Watembea kilometa 10 kufuata huduma za afya

mdau wetu

JF-Expert Member
Apr 20, 2011
548
58
WAKAZI wa Kijiji cha Chabu wilayani Ileje wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 10 kufuata huduma ya afya baada ya kutofunguliwa kwa zahanati waliyoijenga miaka sita iliyopita.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa asasi ya kiraia ya MIICO, Catherine Mlagha alisema hayo juzi alipokuwa akielezea matokeo ya utafiti uliofanywa wilayani hapa na asasi hiyo kuhusu Mpango wa Utekelezaji na Uwajibikaji kwa Umma (SAM).

Mlagha alisema utafiti huo ulilenga sekta zilizoonekana kusahaulika za kilimo na afya na ndipo ilipobainika upungufu, ikiwemo miradi ya Serikali iliyokamilika kutoanza kuwanufaisha walengwa kwa wakati muafaka.

Alisema kutofunguliwa kwa zahanati hiyo ni changamoto kubwa kwa watendaji wa kijiji na kata wanaopaswa kuwahamasisha wananchi kujitoa katika kuchangia miradi mingine ya maendeleo.

Ofisa huyo baada ya kubaini hali hiyo, walimfuata Mganga Mkuu wa wilaya hiyo aliyejibu kuwa zahanati hiyo licha ya kuwekwa jiwe la msingi na kuzinduliwa bado haijasajiliwa hivyo haiwezi kufunguliwa hadi mchakato huo utakapokamilika.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Chabu, Timoth Mwitega alisema wananchi walijitoa kwa hali na mali kuchangia ujenzi wa zahanati hiyo iliyojengwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Mbali na zahanati hiyo, pia wananchi kwa kushirikiana na mfuko huo walijenga nyumba mbili za wauguzi ikiwemo moja iliyokwisha kukamilika.

Mwitega alisema kutokana na muda mrefu kupita tangu kukamilika kwa ujenzi wa zahanati hiyo hivi sasa wananchi wanahoji Serikali ina mpango gani nao, kwani wanaendelea kutembea umbali mrefu huku baadhi wakilazimika kuvuka mpaka na kwenda katika zahanati zilizopo kwenye vijiji vya Malawi.
 
Back
Top Bottom