Wanasiasa Wanatuharibia Ibada Zetu

Njilembera

JF-Expert Member
May 10, 2008
1,496
609
Nyumba zetu za ibada, haijalishi misikitini, makanisani au mahekalu ya kihindi au kichina, zimekuwa kwa miaka mingi sehemu yetu ya kutafakari maisha yetu na hasa uhusiano wetu na muumba wetu. Ni nyumba za upendo, utulivu na unyofu wa mioyo yetu. Ni hekalu la roho zetu. Ni kimbilio letu pale tunaposhambuliwa miili yetu kupata kinga. Ni mahali pa usalama na amani. Ni sehemu iliyotukuka na ya kuheshimika baina yetu. Hata asiye muumini wa dhehebu fulani anapopita mbele ya nyumba yeyote ya ibada, anaijali, hafanyi mambo ya ajabu ajabu.

Lakini imedhihirika kabisa sasa viongozi wetu hasusani wa kisiasa wametuvuruga na sasa wanatumia nyumba zetu za ibada kama sehemu ya kujisafisha kwa ugoro waliounywa na uchafu waliopitishiwa. Siku za karibuni tumeona mengi. Sina haja ya kumtaja Makonda - kama alivyoonekana misikitini na makanisani. Sikusudui hata mara moja mada hii imlenge Makonda ndiyo maana nimetoa tahadhari. Lakini wapo wengi tu tena waheshimiwa sana.

Tunapokwenda kwenye nyumba za ibada ni kwa ajili ya kujinyenyekesha mbele ya Muumba wetu. Hatuendi kujionyesha kwa wenzetu kwamba na sisi ni waumini. Hatuendi kuwadhihirishia wapinzani wetu kwamba sisi ni malaika kuliko wao. Lakini, tazama kinachotokea. Imekuwa ni kawaida kiongozi wa siasa akifika kwenye ibada, kupewa nafasi na mwendesha ibada kuzungumza. Azungumze nini? Bila shaka kwa kuwa hajajiandaa kutoa tafakuri ya neno la ibada atazungumzia siasa, na hasa kujikosha kwa aliyoyafanya. Waumini kwa maajabu kabisa nao wamekuwa wakishabikia na kumpigia makofi mgeni kama huyu. Nyumba ya ibada inajeuzwa kuwa ya kejeli za siasa.

Tena wanasiasa hao hawakai kwa adabu ndani ya majumba haya. Wengi wanapenda kukaa mbele waonekane, walinzi wao wakipita huku na kule ilmradi wawagasi waumin wengine. Ibada inageuka kuwaona na kuwasikiliza viumbe hawa. Wengine hata hawafuati desturi, waumini wakisimama, yeye hupiga magoti na kinyume chake, ilmradi aonekane ni spesho. Majumba yetu ya ibada yamekuwa majumba ya maonyesho na majigambo?

Hebu fikiria wakati anazungumza mheshimiwa ndani ya nyumba ibada, akawepo muumini aliyekwazika kwa kauli za mwanasiasa. Akikurupuka, wewe Shehe, Padri, Baba Mchungaji utamlaani akionyesha hasira zake kwa kumtwanga kichwa mwanasiasa. Je hujawa sababu ya kuvunjisha amani ndani ya nyumba ya ibada.

Viongozi wetu wa dini mnatuangusha sana. Acheni nyumba za ibada zibaki kwa shughuli zilizokusudiwa, na kamwe msiwakaribishe wanasiasa. Nanyi waumini - mnafanywa mazezeta hata mnasahau sababu ya kufika mle ndani ya nyumba takatifu na kupiga makofi. Kwa nini msiinamishe vichwa vyenu na kuwaombea hawa viongozi wa dini warudi ndani ya imani?

Je kuna haja kweli ya kuwavumilia viongozi wa dini wanaowakaribisha wanasiasa kunajisi nyumba za ibada?
 
Tatizo lipo kwa viongozi wa dini kupenda kujipendekeza kwa wanasiasa.
 
Back
Top Bottom