Waziri Mbarawa aitaka TTCL kufanya biashara ya uhakika

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ameitaka kampuni ya simu ya TTCL kutumia vizuri mkongo wa taifa kufanya biashara ili kuiwezesha kushindana katika soko na kuiongezea Serikali mapato.
Akizungumza mara baada ya kukagua mitambo ya TTCL mkoani Mtwara Prof. Mbarawa amesema kwa kuwa kampuni hiyo sasa ni ya Serikali kwa asilimia mia moja inatakiwa kufanya biashara kwa kuongeza wateja wapya na kuhakikisha inapata fedha nyingi zitakazotokana na wateja wengi kuunganishwa.
“Hakikisheni mnaunganisha wateja wakubwa katika mkongo wa taifa wa mawasiliano kama vile Benki, Viwanda, Mifuko ya Hifadhi Jamii na vyombo vya habari ili huduma ya mawasiliano hapa Mtwara na kwingineko nchini iwe ya uhakika na hivyo kukuza uchumi wenu binafsi na Taifa”, amesema Prof. Mbarawa.
Kwa sasa Kampuni ya TTCL inamilikiwa na Serikali kwa asilimia Mia moja baada ya kuilipa kampuni ya BAT Airtel shilingi Bilioni 14.9 kuondoa ubia uliokuwepo hapo awali ambapo kampuni hiyo ilikuwa ikimilikiwa na Serikali kwa asilimia 65 na Bat Airtel kwa asilimia 35.
Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Dkt. Kamugisha Kazaura amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa kampuni hiyo imejipanga kutumia fursa ya mkongo wa taifa wa mawasiliano kufanya biashara nchini kote na kuongeza gawio kwa Serikali.
Katika hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amekagua Bandari ya Mtwara na kuwataka viongozi na wafanyakazi wa bandari hiyo kufanya kazi kwa ubunifu ili kuvutia wafanyabiashara kutumia bandari hiyo na kuhakikisha meli zinazoshusha bidhaa hapo zinahudumiwa kwa wakati.
Ametaka Wafanyakazi wa bandari kuwa waadilifu na wawazi ili kazi yao kuwa kwa manufaa ya taifa na sio binafsi ili kujenga taswira nzuri kwa jamii hapa nchini.
“Nawahakikishia hatutamuonea mtu wala hatutamwachia mtu mbadhirifu kutia hasara taasisi hii muhimu kwa nchi tunafanya hivyo ili kutenda haki kwa watanzania wote”, amesistiza Prof. Mbarawa.
Ameitaka Mamlaka ya Bandari kukusanya shilingi trilioni moja kwa mwaka mpya wa fedha kutoka bilioni 600 ilizokuwa ikikusanya mwaka huu na kusisitiza umuhimu wa kutenda kazi kwa ubunifu na weledi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Bandari Mkoani Mtwara (Dowota) Bw.Abilahi Darusi amemueleza Waziri Mbarawa kuwa kwasasa wafanyakazi wengi wa bandari wanafanya kazi kwa hofu hivyo ni vyema Waziri akakutana na makundi ya wafanyakazi ili kuelezwa hali halisi ya Bandari nchini.
Naye Capten Mkuu wa Bandari Mtwara Hussein Bakari Kasuguru amemueleza Waziri Prof. Mbarawa kuwa kwa sasa meli zinazotia nanga katika bandari ya Mtwara ni kubwa hivyo aangalie umuhimu wa kujengwa eneo kubwa la kuegeshea Meli hizo ili kuendana na mahitaji ya sasa.
Bandari ya Mtwara inayohudumia Lindi na Zanzibar ilijengwa mwaka 1950 na ina gati lenye ukubwa wa mita 385 na kina cha mita 9.8 na inahudumia tani zaidi ya laki mbili na mia tano sabini na sita kwa mwaka.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO​
 
Wapewe malengo na si kuwabembeleza bana..kila miaka nasikia wanakopa tuu sioni chochote zaidi ya kushuka zaidi..wanakopesheka mpaka 40bilioni lakini wenyewe hawana mbinu mbadala wa kuitoa hapo..
 
Wapewe malengo na si kuwabembeleza bana..kila miaka nasikia wanakopa tuu sioni chochote zaidi ya kushuka zaidi..wanakopesheka mpaka 40bilioni lakini wenyewe hawana mbinu mbadala wa kuitoa hapo..
lini walikopesheka tangia 2001 kama sio juzi tu 2016, acha kuropoka au umetumwa na makaburu nini
 
Napendekeza (Kwakua viongozi wengi akiwpo rais wa nchi ni member humu) kua viongozi na taasisi zote za serikali wawe wateja wa simu za mkononi za TTCL, wote ambao bills zao za simu hulipiwa na mwajiri wao (serikali) basi bills hizo ziwe kwa TTCL na sio Voda, Airtel wala tiGo; hivyo ndiovyo nchi zingine zinazojali Uzalendo hufanya. Hatuwezi kuhubiri uzalendo kwa maneno, let actions speak louder than words.
 
Mkuu wazi wazi lugha ya matusi sio nzuri mkuu..hatupo kushindana kutukana humu..makaburu navyowachukia unasema ndio wamenituma tena duu haya bwana..
 
Kaburu ni mbaguzi sana miaka ya nyuma niliishi cape town na kufanya kazi katika oil Rig zao za kuchimba mafuta wanawabagua sana watu weusi wa kule wanaishi katika maisha ya taabu mpaka kesho..hao hao wanakuja kuzoa madini yetu huku na kwenda nayo kule..kuna baadhi ya makampuni tena makubwa wafanyakazi weusi ni wachache wanaona bora wawe na wageni kuriko weusi wa kule..stellenbosch university ndio kabisaa na kuna kipindi walikua wanafundisha kwa kutumia lugha ya Afrikaans tuu..kaburu msikie ni mbaguzi kupita maelezo..na South Africa tusi kubwa ni kumwambia mtu kibaraka wa Kaburu..
 
Back
Top Bottom