Wajibu wa mume kwa mkewe

Amante

JF-Expert Member
Jul 2, 2017
228
216
Habari wanajamvi. Hapa nitazungumzia baadhi tu ya haki za mke kutoka kwa mume ambazo aidha miongoni mwetu hawzifahamu ama wanazifahamu lakini hawazitekelezi. Kutimiza haki hizi kutaongeza mapenzi na uimara wa ndoa.

1) Kuishi naye kwa wema.
Ni wajibu wa mume kuishi na mkewe kwa tabia njema, asiwe na tabia ya kuziumiza hisia za mkewe kwa kumbughudhi kwa kauli chafu au kwa kumtendea matendo yasiyo na chembe ya utu.
Asimbughudhi kiasi cha kumfanya asihisi raha ya ndoa na kupelekea kuiona ndoa kuwa ni mithili ya kifungo.

2) Kuvumilia kero/maudhi.
Ni wajibu wa mume aliyetambua maumbile ya mkewe kustahamilia kero na maudhi anayoweza kuyapata kutoka kwa mkewe.
Ama kwa makusudi au kwa bahati mbaya, kwa sababu ya upungufu wa kibinadamu. Hasa katika kipindi kigumu cha ujauzito.
Yeye mume kama kiongozi wa familia/nyumba siku zote asiangalie matokeo (kero/maudhi), bali daima aangalie chanzo na chimbuko la kero au maudhi hayo.
Kwa nini maudhi haya yako leo na wala hayakuwepo jana? Kwa uchunguzi huu anaweza akajikuta kuwa yeye ndiye aliyetoa mwanya wa kero na maudhi hayo yanayomfika na kumkuta hivi sasa.
Kwa hivyo linalompasa kufanya ni kujaribu kuuziba uchochoro huo wa maudhi ili asipate kuudhiwa akaghadhibika na kuhatarisha ndoa yao.
Mume awe mwepesi kumsamehe mkewe anapomkosea hata bila ya kuombwa msamaha.
Na yeye awe mwepesi pia kumuomba msamaha mkewe anapomkosea.
Sio kwa kuwa yeye ni mwanamume basi hakosei, hivyo sivyo mwanamume pia hukosea kama anavyokosea mwanamke.

3). Heshima na kuthaminiwa.
Ni haki ya mke na ni wajibu wa mume kumthamini na kumpa mkewe heshima zote anazostahiki kama mke, mwandani na msaidizi wa karibu katika maisha kwa mujibu wa sheria.
Mume anatakiwa kumuangalia mkewe kama sehemu yake inayomkamilisha na kumfanya mwanamume kamili atakayeitwa mume, baba na hatimaye babu.
Haya yote yanaonyesha nafasi ya mwanamke kwa mwanamume. Ni nafasi yake hii ukiachilia mbali ubinadamu wake inayomstahikisha heshima na kuthaminiwa sambamba na kutambuliwa utu wake.
Mume asijione kuwa ana haki na kila sababu ya kufanya atakavyo kwa mkewe.
Si haki na wala si sheria mume kumdhalilisha mkewe kwa kumtukana na kumtolea maneno machafu peke yao chumbani, mbele ya watoto au watu wa kando.

4) Mzaha, ucheshi na mchezo.
Ni haki ya mke na ni wajibu wa mume kumtengea mkewe muda maalumu.
Katika muda huo mke apate fursa ya kutoa maoni, nasaha na ushauri kuhusiana na maisha yao na mipango yao ya baadaye.
Mazungumzo ya wawili haya yatiwe kachumbari ya mzahahalali usiofikisha katika maudhi.
Yaambatane na mchezo na ucheshi utakaoyanogesha na kuyafanya matamu maongezi yao hayo. Machoni mambo haya huonekana kuwa ni mambo ya kipuuzi yasiyo na maana.
Lakini ukweli ni kwamba mambo haya yana mchango mkubwa katika kuimarisha mafungamano haya ya ndoa.
Mke ni binadamu kamili mwenye mawazo na maoni juu ya nafsi yake mwenyewe na kwa watu wengine hasa mumewe na familia yake kwa ujumla.
Kama hakupewa fursa na mumewe, akayasemee wapi maoni na mawazo yake haya?! Kama mume hakuwa katika hali ya utayari wa kumsikiliza, akawa katika hali ya furaha, ucheshi, mzaha, je mke atathubutu kumtamkia kitu?!
Ni dhahiri kuwa hataweza, atashindwa, kwa mantiki hii ni muhimu mno kikawepo baina ya wawili hawa kipindi cha mzaha, mchezo na ucheshi.
Ikiwa hukumpa fursa hiyo, maumbile yake yatamsukuma kuitafuta fursa hiyo mahala pengine. Jambo ambalo litaihatarisha ndoa yenu.

