Waziri wa Fedha afichua siri ya watu ‘kuchacha’

Waziri wa Fedha afichua siri ya watu ‘kuchacha’

kirerenya

JF-Expert Member
Joined
Aug 27, 2013
Posts
1,699
Reaction score
2,262
KUCHACHA.gif

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema licha ya nchi kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa Pato la Taifa, umekuwa hauonekani katika maisha ya watu walio wengi kutokana na kasi ndogo ya ukuaji wa sekta ya kilimo iliyo chini ya wastani wa asilimia tatu.

Hivyo, amewataka wachumi kuhamasishana kutafuta nafasi za ubunge ili wasaidie wananchi na Taifa wakiwa bungeni.

“Kule tulipo mimi na mheshimiwa Mwigulu, ikitokea Mwiguku katoka wachumi waliopo pale wanahesabika, lakini sehemu kama ile ya kutungia sheria halafu wachumi ni wachache mimi naona ni shida, lakini chombo hiki kinaweza kushawishi kupatikana kwa wachumi wengi ili kunyoosha mambo,” alisema Dk Mpango.

Alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Jumuiya ya Wachumi Tanzania (EST) katika ukumbi wa Benki Kuu (BoT) jijini Dar es Salaam akiwa mgeni rasmi.

Dk Mpango alisema anaamini kupitia jukwaa hilo wachumi watahamasishana kutafuta nafasi ya kuingia bungeni ili kusimamia mipango ya uchumi ya nchi.

Waziri Mpango alisema changamoto nyingine ya ukuaji wa pato ni ukosefu wa ajira kwa asilimia 10.3 na kiwango cha umaskini kwa asilimia 15, huku ongezeko la watu likiwa asilimia 2.7 kwa mwaka. “Sekta ya fedha imekumbwa na msukosuko wa kuongezeka kwa mikopo chechefu kwa asilimia 12.5 licha ya kiwango cha BoT kuwa ni asilimia tano; riba za kukopa kuwa juu; ongezeko dogo la kiwango cha mikopo na baadhi ya biashara kudorora hasa zile ambazo zilikuwa hazilipi kodi na zenye madeni makubwa,” alisema Dk Mpango.

Nyingine alisema ni wabia wengi wa maendeleo kutoka nje ya nchi kuchoka kutoa misaada ya kibajeti; kuongezeka gharama za mikopo katika benki na taasisi za kifedha za kimataifa na ulaghai unaotekelezwa na kampuni ya uwekezaji kupitia mikataba isiyo na tija kwa Taifa.

Dk mpango alisema ameeleza hayo ili kuwapa wachumi nafasi kupitia EST kufikiri namna watakavyokusanya nguvu na maarifa katika kuongeza kasi ya kuibadilisha Tanzania kuwa kitovu cha uchumi katika bara la Afrika kupitia weledi wao, bidii, uzalendo, uwazi na uwajibikaji.

“Ningependa kuona jumuiya ya wachumi ambayo inajinasibisha kwa umahiri wa kukuza tafiti za kiuchumi, maendeleo ya nchi, mafunzo kwa wachumi kazini, kuratibu jukwaa la mijadala kuhusu sera za kiuchumi, kuibua mawazo mbadala yanayotekelezeka kwa ajili ya kuiinua nchi na kuratibu mifumo ya mahusiano na wachumi wengine,” alisema Dk Mpango.

Awali, Gavana wa BoT, Profesa Florens Luoga alisema hatua ya kurejeshwa kwa jumuiya hiyo ambayo ilikuwa imekufa tangu mwaka 1999 imekuja wakati muafaka kwa kuwa nchi ilikosa jukwaa la kujadili na kuangalia mwelekeo wa uchumi na maendeleo, kutoa tahadhari au ushauri kwa wakati ili kusaidia pale mambo yanapokwenda sivyo.

“Chama cha wachumi ni nyenzo muhimu ya kukuza na kuhakikisha uhai wa wachumi kama ilivyo kwa taaluma nyingine kama vile wanasheria, wahandisi na wahasibu. Chama hiki kinapaswa kuhakikisha uadilifu na elimu endelevu kwa wanachama na hata kuimarisha mafunzo ya uchumi,” alisema Profesa Luoga.

Mwenyekiti wa kamati ya kufufua jumuiya hiyo Geoffrey Mwambe ambaye pia ni mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) aliwaomba wachumi kuiombea jumuiya hiyo iliyosajiliwa kama taasisi isiyo ya kiserikali idumu.

Alisema itakuwa na jukumu kubwa la kusimamia ustawi wa uchumi katika nchi.

“Tutakuwa na jukumu la kuwakilisha maoni ya wachumi, kujadili changamoto za sekta ya uchumi na kuzitafutia ufumbuzi kupitia utafiti, mijadala na uchambuzi wa sera. Tutakaa mbali na sababu zilizosababisha kifo cha jumuiya ile iliyoanzishwa mwaka 1966,” alisema Mwambe.


