Wanyama na ndege wa Afrika. 1-Tembo

Wanyama na ndege wa Afrika. 1-Tembo

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Joined
Jan 31, 2021
Posts
10,884
Reaction score
18,824
Screenshot_20250414-155852.png


Tujifunze habari za Wanyama na ndege kutoka kitabu Wanyama na Ndege wa Afrika.



TEMBO

1.jpg

TEMBO au ndovu ndiye aliye mkubwa kuliko wanyama wote wa dunia hii. Anakaa katika makontinenti mawili-yupo Bara Hindi na huku kwetu Afrika. Iko tofauti kati ya tembo hawa wawili. Huyu wa Afrika yu mkubwa kuliko mwenzake, tena masikio yake ni mapana sana na pembe zake ni ndefu zaidi.

Zamani za kale tembo walikuwa wanakaa katika pande nyingi za Afrika wakitembea makundi makubwa; lakini tangu mwanzo binadamu ametamani pembe zake kubwa apate kujifanyizia vitu vizuri na vyenye faida. Kwa hiyo tembo ambao walionekana zamani tokea Cape of Good Hope mpaka mto wa Nile wamefukuzwa kabisa kutoka South Africa- liko kundi dogo tu katika Cape Province.

Siku si nyingi tembo wengi waliuawa katika mipaka yote ya Afrika lakini siku hizi wamelindwa na serikali, karibu kila mahali, wasiuawe. Maana wakubwa wa serikali wamekwisha kufahamu wasipowazuia watu labda tembo wote wataangamizwa. Katika Afrika ya Katikati hatuna miji mikubwa basi hata leo tunayo makundi makubwa ya tembo.

Wengine husimulia hadithi za ajabu juu ya ukubwa wa tembo dume. Katika wale waliopimwa vizuri aliyekuwa mkubwa amepata urefu wa futi kumi na mbili kasoro inchi tatu. Siku hizi ni shida kumwona mmoja mwenye urefu huu. Masikio ni mapana sana ; watu husema kwamba kipimo toka nje ya sikio la kwanza mpaka nje ya sikio la pili ni sawasawa na kimo cha tembo toka chini mpaka mabega yake. Tena kipimo cha kuzungukia mguu wake mara sita ni kipimo kile kile cha kimo chake.

Pembe zake hasa ni meno, zimeota katika taya la juu. Ndani ya pembe kuna sehemu mfano wa mvungu mtupu, tena iko sehemu nyororo kidogo sawasawa na sehemu ya ndani ya meno yetu. Pembe za tembo zina uzani mbalimbali. Nyingine zilizopatikana zamani zilikuwa na urefu kama futi nane na uzito wa ratili mia nyingi lakini zile za siku hizi ni ndogo. Leo pembe kubwa inapata uzito wa ratili sabini. Tembo jike ni mfupi kuliko dume tena si mnene kama dume, na pembe zake si kubwa, kwa kawaida ni nyembamba zenye uzito wa ratili chache tu.

Tembo haoni vizuri, hawezi kutambua kitu kilicho mbali kidogo lakini ana masikio mepesi mno, hata sauti ndogo au kishindo kidogo atasikia ingawa inatoka mbali kabisa. Tena ni fundi wa kusikia harufu. Ikiwa analetewa harufu kidogo tu ya binadamu anajua kwamba wawindaji wanakuja kumtafuta.

Mkonga wake ni pua yake, tena unamfalia kuokotea vitu vidogo kama matunda ya msituni, au kuvutia matawi ya miti apate kutumia majani yake. Pembe zake pia anazitumia apate kuvunja matawi au kuchimbua mizizi na kujilinda. Tembo wote wanapenda maji, hutumia mikonga yao kwa kujimiminia manyunyu ya maji baridi wakati wa jua kali. Katika nchi nyingine za Afrika maji ni shida. Kwa hiyo pengine kundi la tembo wakisafiri siku nyingi katika nyika wanaweza kuona shida ya maji. Lakini hawa tembo wanayo namna ya ajabu ya kuweka akiba ya maji ndani ya miili yao. Mtoto wa tembo akichoka na kuona kiu katika safari kubwa mama yake anaingiza mkonga wake kinywani mwake na kuteka maji mengi pale ndani ya koo yake apate kumpa mtoto atulize kiu yake.

