CHADEMA wasusiwa uchafu Sinza B
na Efracia Massawe
BAADA ya Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda, kuwataka wakazi wa Manispaa hiyo kutunza mazingira, jitihada hizo zimepingwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Sinza (B) kwa kile kinachodaiwa sababu za kisiasa.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti wakazi hao walisema Aprili 9 mwaka huu walihimizana kufanya usafi wakiongozwa na viongozi wa mtaa huo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakiunga mkono jitihda za serikali kutunza mazingira.
Kwa mujibu wa wakazi hao, taratibu zote za kuufahamisha uongozi wa serikali ya mtaa huo juu ya azma yao zilifanyika lakini uongozi huo wa mtaa uliwanyima mifuko ya kuhifadhi taka watakazokusanya ili kuzipeleka maeneo husika kwa taratibu za kila siku.
Tumekusanya uchafu huu unaouona hapa na maeneo mengine lakini gari lilipofika uongozi wa serikali ya mtaa ulituambia tuwaambie CHADEMA watutafutie gari la kuzolea taka hizi kwa kuwa wao ndio walioratibu suala hili la usafi
kwa kweli inatusikitisha sisi wananchi kuona mambo ya msingi yanashindwa kutekelezwa kwa sababu za kisiasa, walisema wakazi hao.
Katika maelezo yao walisema fedha za kuchangia kwa ajili ya usafirishaji wa taka hizo zilikataliwa na uongozi wa mtaa na kuwaacha katika hali ya kutofahamu siku uchafu huo utakapoondolewa.
Aidha Tanzania Daima ilimtafuta kwa njia ya simu mwenyekiti wa mtaa huo Dk. Kessy ambaye alikataaa kulizungumzia suala hilo kwa madai kuwa suala hilo ni la watu binafsi lakini taka zitaondolewa wakati wowote.
Naye Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mwenda alikiri kufahamu juu ya kadhia ya uchafu na kusema endapo suala hilo linafanywa kisiasa wahusika hawawatendei haki wananchi.