Watanzania wenye ulemavu 'dili' Kenya

BabuK

JF-Expert Member
Jul 30, 2008
1,845
329
BAADA ya nguvu kubwa kufanikiwa kutuliza wimbi la ukatili dhidi ya albino, sasa balaa ya unyanyasaji limewageukia watoto wenye ulemavu wa kawaida, ambao wamejikuta wakivushwa hadi nje ya nchi kufanyishwa kazi ya kuombaomba mitaani.

Moja ya matukio hayo yameripotiwa hivi karibuni, baada ya Mtanzania na mkewe ambaye ni raia wa Kenya kunasa katika mtego wa Polisi katika Jiji la Nairobi, Kenya.

Mtu huyo aliyetajwa kwa jina la Jisena Kulwa Dutu na mkewe, Josephine Mueni, waliburutwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Makadara, kwa kuwaingiza kinyemela nchini humo watoto walemavu wa miguu na kuwageuza mradi wa kujiingizia kipato kwa kuwafanya ombaomba.

Habari za uhakika kutoka chanzo chetu cha habari zinasema, watoto hao walemavu wamekuwa wakitumikishwa kwa kusambazwa katika vituo mbalimbali ili kuomba fedha.

Nyakati za asubuhi, gari maalumu liliwasambaza katika mitaa ya Jiji la Nairobi na kuwapitia jioni, ikiwa ni pamoja na kukusanya kivuno cha siku.

Madai hayo yalithibitishwa pia mahakamani baada ya watuhumiwa hao kufikishwa hapo. Mbele ya Hakimu Terry Ngugi, ilibainika walemavu hao walikuwa wakisafirishwa kinyemela kutoka Bariadi, Shinyanga, kabla ya kunaswa katikati ya mwezi uliopita.

Mwendesha Mashitaka Esther Ngure, alidai mahakamani hapo kuwa, waliifanyia kazi taarifa ya kuwapo kwa watoto hao wanaovushwa na kutumikishwa nchini humo na kwamba mtego ulizaa matunda kwa kuwanasa Dutu na mkewe.

Alidai pia kuwa, utafiti ulionesha kwa siku walikuwa na uwezo wa kukusanya hadi Sh 13,000 za Kenya, sawa na Sh 234,000 za Tanzania.

Hii ina maana kwamba, kwa mwezi walimwingizia 'tajiri wao’ zaidi ya Sh milioni 6 kwa kazi ya kuomba, huku ujira wao ukiwa ni kula na kulala.

Akijitetea, Dutu alikiri kuwatumia watoto hao kuomba, lakini akasisitiza kuwa alilenga kukusanya fedha kwa ajili ya kujiongezea kipato.

“Niliwaleta watoto hawa kutoka Tanzania ambako ninauza khanga,” alisema kwa unyenyekevu mkubwa mahakamani hapo.

Lakini alipobanwa zaidi, alisema hakuwa na nia mbaya ya kuwadhalilisha watoto hao walemavu, bali alilenga kuwasaidia kwa kuwajengea nyumba Shinyanga, chanzo cha fedha kikiwa ni hicho walichokuwa wakiomba kutoka kwa wasamaria wema.

“Pia nazitumia kwa chakula na matunzo yao ya kila siku,” alisisitiza Dutu ambaye mkewe, Josephine, aliomba huruma ya mahakama, akidai kwamba wakati wanaoana hawakuwa na mtoto hata mmoja mlemavu aliyetumiwa kuomba mitaani.

Taarifa ambazo zilipatikana baadaye, zinasema mahakama iliamuru walemavu hao warudishwe haraka Tanzania.

Juhudi za gazeti hili kupata habari za kina kutoka ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Kenya, hazikuzaa matunda, kwani mara zote maofisa wa ubalozi walipotafutwa, hata kwa simu za ofisini, hawakupatikana.

Aidha, juhudi hizo ziliendelea katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Dar es Salaam, ambako maofisa wa kitengo uhusiano, walijitahidi kutoa ushirikiano kwa karibu wiki mbili, lakini wakikwama kutoa majibu halisi kutoka Kenya, kwa walichodai bado wanaendelea kuwasiliana na maofisa hao nchini humo.
Chanzo: HabariLeo
 
Back
Top Bottom