Wanaume wapo hatarini kupata ugumba

Wanaume wapo hatarini kupata ugumba

Miss Zomboko

JF-Expert Member
Joined
May 18, 2014
Posts
4,618
Reaction score
9,611
Madaktari bingwa wa upasuaji wa maradhi njia ya mkojo wanasema ajali, saratani ya kibofu na maradhi ya njia ya mkojo ni sababu za kasi ya kukua kwa tatizo la fistula kwa wanaume nchini.

Wakati sababu hizo zikitajwa, Mtaalamu wa masuala ya uzazi na tatizo la fistula nchini Kenya, Dk Weston Khisa anasema tatizo la fistula kwa wanaume lipo lakini halifahamiki sana kwasababu halitokei mara kwa mara kama ilivyo kwa wanawake.

Kwa Tanzania, wastani wa wanawake 3,000 kila mwaka wanapata tatizo la fistula wakati wa kujifungua, huku 1,400 pekee ndiyo hujitokeza kutibiwa.

Hata hivyo, Dk Khisa anasema kwakuwa mtu akipatwa na fistula ni lazima litokee tundu eneo la njia ya kutolea haja kwa wanawake, lakini kwa mwanaume tatizo hilo husababishwa na saratani ya tezi dume na maradhia mengine ya zinaa yanayoweza kusababisha tundu katika maeneo hayo ya mwili.

“Fistula kwa mwanaume dalili zake ni sawa na zile za fistula kwa upande wa wanawake na tatizo hilo lisipodhibitiwa mapema, linaweza kumsababishia muathirika ugumba.

Ila likitibiwa mapema anaweza kurudi katika hali yake ya kawaida,” anasema Dk Khisa.

Daktari Kiongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Stanley Binagi anasema fistula kitaalamu ni pale njia mbili zinapounganishwa na tundu katikati.

Anasema mara nyingi kwa wanawake tundu hilo hutokea pale mjamzito anapoumwa uchungu na kutaka kujifungua, mtoto anaweza kukandamiza sehemu zote mbili za kutolea haja kubwa na ndogo na kusababisha tundu linaloziunganisha.



Kwa wanaume inakuwaje?

Daktari huyo anasema wanaume hawawezi kupata

fistula kama wanayopata wanawake, kwa kuwa mifumo yao ya uzazi iko tofauti, bali huipata kwa kuugua maradhi ya saratani. Anasema saratani ikiwamo ya kibofu ni miongoni mwa zinazowasababishia wanaume fistula kwa sababu wakati mwingine hutoboa hadi njia ya haja kubwa.

“Tatizo la mwanaume kutokwa mkojo bila kujizuia linatokea zaidi kwa walio na saratani ya kibofu,” anasema Dk Binagi.

Anasema mara nyingi saratani hiyo husababisha kuzalishwa tundu ambalo hutokea njia ya haja kubwa na wakati mwingine mkojo unaweza kuziba mbele hautoki na ukatafuta kupenya kati ya njia ya mkojo na ngozi chini ya hashuo, sasa hiyo ni fistula.



Dk Binagi anasema wanaume hupata aina kadhaa za fistula ambazo wakati mwingine hutokana na maradhi ya zinaa yanayosababisha njia ya mkojo kuota majipu.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanasema zipo aina nyingine za fistula anazoweza kuzipata mwanaume kuwa ni pamoja na ya koo na mfumo wa hewa ambayo ni njia ya kumeza na kukohoa, utumbo, kuumia au kupata ajali.

Wanasema tundu lolote likitokea kati ya mifumo hiyo, huitwa fistula.

“Ni rahisi sana mwanaume kupata fistula ila hawezi kupata kwa njia ya uzazi kwa sababu saratani ya kizazi ni ya wanawake na yenyewe inaweza ikachimba na kutokezea kwenye njia ya haja kubwa au mkojo, lakini ambayo huwapata wote ni ile ya haja kubwa,” anasema Dk Binagi.

Lakini pia anasema mwanaume anaweza kupata fistula ya kutengenezwa na madaktari kwaajili ya watu wanaopatwa na matatizo ya mkojo yaani hawawezi kukojoa vizuri, hivyo huhamisha njia yake ya mkojo ili uwe unapita sehemu ya haja kubwa kama sehemu ya matibabu ya kawaida na sio ugonjwa.

“Wakati mwingine tunatengeneza Fistula kwa watoto wachanga ambao wanazaliwa na ulemavu wa matundu yake kuungana. Kwakuwa fistula inahusisha tatizo la tundu kati ya njia moja na nyingine, matukio ya aina hiyo ni mengi lakini ya uzazi inatokea kwa mwanamke pekee,” anasema Binagi.

Daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya njia ya mkojo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Obadia Nyongole amewahi kunukuliwea na gazeti hili anasema awali kulikuwa na wagonjwa wachache wa fistula kwa wanaume, lakini sasa wanaongezeka.

