mayoscissors
JF-Expert Member
- Nov 24, 2009
- 975
- 479
KATIKA muktadha wa mjadala unaoendelea sasa hivi katika jamii, nimependa kujua walipo baadhi ya wanasiasa hawa waliowahi kuvuma katika vyama vya upinzani.
Yuko wapi Dk. Walid Aman Kabourou? Aliwahi kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya CHADEMA. Amewahi pia kuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA.
Ni mmoja wa wasomi wachache wa awali waliovutiwa na kushiriki siasa za mageuzi. Hivi ndiye alikuwa mbunge wa kwanza wa mageuzi?
Kuna mtu kaniambia kuwa siku hizi Dk. Kabourou ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Eti ndiye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma? Siamini. Naomba wenye kujua zaidi wanieleze.
Nimemkumbuka pia Dk. Masumbuko Lamwai, msomi wa sheria, wakili mahiri aliyewika kisiasa akiwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Mkoa wa Dar es Salaam. Alikuwa pia Mkurugenzi wa Sheria wa chama hicho. Ndiye alikuwa Mbunge wa Ubungo kupitia NCCR-Mageuzi 1995-2000.
Siku hizi hasikiki katika siasa. Hata mahakamani hasikiki kama zamani. Nimesikia naye alishajiunga na kuwa mwanachama wa CCM. Sijasikia kama alipata cheo. Sijui alipo, na alichonacho kisiasa.
Sijamsahau Daniel Nsanzugwanko aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi. Sijui aliko siku hizi, lakini nimeambiwa alishakuwa Mwana CCM, na alipata ubunge wa Kasulu Mashariki (2005-2010), akapata unaibu waziri, baadaye Rais Jakaya Kikwete ‘akamtupa.' Yuko wapi siku hizi?
Wapo wengi lakini nitataja wachache kama mifano. Sitamsahau Thomas Ngawaiya, aliyewahi kuwa Katibu Mwenezi wa Tanzania Labour Party (TLP), na Mbunge wa Moshi Vijijini kupitia TLP.
Nimeambiwa naye alisharejea CCM baada ya kukosana na Augustine Mrema, na sasa amepewa cheo cha Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro.
Namkumbuka pia Tambwe Hiza, aliyewahi kugombea ubunge wa Temeke mara kadhaa kupitia NCCR-Mageuzi na Civic United Front (CUF).
Mwanasiasa huyu machachari, mwenye maneno makali, aliwahi kujiapiza kwa jina la mama yake mzazi kwamba asingeweza kurudi CCM.
Sijui alisahau? Maana nimeambiwa naye siku hizi ni mwanachama wa CCM, na katika miaka michache iliyopita alikuwa amepewa fursa ya kuwa naibu kiongozi wa kitengo cha propaganda ndani ya CCM, Makao Makuu.
Siku hizi simsikii. Nani anayejua Tambwe Hiza yuko wapi, anafanya nini?
Lililo wazi ni kwamba wote hawa na wengine waliofuata mkondo huo, waliwahi kuwa wanasiasa mahiri wapenda mageuzi.
Mambo yalipokuwa magumu, mabadiliko yakawa na mikikimikiki mizito, wakayakimbia, wakaanza kuwa maadui wa mageuzi.
Wakabadilika na kuwa Wana CCM wasioamini katika mabadiliko. Wakashangilia udhaifu wa mfumo mkongwe waliokuwa wanaupinga siku zote. Baadhi yao wakapewa vyeo, wakautumikia. Wakawa wasaliti wa mabadiliko, na mageuzi.
Ndiyo, wameendelea kuishi na kufanya siasa. Lakini heshima yao mbele ya umma si ile ile waliyokuwa nayo. Imeshuka. Ndiyo maana hatuwasikii tena. Hata wanapojaribu kusikika, hawasikilizwi kama ilivyokuwa zamani.
Wamejiua kisiasa. Na baadhi yao bado wanatafuta wengine wa kufa nao kisiasa!
Kubwa kuliko yote ni kwamba jamii haiwaamini tena, maana wamekuwa ni watu wa ndimi mbili kama nyoka. Wanasifia maovu yale yale ambayo wamekuwa wanayachambua na kuyalaani. Wanashambulia wenzao wale wale wanaoshikilia msimamo wa awali, kwa kigezo kuwa wao ni wapenda demokrasia, wenzao ni wahafidhina.
Wanatushangaa na sisi tunaokataa kujiunga nao kushangilia uovu wa mfumo mkongwe, na kushambulia wakosoaji wa mfumo huo. Wamegeuka mabingwa wa kushambulia wana mageuzi na wapenda mabadiliko, na wanataka tuwaamini kwamba wao ndio sahihi.
Hapana. Hebu tuelezane ukweli. Uongozi una sifa nyingi kwa wanaoutaka. Si uwezo wa kifedha. Si umahiri wa kujenga hoja. Si ushawishi kwa umma. Si wingi wa miaka ya kuzaliwa au ya kufanya siasa. Si usomi wa darasani.
Ipo sifa kuu moja ambayo kiongozi au mwanachama yeyote akiikosa, hata kama anazo nyingi zilizobaki, hatapewa uongozi na watu wake.
Sifa hiyo ni kuaminika. Kama huaminiki kwa watu unaowaongoza au wanaopaswa kukupa uongozi, hautaupata.
Na wakikupa fursa hiyo bila kujua, baadaye wakagundua kuwa huaminiki, hata kama una sifa zote zilizobaki, watakunyang'anya fursa hiyo.
Naamini kwamba hawa niliowataja hapo juu, na baadhi ya wanasiasa wenye hulka za namna hiyo, wamepata shida kwa kushindwa kujiaminisha kwa wenzao. Hawakuaminika kwenye vyama vyao vya awali. Baadhi yao wakawahi kujiondoa. Wengine wanaondolewa kwa nguvu au kiufundi. Wengine wakaondoka upinzani na kujiunga ‘CCM kwa sababu ya njaa zao', kama alivyosema mzee Yusuf Makamba siku alipowapokea Dk. Kabourou na Tambwe.
Ndiyo maana hata huko walikokimbilia hawakupata heshima ile ile waliyokuwa nayo wakiwa kwenye upinzani. Baadhi ya waliopewa fursa za uongozi, walinyang'anywa baada ya muda mfupi.
Ndiyo maana wapo wengi waliosahaulika kisiasa. Wamejiua, na wengine wamejizika kisiasa. Usishangae kwamba nauliza: Wako wapi siku hizi? Wana anuani zipi? Wametufunza nini?
Ni wazi, haya si maswali magumu. Lakini je, yanaweza kutufikirisha?
Imeandikwa na Ansbert Ngurumo, Tanzania Daima