Tembo hawaui wanyama kwa ajili ya chakula, wanakula majani ya miti, mizizi na vitu vya namna hii. Tembo mtoto hunyonya maziwa ya mama mpaka anapopata umri wa miezi sita; hapo anang'oka na meno yake ya kitoto na kuanza kutumia chakula cha matunda na majani sawasawa na wazee wake.

Safari ndefu hazina taabu kwa tembo kwa sababu wanaweza kwenda maili nyingi kabisa pasipo kuchoka ikiwa wanasafiri wakati wa baridi ya usiku. Mchana kwenye hali ya jua kali wanapenda kupumzika kivulini na kuoga kwenye matope na kujitupiatupia maji. Wanapojifurahisha hivyo wanapiga mlio mkubwa unaofanana na sauti ya tarumbeta ambao husikilikana mbali sana.

Tembo wanazo akili nyingi sana hata wanaweza kukumbuka mambo yaliyopita zamani. Wanaposakwa na watu kwa ajili ya pembe zao wanapata kuhangaika sana wakihamahama na kuwa macho kwa hatari. Nyakati hizi ni tembo mama hasa anayehadhari kwa adui kuliko dume, zaidi akiwa na mtoto mdogo. Wanajifanya kuwa wakali mno hata mara kwa mara wanamshambulia na kumrukia mtu ye yote ambaye wanamwona anataka kuwaumiza watoto wao. Kwa kawaida ni wanyama wasio na matata. Pengine dume mzee hufanya ukali na ukatili juu ya wenzake. Neno hili kwa kawaida linatokea iwapo ameumizwa na wawindaji naye hawezi kuacha kuogopa adui. Basi anajifanyizia kuwa mkali kwa wote na kujitenga na kundi.

Kwa kuwa ni wanyama wakubwa tembo wanahitaji chakula kingi na mara nyingi wanaharibu misitu na mashamba pia. Kuliko yote wanapenda mahindi na nafaka nyingine. Pengine kundi la tembo wakiona shamba la mihindi karibu ya mji watakuja usiku na kuharibu shamba zima kwa usiku ule ule wakikanyaga mashina ya mimea na kuvunja- vunja mingine kama kwa mchezo tu na pia wanatafuna chakula kingi kabisa. Inaonekana kwamba tembo ni fundi wa kujua nyakati za kupanda na kuvuna, maana kila mwaka mahindi yakianza kuzaa, tembo wanatokea na kuzunguka mtaa mzima wakiharibu mashamba moja moja. Kwa hivi mara kwa mara ni lazima kuwaua tembo wengine kusudi wenzao wa kundi wafukuzwe warudi kwao msituni.

Watu wa Afrika husema kwamba wanyama wote wa mwitu wanamwita tembo 'Mzee' naye hana adui ila binadamu tu.

Anapopata kushtushwa ananyosha masikio yake mpaka yamefanana na vipepeo vikubwa juu ya mashavu yake na huko nyuma amesimama kimya na kusikiliza tu. Ingawa yu mkubwa kabisa ni ajabu jinsi anavyoweza kujificha penye vichaka au katikati ya miti, hata wawindaji wanaweza kuja karibu yake, kwa umbali wa yadi chache tu, wasimwone. Hii ni kwa sababu rangi ya ngozi yake inalingana na mahali anapokaa, zaidi ya haya anajua kusimama kimya kwa muda mrefu asipige kelele. Atembeapo hafanyi vishindo hata pengine kundi zima la tembo limepita ndani ya kambi la watu wanaolala usingizi asiamshwe hata mtu mmoja.
 
Back
Top Bottom