Watakuja Mtwara kuomba 'KULA'

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,009
Wabunge Mtwara wakacha kikao cha maendeleo

na Hassan Issa, Mtwara
Tanzania Daima~Sauti ya Watu​

WADAU wa maendeleo mkoani hapa juzi waligeuka mbogo dhidi ya wabunge wao, baada ya kupewa taarifa kuwa hakuna hata mbunge mmoja kati ya tisa wa mkoa huo uliyehudhuria katika kikao cha kujadili maendeleo ya mkoa huo.

Wadau hao ambao ni pamoja na viongozi wa asasi za kiraia, wakulima, wanafunzi na wafanyabiashara wa mkoani hapa, walikuwa katika mdahalo wa maendeleo ya mkoa, kikao kilichoitishwa na mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali Mkoa wa Mtwara (MRENGO), na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa shule ya Sekondari ufundi Mtwara.

Zogo lilianza baada ya Katibu wa Mrengo, Allan Mkopoka, kuwaambia wajumbe kuwa licha ya wabunge kupewa taarifa na kujulishwa kuwa wanawajibika kutoa mada maalumu katika mdahalo, lakini hakuna hata mbunge mmoja kati yao aliyefika katika kikao hicho. Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Anatoli Tarimo.

"Wadau kama mnavyoona katika ratiba yetu kuna mada ambazo zilitakiwa kutolewa na wabunge wetu, lakini hadi sasa hakuna hata mmoja wao aliyefika na hakuna uwezekano wa kutokea…lakini hiyo isitufanye tushindwe kuendelea na mdahalo wetu naomba tuendelee," alisema Mkopoka.

Baada ya kauli hiyo ya katibu, ndipo wajumbe wa mdahalo huo waliotoka katika wilaya zote za mkoa wa Mtwara, walipoanza kushutumu juu ya tabia ya wawakilishi hao wa wananchi kushindwa kuhudhuria katika vikao vinavyojadili masuala ya maendeleo ya mkoa wao.

"Hawa waheshimiwa wanatukatisha tamaa na hali hii inatufanya tukose kuwa na imani na yale wanayoyasema bungeni…maaana hapa ndipo ambapo tungewatuma nini wakaseme na hawajatokea sasa, hayo wanayoyasema wametumwa na nani?" alihoji mjumbe mmoja aliyejulikana kwa jina la Kwiyunga.

"Hawa jamaa hawana la kutueleza ndiyo maana wamekacha kikao…wao ni Dar e Salaam tu, kuja huku ni mara moja moja tu sasa haya maendeleo ya mkoa yanawahusu nini…wameona posho ndogo ndiyo maana hawakuja, lakini kama wangehakikishiwa posho nzuri wangejaa hapa…hukumu yao ni mwaka 2010," walisikika wadau hao wakilalama ukumbini hapo.


Hoja ya wabunge kutofika ilichukua muda mwingi wa majadiliano, huku kila aliyepata nafasi ya kuchangia akiwashutumu wabunge hao na kufanya mkutano uchelewe kuanza.

Mkuu wa mkoa alilazimika kuwaeleza wananchi hao kuwa kwa wale ambao hawajafika atawafikishia ujumbe huo, ili siku nyingine wahudhurie iwapo wataalikwa.

Akizungumza na Tanzania Daima, katibu wa Mrengo, ambaye pia ndiye mratibu wa mdahalo huo, Mkopoka, alisema kati ya wabunge hao alikuwa na taarifa ya Geoge Mkuchika tu aliyetoa taarifa kuwa hataweza kuhudhuria kikao hicho kwa kuwa alikuwa na kazi maalumu ya chama chake huko mkoani Mbeya.

"Mkuchika aliniarifu, na Mbunge wa Viti Maalumu, Anastazia Wambura, ni mgonjwa na yuko Dar es Salaam kwa matibabu, lakini wengine sina taarifa nao juu ya kushindwa kwao kuja hapa leo (juzi)," alisema Mkopoka.

Wabunge wote walipelekewa barua rasmi za kualikwa katika kikao hicho na baadhi yao pamoja na barua pia aliwapigia simu, lakini hata hivyo hawakuonyesha ushirikiano mzuri wa kueleza wazi kama watafika au la.

Mkoa wa Mtwara una wabunge tisa - wote kutoka CCM. Nao ni Raynald Mrope (Masasi), Selemani Kumchaya (Lulindi), Juma Njwayo, (Tandahimba), Mohamed Sinani (Mtwara Mjini), Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini), Geoge Mkuchika (Newala), Mariam Kassembe (Viti Maalumu), Anastazia Wambura (Viti maalumu) na Dansatan Mkapa (Nanyumbu).
 
Back
Top Bottom