Wanakijiji waigomea serikali wakidai taarifa ya fedha zilizoliwa

Kiranja

JF-Expert Member
May 19, 2007
751
336
WAKAZI wa kijiji cha Machochwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara wamegoma kushiriki shughuli zozote za maendeleo , hadi hapo watakaposomewa mapato na matumizi ya fedha za kijiji chao.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kata hiyo zimeliambia gazeti hili kwa njia ya simu juzi kwamba wananchi hao wanamtuhumu Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Peter Hagare, kuwa hajawahi kuwasomea mapato na matumizi kwa zaidi ya miaka mitano sasa.
Imeelezwa kwamba Hagare ambaye pia ni Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Machochwe hataki kuitisha mikutano ya hadhara.
Kwa mujibu wa habari, mgomo huo ulianza mwanzoni mwa mwezi huu baada ya makubaliano yaliyofikiwa na wananchi kupitia mikutano mbalimbali waliyoifanya kwa kuwashirikisha wenyeviti wa vitongoji.
Habari hizo ambazo pia zimethibitishwa na Diwani wa kata hiyo, Chacha Samwel(Chadema), zinadai kuwa mgomo huo ni miongoni mwa hatua chache ambazo tayari zimeshachukuliwa na wananchi hao ili waweze kusomewa mapato na matumizi.
“ Kilichotukasirisha zaidi ni kitendo cha Ofisa Mtendaji huyu ‘kutafuna’ shilingi 100,000 ambazo alizichukua kwa lengo la ufunguzi wa akaunti ya kijiji cha Machochwe, badala yake hakufanya hivyo; na hivyo inadhihirisha kwamba hana mapenzi mema na maendeleo ya wananchi” anasema Chacha John, kutoka kijiji cha Machochwe.
Anasema Ofisa Mtendaji huyo kila anapoulizwa juu ya suala hilo, hutoa visingizo mbalimbali kwa lengo la kukwepa kukutana na wanakijiji.
Anaendelea kwa kusema; “ Hatua nyingine ambayo tumeichukua ni pamoja na kuifunga ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Machochwe ili mwajiri wake( Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti) pamoja na Mkuu wa Wilaya wafike kwa ajili ya kusikiliza kilio chetu”
Imeelezwa kwamba siku nne baada ya wanakijiji kufunga ofisi hiyo, ilifunguliwa na uongozi wa Wilaya ya Serengeti kwa msaada wa polisi.
“ Matokeo yake ni kwamba Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Edward
Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Dk. Kebwe Stephen

Ole Lenga, aliyekuwa amefuatana na polisi alifika kijijini Februali 6 na kuamuru ofisi hiyo ifunguliwe bila hata kusikiliza malalamiko yetu. Hata hivyo, bado tunaendelea na mgomo wa kutoshiriki shughuli za maendeleo hadi ‘kieleweke” alisema mwanakijiji huyo.
Diwani wa kata hiyo alithibitisha kuhusu kuwepo kwa mgomo huo na kuongeza kuwa Afisa Mtendaji huyo amekuwa kikwazo kikubwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
“ Wakati mwingine huitisha vikao vya WDC (vikao vya Maendeleo ndani ya Kata) pasipo hata kunishirikisha” anasisitiza diwani huyo, Chacha Samwel (Chadema).
Chacha anasema kwamba zaidi ya kugoma kushiriki katika shughuli za maendeleo, wakazi zaidi ya 200 wa kijiji cha Machochwe wanashinikiza Ofisa Mtendaji huyo ahamishwe.
Diwani huyo anasema wanakijiji wanaamini kwamba ofisa huyo hukingiwa kifua na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri pamoja na Mkuu wa Wilaya.
Ofisa Mtendaji huyo amethibitisha kuwapo kwa mgomo huo, lakini amemlaumu Diwani Chacha kuwa ndiye anayewachochea wananchi kwa kile alichokieleza kwamba ni kujitafutia umaarufu wa kisiasa.
“ Ni kweli kwamba wanakijiji wamegoma kushiriki shughuli za maendeleo; eti waataka nihamishwe kwa madai ambayo ata hayana msingi wowote,” anasema Ofisa Mtendaji huyo na kuongeza; “… Hata hivyo, mimi sijakataa kuhamishwa iwapo mwajiri wangu ataridhia.”
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo hakupatikana kwa njia ya simu ili weze kuzungumzia suala hilo; simu yake haikuwa hewani wakati Mkuu wa Wilaya, Ole Lenga alielekeza suala hilo kwa Mkurugenzi Mtendaji.
“ Suala hilo lipo, lakini linashughulikiwa na DED (Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri); muulize atakuambia kinachoendelea ni nini,” anasema Mkuu wa wilaya hiyo, Ole Lenga.
Taarifa hii imeandaliwa na Juma Ng’oko, aliyekuwa Serengeti


Wanakijiji wagomea kushiriki miradi ya kijiji wakidai taarifa ya fedha | Fikra Pevu | Kisima cha busara!
 
Back
Top Bottom