5). Mahitaji ya lazima.
Ni katika jumla ya haki za mke zilizo katika dhima ya mumewe kupata mahitaji yake yote ya lazima.
Mume anawajibika kutoa gharama zote za mahitaji ya lazima ya mkewe, ikiwa ni pamoja na chakula bora cha kulinda, kujenga na kutia mwili nguvu.
Ni wajibu wa mume kuhakikisha kuwa mkewe anapata maji safi na salama ya kunywa.
Ampatie mavazi yatakayomfaa katika vipindi/majira yote ya mwaka; nguo za masika na kiangazi.
Ni haki ya mke kupatiwa makazi yatakayomsitiri na kumpa amani na usalama wa nafsi, mali na akili. Kadhalika ni wajibu wa mume kumpa matibabu mkewe anapougua na kushirikiana nae kwa kumliwaza katika kipindi kigumu cha maradhi au ujauzito.

6). Mahari.
Ni haki ya mke na ni wajibu wa mume kwa mujibu wa sheria kumpa mke mahari yake kamili. Kwa kuwa hiyo ni haki yake aliyopewa na Allah Mola Muumba wake.
Mahari ni haki ya mke hata kama ulimpa nyumba, gari, shamba... n.k.kuwa ndio mahari yake. Ukimtaliki na kuoa mke mwingine huna ruhsa kuchukua cho chote katika hiyo mali uliyompa.

7). Haki ya kupata elimu.
Mke ana haki ya kupata elimu ambayo ni wajibu wa mumewe kuhakikisha kuwa anaipata.
Ikiwa mke hakupata elimu ya msingi ya dini yake huko kwao atokako, basi ni jukumu la mume kuhakikisha kuwa mkewe anapata elimu hiyo muhimu.
Amfundishe yeye mwenyewe au amtafutie mtu/mahala ambapo ataipata elimu hiyo. Aanze kufundishwa mambo ya msingi kama vile nguzo za imani na baki ya mambo mengine yanayohusiana na akida (itikadi).
Kisha afundishwe hukumu za mambo ya kisheria yanayomtokea katika maisha yake ya kila siku. Yaani hukumu za twahara, hedhi, swala, swaumu na kadhalika.
Pia si vibaya akipata elimu na taaluma ya ziada itakayoisadia familia kujikimu kimaisha, taaluma itakayomuwezesha kufanya kazi na kuchangia kuongeza pato la familia.
Afanye kazi kwa ridhaa ya mumewe na chini ya mazingira yanayokubaliwa na sheria. Kumbuka mama (mke) ni shule ya familia, kumuelimisha mama ni kuielimisha familia.
Kadhalika ni jukumu na wajibu wa mume kumuhimiza mkewe swala na mambo mengine ya kheri.

8). Kuonewa/kuliliwa wivu.
Ni haki ya mke na ni wajibu wa mume kisheria kumuonea wivu wa kisheria mkewe.
Mume awe na wivu kwa mkewe, wivu utakaokuwa wigo wa kulinda na kuhifadhi utu, cheo, nafasi na utukufu wa mkewe.
Mume anatakiwa asighafilike na kutoa mwanya ambao unaweza kuwa ni sababu ya fisadi itakayopelekea kulegalega au pengine kuvunjika kwa ndoa yao.
Naam, ni kweli mume anatakiwa kuwa na wivu kwa mkewe, lakini si haki wala sheria kupindukia katika wivu.
Wivu utakaomtumbukiza katika lindi la dhana mbaya dhidi ya mkewe.
Dhana hizi zikamgeuza kuwa kachero na jasusi wa kuchunguza nyendo na pengine mambo ya ndani kabisa ya mkewe.
Huku si kuutekeleza wajibu wako kwa mkeo, wala huambiwi kuwa ndio unampenda sana mkeo. Wivu huu wa kupindukia ni ugonjwa unaoweza kuondosha masikilizano na maelewano ndani ya nyumba.
Na mahala pake kutawaliwa na mizozo na gubu lisilokwisha. Pengine wivu wa namna hii unaweza kuwa kichocheo na kumuamshia mke ari ya kufanya uchafu anaoshukiwa kuufanya na kumbe masikini hana khabari nao kabisa.


UZI UNAOFATA NITAZUNGUMZIA HAKI ZA MUME KUTOKA KWA MKE.
 
Tunayatekeleza sana haya,ila wengine hawana shukrani
Ni kweli unayosema mkuu lakini yapasa kumvumilia na kumfundisha mema ipo siku atabadilika na kushukuru. Me ninachoamini ukiishi kwa kufata sheria na misingi ya kiimani basi utafanikiwa katika mambo yako hivyo jaribu kumpa mafunzo ya kiimani.
 
Back
Top Bottom