Wasanii wetu, hii ni njaa ama nini?

Wasanii wetu, hii ni njaa ama nini?

sulphadoxine

JF-Expert Member
Joined
Nov 1, 2010
Posts
2,257
Reaction score
649
KAMA kuna ujinga wanaoweza kuufanya wasanii wetu hapa nchini, basi ni kuwapoteza mashabiki wao kwa kujaribu kuwagawa kwa misingi ya itikadi za kisiasa n.k.


Pamoja na ukweli kwamba siasa siyo uadui, lakini kwa jinsi mvutano wa kisiasa ulivyo mkali hapa kwetu na namna mfumo wa vyama vingi ulivyopokelewa na baadhi ya Watanzania kutokana na propaganda za chama tawala, hilo linaweza kuwa ni moja ya mambo yanayoweza kuwagawa wananchi ingawa siyo kwa kiwango cha uadui mkubwa!

Nasema hivyo kwa sababu kila Mtanzania ana uhuru wa kuchagua analolipenda katika masuala mbalimbali bila kuvunja sheria na katiba ya nchi, lakini pamoja na uhuru huo, bado hilo halimpi mtu nafasi ya kumkwaza mwenzake kwa namna yoyote ile iwe ni kwa itikadi za kisiasa, kidini, n.k.

Ndiyo maana hapa nchini petu kuna washabiki wa fani na itikadi mbalimbali kama vile, siasa; ambapo tuna mfumo wa vyama vingi ambavyo ni pamoja na Chama Cha Mapinduzi, CCM, Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema, Chama cha Wananchi, CUF, n.k, vilevile kwenye fani ya mpira hasa wa miguu, wapo Mashabiki wa timu za Simba, Yanga, Azam, Mbeya City n.k.

Siyo hao tu, hata katika tasnia ya Muziki wa dansi, Bongo fleva, Filamu na Maigizo wapo pia mashabiki kibao ambao wanaunganishwa kwa pamoja bila kujali itikadi zao nyingine walizonazo katika masuala mengine, maadam anayewaburudisha na kukonga nyoyo zao, hawagawi mashabiki wake kwa misingi ya udini, ukabila, siasa wala jinsia!

Nimeianza hivyo makala hii ya leo baada ya kusikia kwenye baadhi ya vyombo vya habari, kwamba kuna baadhi ya wasanii wa muziki na filamu wasiopungua 11, eti wametangaza kujiunga na Chama Cha Mapinduzi, CCM walipokuwa wamealikwa kutumbuiza kwenye sherehe za miaka 37 ya kuzaliwa kwa chama hicho.

Kwenye sherehe hizo zilizofanyika kitaifa jijini Mbeya, wasanii hao walitangaza hadharani msimamo huo mbele ya mashabiki wao waliokuwepo pale uwanjani sambamba na wengine wengi waliokuwa wakiwasikiliza na kuwatazama kwa njia ya redio na televisheni.

Bila kujali kwamba kwa kitendo hicho wangelikuwa wakiwakwaza mashabiki wao mbalimbali kote nchini, ambao wana itikadi zao tofauti za kisiasa na kwamba wanawapenda tu wasanii hao kwa sababu tu ya maigizo na nyimbo zao na siyo kutokana na ushabiki wao wa kisiasa!

Kwa mujibu wa matangazo hayo yaliyokuwa yakirushwa moja kwa moja toka jijini humo, wasanii hao walikabidhiwa kadi zao za uanachama na mgeni rasmi katika sherehe hizo, Mwenyekiti wa CCM taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.

Siyo kwamba napinga wasanii hao kuhudhuria sherehe hizo za miaka 37 toka kuzaliwa CCM, la, bali kinachogomba hapa ni kutangaza kwao hadharani kuwa wao ni wafuasi, wapenzi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi, wakati wakijua fika kuwa kufanya hivyo kutawakwaza baadhi ya mashabiki wao!

Haikatazwi msanii yoyote yule kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa ama hata ikiwezekana kuwa mgombea wa nafasi yoyote ile ya uongozi ndani ya chama chochote cha siasa, bali vibaya ni kutangaza msimamo huo wazi na hadharani pasipo ulazima wowote ule!

Mfano; wasanii kama Mrisho Mpoto, Jacline Wolper, Wastara Sajuki na Jacob Steve (JB), wengine ni Single Mtambalike (Rich), Irene Uwoya, Baba Haji, Blandina Chagula (Johari), Omari Mrisho, Juma Kichoka na Banana Zoro, ambao walihudhuria sherehe hizo, hawakuwa na sababu ya kujitangaza hadharani kwa sababu ya kulinda maslahi ya wapenzi wao wasio na itikadi hiyo.