“Kama linaweza likatokea tundu kwenye kiungo kingine na likashindwa kupona vizuri au wakati wa kufanya upasuaji kuna kiungo kiliguswa na kifaa kingine bila kugundulika wakati wa upasuaji kikaachwa hivyo hivyo, kinaweza kutengeneza fistula hasa sehemu ya utumbo,” anasema Dk Nyongole.

Anasema wanaume wengi wanaopata fistula ni wale waliofanyiwa upasuaji katika njia ya mkojo wakawekewa mpira baada ya kutolewa, kuna kovu ambalo hutakiwa lipone lakini likashindikana. Hivyo husababisha mkojo kuanza kutokea tumboni chini ya kitovu, hiyo ni fistula kwa sababu tundu limeshindwa kuziba.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Hospitali ya CCBRT, Brenda Msangi anasema fistula ya uzazi haiwapati wanaume bali huwapata wanawake waliomaliza kujifungua kwa uchungu pingamizi wa muda mrefu bila kupata huduma ya haraka ya kumtoa mtoto.

“Hili tatizo siyo la wanaume ni la wakina mama ambao na wao linawapata baada ya kujifungua. Mwanaume anaweza kupata fistula lakini sio ‘Obstetric fistula’ (ya uzazi).

Takwimu zinasemaje juu ya fistula
Mwezi mmoja uliopita, Serikali ilitangaza mpango wake wa kutaka kufanya utafiti wa hali ya tatizo la fistula nchini kwa lengo la kupata takwimu sahihi zitakazosaidia kupambana na kadhia hiyo.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema takwimu zinazotumika sasa zilitokana na utafiti uliofanyika miaka 18 iliyopita.

“Takwimu tunazotumia ni za miaka 18 iliyopita, tunatarajia kufanya utafiti ili kupata takwimu mpya mwaka huu, hizi tunazozitumia zimepitwa na wakati, tunahitaji za sasa ili tujue tatizo ni kubwa kiasi gani ili tulimalize kabisa kwani halipaswi kuwa jambo la kujadiliwa kitaifa,” anasema Dk Ndugulile.

Ili kukabiliana na tatizo la fistula, Serikali, mashirika ya Afya na wanaharakati mbalimbali, jicho lao linatazama zaidi upande wa wanawake pekee bila kukumbuka kuwa lipo hata kwa wanaume, isipokuwa tofauti ni urahisi na sababu za tatizo.

Dk Ndugulile anasema ili kulimaliza tatizo, lazima zichukuliwe hatua za makusudi ambazo hazikuwahi kuchukuliwa awali. “Hatuwezi kuendelea kufanya mambo yaleyale na ukatarajia mabadiliko makubwa.”

Fistula kwa wanawake.
Wanawake huathiriwa zaidi na fistula ya uzazi, kwa mujibu wa takwimu za Serikali .

Muwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu duniani (UNFPA), Jacqueline Mahon anasema zaidi ya wanawake milioni mbili hupata tatizo la fistula na wengi wao wanaishi Kusini mwa Jangwa la Sahara, Asia na Uarabuni.

Kitaalamu fistula ni tundu linavujisha vitu katika njia ya uzazi inaweza ikawa ni mkojo (Vesco Vaginal Fistula), haja kubwa (Rectal Vaginl Fistula) au vyote kwa pamoja.

Ripoti mbalimbali zinaeleza zaidi ya asilimia 90 ya wanawake wanaopata tatizo hilo husababishwa na uchungu pingamizi.

Uchungu pingamizi unaweza kutokana na ukubwa wa mtoto usiolingana na nyonga ya mzazi. Mtoto hukwama lakini tumbo la uzazi huendelea kusukuma mpaka mtoto atoke suala ambalo husababisha majeraha kwakuwa mtoto hukandamiza kibofu na njia ya haja kubwa.

Kinga na Matibabu ya fistula ya uzazi.
Fistula hutibiwa kwa njia ya upasuaji na kuziba sehemu ya tundu lililojitokeza. Baada ya upasuaji, mgonjwa anatakiwa kukaa siku 14 akiwa anatumia mpira wa kutolea haja na baada ya hapo, atakuwa amepona vizuri.

Namna ya kuiepuka fistula
Mtu anaweza kujikinga na tatizo hilo hasa wajawazito mara asikiapo dalili za uchungu, awahi kwenye kituo cha kutolea huduma za afya na wazazi kuwapatia lishe nzuri watoto itakayowasaidia kukua vizuri ili wasikumbane na tatizo la kutotanuka kwa nyonga zao.


MWANANCHI
 
Vitisho tu ivyo ....sasa hivi wanaume tunaochoogopa ni Ukimwi wa kurogwa.
 
Back
Top Bottom