Kakke
JF-Expert Member
- Dec 4, 2010
- 1,883
- 1,482
Monday, March 21, 2016
BY GWAMAKA ALIPIPI
Wasomi na wachambuzi wa siasa, wameelezea hatua ya Chama cha Wananchi (CUF) kususia uchaguzi mkuu visiwani Zanzibar, uliofanyika jana na idadi ndogo ya wananchi kujitokeza kupiga kura ukilinganisha na ule wa Oktoba 25, mwaka jana, kuwa ni anguko la demokrasia visiwani humo.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha.
Januari 28, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, CUF kupitia Baraza Kuu, ilitoa msimamo wake kuwa haitashiriki uchaguzi mkuu wa marudio, ikiwa ni siku chache baada ya tangazo la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, kutangaza kuwa uchaguzi utarudiwa Machi 20, mwaka huu (jana).
Hata hivyo, wakati uchaguzi huo ukirudiwa jana, vyombo vya habari vilivyokuwapo Zanzibar, vilieleza kuwa kuanzia asubuhi hadi mchana, kulikuwapo na idadi ndogo ya wananchi waliojitokeza katika vituo vya kupigia kura, kulinganisha na uchaguzi uliofutwa wa Oktoba 25, mwaka jana.
Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia, Idara ya Uandishi wa Habari na Teknolojia ya Habari nchini Namibia, Julius Mtemahanji, alisema hatua ya CUF na wananchi kutojitokeza kupiga kura ni anguko la demokrasia.
Alisema kulingana na katiba iliyopo, ni vigumu kufanya chochote kwa kuwa Zanzibar ni nchi kamili, lakini serikali ya Rais Dk. John Magufuli, inaweza kutumia busara ya kuleta maelewano na maridhiano kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Hilo ni anguko la demokrasia ambayo ni mfumo wa uwakilishi. Anayeshinda atatawala vipi waliosusia uchaguzi? Tanzania inatakiwa ijihoji. Hii ni aibu kwa nchi yetu,” alisema Mtemahanji.
Mwanazuoni kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Ernest Mallya, alisema kinachotokea sasa Zanzibar kiliwahi kuzungumzwa na baadhi ya viongozi wa CCM.
Alisema kuna mmoja wa wawakilishi wa Zanzibar aliwahi kuzungumza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), haiwezi kuondolewa madarakani kwa kutumia karatasi za kura.
Alisema kuna vitu vinavyoendelea katika Uchaguzi wa Zanzibar ambavyo ni aibu kwa taifa.
Alisema hatua ya CUF kujitoa katika uchaguzi huo na wananchi kususia kwa kutojitokeza kupiga kura, inaashiria wameshaona kuwa haki yao ya kikatiba haitapatikana hata wakishiriki kupiga kura.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vyuo Vikuu barani Afrika, Prof. Tolly Mbwette, alisema demokrasia haiwezi kulazimishwa, bali ni uhuru wa mtu.
Prof. Mbwette alisema kitendo cha wananchi kutojitokeza kwa wingi kupiga kura ni uamuzi wao binafsi, na kwamba vyama vikuu vya siasa visiwani Zanzibar vinapaswa kukaa kwa pamoja na kufanya mazungumzo ya amani.
Alisema kitendo cha CUF kususia uchaguzi si kizuri na kinaleta picha mbaya kwa mataifa ya nje. Alifafanua kuwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar ni tofauti na wa bara kwa kuwa unakuwa na hisia kali na kwamba kuendelea kuwapo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, itakuwa njia pekee ya kuleta amani visiwani humo.
Uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar ulifanyika jana baada ya ule wa awali wa Oktoba 25, mwaka jana, kufutwa na Mwenyekiti wa Zec, Jecha kwa kile alichokieleza kuwa uchaguzi huo ulikuwa na kasoro nyingi.
Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema Zanzibar hakuna uchaguzi wowote unaoendelea.
Alisema kinanachofanyika kwa sasa ni CCM kutafuta uhalali wa mchakato wa kutaka Rais Dk. Ali Mohamed Shein kuendelea kuongoza Zanzibar.
“Wanataka Dk. Shein aendelee, lakini wanashindwa watumie mbinu gani, na ndiyo maana wanalazimisha uchaguzi ufanyike,” alisema Kafulila.
Aliongeza kuwa uchaguzi wa Zanzibar unafanyika bila ya kuwapo na waangalizi kutoka Ulaya, na kwamba waangalizi waliopo Zanzibar wanatoka ndani ya Bara la Afrika ambao wengi wao ni marafiki wa CCM.
SOURCE: NIPASHE