Waziri: Mgawo umekwamisha biashara yangu

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Imeandikwa na Dativa Minja; Tarehe: 2nd August 2011

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, amesema mgawo wa umeme umesababisha shughuli zake za ujasiriamali kudorora.

“Mimi nimekwama biashara yangu ya kuoka mikate kutokana na tatizo la umeme, nimepata hasara kubwa ya kumwaga unga wa ngano baada ya katizo la umeme wakati mashine inaendelea kuumua mikate,” amesema Dk. Chami.

Dk. Chami alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, alipokuwa akishawishi wafanyabiashara kukabiliana na changamoto za biashara wakati wa kufunga mafunzo yao ya ujasiriamali.

Mafunzo hayo yalihusisha wafanyabiashara 673 na yaliandaliwa na Shule Kuu ya Biashara Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Safari ya ujasiriamali si rahisi, inahitaji ujasiri na lazima ukubali faida na hasara na uwe na moyo wa chuma,” alisema Dk. Chami.

Akijitolea mfano, waziri alisema; ”mashine (ya kuoka mikate) ni kubwa na uwezo wa kununua jenereta kubwa sina na wakati huo natakiwa kurudisha mkopo wa kufungua tanuri mikate.”

Alifafanua kwamba ujasiriamali ni safari ndefu ya kuufikia utajiri ambayo inahitaji kutokata tamaa na kutumia fursa za biashara zilizopo.

Aliwataka wajasiriamali wadogo na wa kati, wasiogope kufanya biashara kwa kuwa ndio mwanzo wa mafanikio na kuwa hata wamiliki wa viwanda vikubwa Tanzania walianzia huko.

Dk. Chami alisema anapenda ujasiriamali na anapoona sehemu yenye fursa ya biashara, hawezi kuiacha bali huitumia kikamilifu na kinachotakiwa kwenye biashara ni uaminifu.

Akitolea mfano alivyoanza biashara yake ya kwanza, alisema alianza kufuga kuku wa mayai akiwa jijini Dar es Salaam, lakini biashara ilikufa baada ya maji kutatika kwa muda mrefu.

Alisema yeye alikuwa mtu wa kwanza kutoa huduma ya chakula pale Chuo Kikuu cha Dodoma na alianzisha duka la vifaa vya ofisi.

“Nilianza kufuga kuku wa mayai pale Gongo la Mboto, nikaweka vijana wa kunisaidia kazi pamoja na kupeleka mayai kwa wateja mjini. Lakini walikuwa wakiniibia, nikinunua chakula cha kuku magunia 50 wao wanauza magunia 20 wanalisha kuku magunia yaliyobaki na maji yalipokatika biashara ikafa.

“Duka la kwanza pale UDOM la kugawa chakula ni la kwangu na familia yangu hata ukienda pale utakuta duka kubwa la vifaa vya ofisi iliyoonadikwa Junior Stationery ni la kwangu hilo,” alisema.

Akisimulia alivyoanzisha tanuri mikate, Dk. Chami alisema baada ya kuona chakula hakinunuliwi sana na wanafunzi wengi wanakula mikate na soda, aliona hiyo ni fursa nyingine ya biashara.
“Nikatafuta mkopo nikafungua tanuri mikate hilo ila shida ilikaja pale umeme ulipanza kusumbua. Wakati kwenye mashine naumua kilo 70 za ngano mashine nyingine inakoroga unga mwingine kilo kama 80. Ukiangalia hatua zote nilipata hasara ya kilo kama 200 hivi,” alisema Dk. Chami.

Alisema baada ya kuona anazidi kupata hasara, aliamua kutengeneza bwawa la samaki ili umeme unapokatika unga ukiharibika anawapa samaki.

Alifafanua kwamba aliwaambia wajasiriamali historia ya biashara zake na changamoto alizokutana nazo ili kuwatia moyo na kuwaasa kwamba wanapokutana na matatizo magumu na changamoto katika biashara, watafute mbinu za kuyatatua bila kurudi nyuma.

Aliwataka wajasiriamali hao kwenda Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) kupata mkopo na kwamba faida kubwa ya mkopo katika shirika hilo ni kukopeshwa na kusimamiwa hadi wasimame wenyewe na kupata masoko.

Dk. Chami alisema matarajio yake wakati wa kustaafu siasa ni kumiliki kiwanda kikubwa nchini. Alisema yuko mbioni kufunga mashine ya kukamua mafuta ya alizeti.

Alisema kwa kutumia fedha atakazolipwa za kiinua mgongo wakati wa kumaliza kipindi chake cha ubunge, atanunua mashine ya kusagisha na kukoboa na kuwa na shamba la mifugo, ili auze mashudu na pumba na pia apate chakula cha mifugo wake.

Akijibu ombi la wajasiriamali hao kutaka Serikali iwafikirie kuwakopesha Dk. Chami alisema hicho ni kitu kisichowezekana, kwa kuwa Serikali kumkopesha kila mjasiriamali labda siku Mungu atapofungua bomba la mafuta Tanzania, ndipo itakapowezekana.
 
inavutia sana, inatia moyo kwa sisi wajasiliamali underground - hongera DR. Chami kutupa uthubutu wa kutokwepa au kukata tamaa endapo vikwazo kama hivi vinapotutokea wakati wa uendeshaji hizi biashara ndogo ndogo.
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom