singidadodoma
JF-Expert Member
- Nov 11, 2013
- 4,394
- 1,536
Sehemu ya jengo ambayo inaonekana imepasuka.
WAZIRI wa Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewaagiza watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala na Shirika la Nyumba la Taifa kubomoa jengo refu lilojengwa chini ya kiwango lililopo katika mtaa wa Indira Ghandhi ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa.
Lukuvi ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam kabla ya kuelekea kwenye ziara fupi katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani ambapo nako pia amebaini matatizo mbalimbali katika sekta ya Ardhi.
“Miezi sita iliyopita Rais Mstaafu alikuja hapa akaagiza jengo hili libomolewe na nyie mkajiridhisha kweli lafaa kubomolewa sasa inakuwaje mpaka leo linaendelea kuwepo? Naagiza mfanye haraka jengo hili ndani ya mwezi mmoja taratibu za ubomoaji ziwe zimeanza ili kulinusuru taifa kuingia katika janga jingine.”alisema Waziri Lukuvi.
Akiwa bagamoyo waziri Lukuvi alibaini katika Wilaya ya Bagamoyo upotevu wa viwanja vya wanachi ambavyo walitakiwa kupewa katika eneo la ukuni ambapo vimetoweka
Mara baada ya kupata taaarifa hiyo mmoja wa wakaazi wa bagamoyo ambaye alitoa malalamiko juu ya viwanja hivyo mbele ya mkutano wa hadhara na kutaja kuwa Halmashauri ilichukua kiasi cha pesa kuanzia laki sita kwa kila mtu mwaka 2005 na kuahaidi kuwapatia viwanja lakini mpaka leo hawajapewa.
Mara baada ya kupata taarifa hiyo waziri Lukuvi aliwagiza watendaji wa wilaya hiyo ndani ya miezi sita wawe wamewapatia wakazi hao viwanja hivyo.
- Taarifa hii ya agizo la Waziri imepatikana kupitia blogu ya Michuzi
Habari inayohusiana na jengo hilo kama ilivyochapishwa kwenye gazeti la serikali, HabariLeo Agosti 20, 2015 inasomeka hivi...
ACHOMOA KUBOMOA JENGO PACHA
UBOMOAJI wa jengo pacha lenye ghorofa 16, lililopo mtaa wa Indira Ghandi Dar es Salaam, imeshindikana.
Imeelezwa kuwa mkandarasi aliyepewa kazi hiyo amebadili msimamo wake dakika za mwisho kwa madai kuwa, kazi ya kubomoa ni ngumu na yenye madhara kwa majengo yaliyo jirani.
Hayo yamebainishwa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngurumi wakati akizungumzia hatua zilizofikiwa wa ubomoaji wa jengo hilo, kufuatia kubainika kuwa limekiuka sheria za mipango miji.
Mngurumi alisema mmiliki wa jengo hilo baada ya kupewa taarifa ya kulibomoa alikimbilia mahakamani, na kwamba kesi hivi sasa imesikilizwa na imeisha na maamuzi ni kwamba jengo hilo linapaswa kubomolewa.
Alisema Manispaa ya Ilala ilitangaza zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi atakayeweza kubomoa jengo hilo, na kwamba katika zabuni hiyo, alijitokeza mkandarasi mmoja kampuni ya kichina ya CRJ, ambapo ilikubali kazi hiyo, ila ilijitoa dakika za mwisho.
Aliongeza, wao hawawezi kulibomoa kwa kuwa hawana ujuzi wa kazi hiyo na kwamba kinachofanyika hivi sasa ni Manispaa hiyo inazungumza na Bodi ya Wakandarasi Nchini (CRB), kuangalia kama wanaweza kumpata mkandarasi mwenye sifa na uwezo wa kufanya kazi hiyo ya ubomoaji.
Kubomolewa kwa jengo hilo, kunatokana na kuporomoka kwa jengo lililokuwa jirani na hilo ambalo lilisababisha vifo vya watu 36, na kujeruhi wengine 18, tukio lililotokea Machi 29 mwaka 2013.
Hata hivyo, sababu za kuporomoka kwake zilitokana na kujengwa chini ya kiwango lakini pia ukiukwaji wa sheria kwa kuongeza idadi ya ghorofa kutoka ghorofa nane zilizoidhinishwa kisheria hadi ghorofa kumi na tano.
Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, inatoa maelekezo kwa mwekezaji yeyote anayetakiwa kufanya ujenzi wa mradi wowote ambao ni zaidi ya ghorofa tano, lazima aombe kibali cha tathimini ya mazingira katika ofisi hiyo.
Mara baada ya tukio hilo, la Machi 29, Aprili 5 mwaka 2013, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka aliyeambatana na wajumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira walitembelea eneo hilo na kutoa siku 30 kwa mmiliki wa jengo hilo, Ally Raza kulibomoa baada ya kubainika kujengwa chini ya kiwango na sehemu isiyo zingatia mipango miji.
Kulingana na sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999, kifungu cha 44 na 45 na pia kanuni za ardhi za 2001 inaelekeza mhusika aliyekiuka masharti ya uendelezaji anapaswa kupewa ilani ya kubomoa na akiendelea kukaidi amri analipa faini ya asilimia mbili.
Hata hivyo, mmiliki huyo alikaidi na kukimbilia mahakamani kufungua kesi ya kupinga kubomolewa kwake, kesi ambayo imeisha na hukumu yake ni jengo hilo linapaswa kubomolewa.