuleni akaongee na walimu walioomba uhamisho wamwambie madhira yao kwa uwazi bila kuogopa. Atajifunza mengi yatakayomwezesha kufanya maamuzi sahihi.

Haya ni baadhi tu ya matatizo ya watumishi wa wizara hii nyeti. Yanaweza kufanana na ya wizara nyingine pia. Shida ni nyiingi na kubwa mno mno mno. Ila hili la uhamisho lishughulikiwe. Walimu wengi wanateseka nalo na linawavunja moyo wa kazi. Elimu ni ufunguo wa maendeleo. Tukiipuiza, tutabaki kuwa Taifa la wajinga wengi. Na wajinga ndiyo waliwao.

Ni mimi mwananchi niipendaye nchi yangu Tanzania

The voice of wise
 
Uhamisho ni changamoto iliyowashinda mawaziri wengi,akiwemo huyu mchengerwa
 
Back
Top Bottom