Wangeweza kufanya hivyo kama tu wangelikuwa wanataka kutangaza nia ya kuwania nafasi za uongozi kama udiwani, ubunge na hata uraisi kama ikiwezekana (hilo linaweza kutazamwa kama ni maslahi binafsi ya msanii), kuliko kufanya hivyo hadharani kwa minajili ya kukipigia chama kampeni na kuwa mmoja wa wanachama wake!

Lakini wakati mwingine pia ni vizuri msanii akaamua kuchagua kimoja chenye maslahi kwake kati ya muziki, filamu ama siasa; mfano mzuri ni kama Joseph Mbilinyi aliyeamua kuweka kando muziki na kuwa mwanasiasa, siye yeye tu hata Mudhihil Mudhihil na wengine wengi.

Ama kama huwezi kabisa kufanya hivyo na kwa kuchelea kuwakwaza wapenzi na mashabiki wako, basi ni vyema ukajikita upande mmoja tu katika fani uliyonayo ili jamii ikuelewe hivyo toka mwanzo na kukuheshimu, kama afanyavyo Captain John Komba ambaye wananchi siku zote wanamtambua kama msanii wa CCM.

Na kama huwezi vyote basi ni vizuri ikitokea umealikwa wewe kama msanii kwenye tamasha ama mkutano wa chama chochote cha kisiasa, itakuwa vyema na haki kama utaimba nyimbo zako za kila siku zisizo na maudhui ya kisiasa, maadam unalipwa pesa kama msanii mwalikwa!

Hii tabia ya kubadilika badilika kama kinyoga kwa sababu ya kuendekeza njaa na maslahi kiduchu yasiyokidhi haja, inamshushia msanii hadhi na heshima mbele ya wapenzi na mashabiki wake; kwani ni lazima utangaze hadharani wewe ni Chadema au CCM eti maadam tu wamekualika? Kwanini usibaki kama msanii tu?

Hili linadhihirisha ni jinsi gani mlivyo na dhiki na kwamba inaonekana hata fani ya filamu na muziki mmo mmo tu kiujanja janja mkiganga njaa zenu, huku mkitafuta pengine pa kushika, alimradi mmepata chochote: Ndiyo… naweza kusema hivyo kwa sababu mmekuwa mkichukuliwa na kila upepo unaovuma.

Zipo taarifa kwamba baadhi yenu wamekuwa wakivizia vipindi vya kampeni za uchaguzi mkuu, ambapo wamekuwa wakijiunga na bendi na vikundi vya sanaa vinavyomilikiwa na CCM kwa ajili ya vijisenti vinavyosemekana kumwagwa na chama hicho nyakati za kampeni na baada ya hapo wanatimka tena!

Wengine wamekuwa wakizibadili nyimbo zao maarufu zilizopendwa sana na kuwapa umaarufu na kuzifanya kuwa za kisiasa kwa toni na mahadhi yaleyale, alimradi kuwapendeza wanasiasa kwa maslahi duni na dhalili, bila kujali kama wanawakwaza au kuwapoteza wengi wa mashabiki wao!

Hata kama ni ku-declare interest, jambo hilo pia lina faida na hasara zake; mfano mchezaji mmoja wa kilabu ya mpira wa miguu huko ulaya, aliwakwaza baadhi ya washabiki wa timu yake kwa kuonesha ishara ya alama ya Nazi (utawala dhalimu wa kijerumani enzi hizo), jambo lililoplekea siyo yeye tu kufungiwa na timu yake, bali hata mashabiki kususia mechi za kilabu hiyo!

Wapo pia baadhi ya wanamuziki na wacheza filamu ambao kazi zao za sanaa zimesusiwa kwa kitendo chao cha kutangaza hadharani misimamo yao ya kuunga mkono na kushiriki vitendo vya ushoga, jambo lililopelekea baadhi yao kushuka kimapato kwa kiasi kikubwa mno!


Nitake tu kuwaasa wasanii wetu kuwa; kama wana ndoto za kupata maslahi kupitia siasa basi waachane na usanii na kujiendeleza kielimu, kwani Tanzania ijayo kiongozi hatopata nafasi kwa usanii wake kama ilivyo sasa, bali ni kupitia elimu yake tu.

Hakutakuwa na nafasi za upendeleo za kujaza wasanii bungeni, na kwenye nafasi za wakuu wa wilaya na mikoa kupitia sanaa ya kusifu chama na viongozi wake, bali ni kwa misingi na vigezo vya elimu tu kuanzia mwenyekiti wa mtaa hadi Rais wa nchi. Tuambieni leo tuwatambue, ninyi ni makada wa vyama vya siasa ama wasanii?
 
Back
Top Bottom