Wanaowania urais Z’bar waonywa kuacha kuchafuana

MzeePunch

JF-Expert Member
Jun 8, 2009
1,412
203
Wanachama wa CCM Zanzibar ambao wameanza mbio za kuwania urais mwaka 2020 kwa kuunda makundi wameonywa kuacha malumbano na kuchafuana ili kulinda mshikamano uliopo ndani ya chama hicho.

Onyo hilo limetolewa mjini hapa na mmoja wa wazee wa CCM, Kombo Mzee, ambaye amesema hali ya mshikamano iliyoimarishwa na Rais Dk Ali Mohamed Shein inapaswa kudumishwa kwa kuepuka makundi hasimu.

Mzee amesema baadhi wa watu wenye nia ya kumrithi Dk Shein atakayemaliza kipindi chake cha pili na cha mwisho cha uongozi miaka mitatu ijayo, wameanza kulumbana na kuchafuana kwa lengo la kuharibiana katika kinyang’anyiro hicho.

“Tunawasihi wana CCM wenzetu wanaotaka kuwania urais kuwa na subira na kuheshimu utaratibu tuliojiwekea wa kumpata mgombea wa urais badala ya kuanza kucheza rafu, hasa kipindi hiki ambapo Rais Shein anafanya mambo makubwa kwa ajili ya Zanzibar,” alisema Mzee katika mahojiano.

Alisema ni vema wana CCM wakaendelea kumuunga mkono rais aliyepo madakarani ambaye ameonesha ubunifu mkubwa katika kuiletea Zanzibar maendeleo ya kiuchumi badala ya kuanzisha chokochoko zinazoweza kukwamisha mikakati ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Mzee, watu kadhaa wanaokusudia kuwania urais mwaka 2020 wameanza kujichomoza huku wengine wakiwatumia wapambe wao kuwachafua wale wanaoonekana kuwa wapinzani wao katika kinyang’anyiro hicho.

Alisema baadhi ya watu wanaotajwa kutaka kumrithi Dk Shein wana sifa zinazofaa lakini wanaweza kujikuta wakichafuliwa iwapo malumbano yaliyoanza kujitokeza hayatakemewa hivi sasa.

Mzee, ambaye ni mmoja wa walioshiriki katika harakati za mapinduzi ya Zanzibar, alisema kuibuka kwa makundi ya urais hivi sasa kunaweza kuvuruga utulivu na hatua kubwa za maendeleo, ikiwa ni matunda ya kazi kubwa iliyofanywa na Dk Shein.

“Tuache malumbano ya urais na badala yake tumuunge mkono rais huyu mzalendo wa kweli (Dk Shein) mwenye nia ya dhati ya kuhakikisha anaacha alama baada ya kumaliza muda wake wa urais,” alisema Mzee.

Mara baada ya kuapishwa baada ya uchaguzi wa marudio uliosusiwa na chama kikuu cha upinzani, CUF, Rais Dk Shein, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM upande wa visiwani, aliahidi kuhakikisha kuwa Zanzibar inabaki salama wakati wote.

Hatua mbalimbali alizochukua Dk Shein kuimarisha uchumi wa Zanzibar na kusimamia kwa nguvu zote amani na utulivu zinaonekana kuwanyima wapinzani hoja za kuikosoa serikali yake.
 
Back
Top Bottom