Waziri Mkenda: Tutawekeza nguvu katika utafiti wa mbegu kuboresha kilimo nchini

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema katika bajeti ya Wizara yake ya 2021/2022 imeweka mkazo katika masuala ya utafiti wa kilimo na kuongeza uboreshaji wa ugani ili kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo.

Prof. Mkenda ameyabainisha hayo jijini Dodoma wakati akifunga Kikao cha maafisa kilimo na wadau wa huduma za ugani nchini waliokutana Dodoma ikiwa ni kutafuta mbinu za kuboresha kilimo hapa nchini amesema ili kuwa na kilimo chenye tija taifa linatakiwa kuwekeza katika utafiti ili kuongeza ufanisi katika sekta hiyo.

“Katika bajeti ijayo tutahakikisha kuwa tunaweka kipaumbele katika masuala ya utafiti hata ikibidi kupunguza baadhi ya matumizi kama vile ununuzi wa magari pamoja na posho” amesema Prof. Mkenda

Prof Mkenda amebainisha kuwa kuwekeza kikamilifu kwenye utafiti utasaidia kupatikana kwa mbegu bora ambazo zitaongeza uzalishaji na kuliondolea taifa utegemezi wa bidhaa za kilimo kutoka nje.

Amesema kuwekeza katika utafiti kuna manufaa kwa sababu mfano zao la Michikichi kwa nchi kama Malaysia kwa Hekta moja wanavuna tani 10 lakini hapa Tanzania ni tani 1.6 kwa hekta moja lazima tujue kwanini.

“Kwa hali hii huwezi kushindana na watu hawa ambao wanalima kisasa sawa na wewe lakini wanavuna zaidi hivyo tunahitaji kufanya utafiti ili kupata mbegu bora ambazo zitaongeza uzalishaji tofauti na ilivyo sasa”amesema.

Kwa upande wake mjumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Livingstone Lusinde ambaye ni Mbunge wa Mvumi, amesema kuwa ili kuifanya sekta kilimo kuwa na tija mageuzi makubwa yanahitajika katika sekta hiyo.

Pia Mhe. Lusinde amebainisha kuwa kutokana na umuhimu wa kilimo nchini suala hilo linahitaji utekelezaji wa kina kama ilivyoahidiwa katika ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM kwa wananchi walipoomba ridhaa ya kuwekwa madarakani.
 
Back
Top Bottom