Chanzo: Mwananchi
 
uchumi mnauua nyinyi wenyewe hamtaki kuambiwa ukweli nyinyi maliwali wa dikteta uchwara wenu.

Kila kitu mnafanya kwa kufuata maelekezo toka juu

kama hamna hela kachapisheni ni maelekezo yangu yafuateni
 
Hata wakijaa bunge zima wachumi hakuna lolote kama bunge litashindwa kukaa kando na serikali na kutenda kazi yake ya kuisimamia serikali kwa kigezo cha chama tawala ni bure tu kama viongozi Wa bunge wataegemea kwenye chama zaidi kuliko kusimamia rasilimali na kufuatwa kwa utaratibu Wa sheria za nchi
 
Dk mpango alisema ameeleza hayo ili kuwapa wachumi nafasi kupitia EST kufikiri namna watakavyokusanya nguvu na maarifa katika kuongeza kasi ya kuibadilisha Tanzania kuwa kitovu cha uchumi katika bara la Afrika kupitia weledi wao, bidii, uzalendo, uwazi na uwajibikaji.

[emoji115] tutalifanyia kazi
 
Au ndio imesababisha watumishi wa serikali ngara hawajapata mshahara wa mwezi wa pili hadi leo?
 
Kama anamkubali Mwigulu basi siyo mbaya wakibadirishana nafasi, Mwigulu awe Waziri wa Fedha yeye akawe waziri wa mambo ya ndani nadhani itapendeza
 
Wafadhili hawajachoka,bali wamekata misaada baada ya kuona kanuni za utawala bora zinavunjwa waziwazi bila kutambua haki ya mtu mwingine
 
Wananchi tuna makosa makubwa, hatuangalii elimu ya mtu anapoomba kura. Akishajua ujanja wa kuongea na mbwembwe nyingi anapita. Siku tukijua kuchambua hali ya uchumi itabadilika. Baba wa taifa alijua akaweka nafasi za wabunge wa kuteuliwa ili tukichagua wote vilaza awake watu wa kuwapa kazi maalumu zinazohitaji usomi wa hali ya juu. Je utampa uwaziri darasa la saba?? Ningetamani mawaziri kwani ni wasemaji wa wizara husika wawe professor. Yule mwenye vision na weledi
 
Point ya msingi niliyoiona ya mpango ni kuhusu bunge kujaa ma mbumbumbu, ni wakati sasa wasomi tena vijana wanaojielewa (sio mabashite) washike hatamu bungeni, kinyume na hapo hata uwe profesa ukiwa kule bungeni unashuka hadi levo za kina nkamia ili muongee lugha moja.
 
Hata uwe professor wa uchumi, si utakuwa ni CCM? WEWE NI KUSUBIRI KUSEMA NDIYO TU.

Mwigulu amewahi kusaidia nini katika michango yake kuhusu uchumi? MTU anayeongelea uchumi kama uchumi kwa uhalisia na takwimu ni zitto, na bashe sometimes. Huyo mwigulu ni kituko tu.
 
Mpango ana logic ya ajabu kweli. Cha msingi ni nchi kuwa na wachumi wa kutosha kwa kiwango kinachotakiwa na serikali kupata ushauri toka kwao. Wakisha ingia bungeni wengi uchumi wao huweka kando. Hata huyo Mwigulu anaemsema yeye sijui kama ana muda wa kupiga mada za kichumi wakati anatarajiwa kuongoza usalama na ulinzi wetu 24/7. Yeye atumie nafasi yake kuwapa wachumi sauti katika utengenezaji na utekelezaji wa sera na sio lazima wawe bungeni kama wabunge. Pamoja na hayo awaulize wachumi faida na hasara za serikali kukomaa kufanya biashara na serikali yenyewe? Lingine wanashaurika huko?
 
Ana point nzuri ila tatizo wanaingiliwa na siasa. Tumeona ma prof ana dkt wenye phd wakiwa nje wanakuwa na maono yenye nguvu. Lakin wakisha ingia bungeni wanakuwa wajinga.
 
Mpango ya serikali inapangwa serikalini ambako Wachumi wamejaa na wengine hawana kazi za kufanya. Hiyo kazi anayotaka kuwepo wabunge siyo yao.

By the way Zitto ni Mchumi ... Kitwanga ni Mchumi!!
 
Ujinga ukonga tu,nilijua anasuruhisho,kumbe ni ushauri na kulalamika tu!!
 
kirerenya Kwa maana hiyo wachumi wakiingia bungeni kwa wingi ndio jibu la kukuza kilimo !!!??? Duuuhh Tanzania na watu wake kwelii Mungu tusaidie .Amina
 
Back
Top Bottom