Wagombea watano wapeta | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wagombea watano wapeta

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by MziziMkavu, Jul 5, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Jul 5, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,616
  Likes Received: 4,617
  Trophy Points: 280
  [​IMG] Watatu wabanwa kwa hoja nzito, wajitetea
  [​IMG] Wengine wapata mteremko wa kujieleza
  [​IMG] Walihojiwa chini ya ulinzi mkali wa dola  [​IMG]
  Waziri Kiongozi Mstaafu, Gharib Bilal

  [​IMG]
  Makamo wa Rais Dk. Ali Mohammed Shein

  [​IMG]
  Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha

  [​IMG]
  Haroun Suleiman

  [​IMG]
  [​IMG]
  [​IMG]
  [​IMG]
  [​IMG]
  [​IMG]  Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar imependekeza majina matano kati ya wagombea 11 walioji tokeza kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar, katika mchujo uliofanyika mjini hapa jana.
  Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zimesema vigogo hao watano wamependekezwa baada ya kikao hicho kumaliza kazi ya kuwajadili wagombea wote waliojitokeza kuwania nafasi hiyo, chini ya Mwenyekiti wa kikao hicho Rais Amani Abeid Karume.
  Wagombea waliopendekezwa ni pamoja na Waziri Kiongozi Mstaafu, Gharib Bilal, Makamo wa Rais Dk. Ali Mohammed Shein, Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Haroun Ali Suleiman na Naibu Waziri Kiongozi Ali Juma Shamuhuna.
  Wakizungumza na Nipashe Jumapili baadhi ya wajumbe wa kikao hicho wamesema kwamba kila mgombea alipewa dakika tatu za kujieleza kuulizwa maswali matatu na wajumbe wa kikao hicho.
  Majina ya wagombea hao ndio yatakayopewa uzito katika suala zima la kutafuta mgombea mmoja katika vikao vya kamati kuu na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) ambacho kitapokea majina matatu kutoka Kamati Kuu (CC).
  “Kazi haikuwa ndogo majina ya watu watano yamepitishwa na kikao ingawa majina ya wagombea wote waliojitokeza yatapelekwa kamati kuu”, alisema mjumbe mmoja ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake.
  Hata hivyo, alisema wagombea hao hawajaekewa alama kama ilivyozoeleka miaka ya nyuma isipokuwa Sekretariet imetakiwa kupanga orodha ya majina wakiwemo watano waliopitishwa pamoja na wagombea wengine.
  Katika kikao hicho wagombea watatu walibanwa kwa maswali na wajumbe baada ya hoja nzito kujitokeza akiwemo Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha, Makamo wa Rais Dk. Ali Mohammed Shein na Waziri Kiongozi Mstaafu Dk. Mohammed Gharib Bilal.
  Wajumbe wa kikao hicho walitaka kujua suala la Makamo wa Rais Dk. Shein kutojiandikisha katika daftari la wapiga kura wa kudumu Zanzibar, lakini Dk. Shein alisema kwamba mgombea hapotezi sifa za kisheria kwa kutojiandikisha katika daftari hilo la wapiga kura.
  Alisema kwamba ni kweli wamejiandikisha Tanzania Bara lakini bado sheria inampa uwezo wa kuhamisha kura yake kutoka kituo alichojiandikisha hadi kingine na kuwataka wajumbe wa kikao hicho kuondoa wasiwasi kuhusiana na suala hilo.
  Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zimedai kuwa Waziri Kiongozi Nahodha alitakiwa kukieleza kikao alikusudia nini nafasi yake ya uongozi kujilinganisha na kondakta wa daladala alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.
  Hata hivyo, Shamsi alijieleza kwa umakini na kikao chote kubakia kimya baada ya kufafanua kauli yake na kueleza kwamba katika masuala ya utawala kuna mwamuzi wa mwisho na wengine wasaidizi na kutoa mfano wa yeye sio mwamuzi wa mwisho.
  Alisema kwamba aliamua kujilinganisha nafasi yake na kondakta wa daladala na kutoa mfano kila chombo mwenye maamuzi ya mwisho ni dereva na sio kondakta, jambo ambalo halina tofauti katika masuala ya uongozi akimainisha kuna waziri Kiongozi na Rais na ndio maana akajitokeza kuomba nafasi hiyo, ili aweze kukamilisha yale ambayo hayajakamilishwa na rais wa awamu ya sita.
  Katika kikao hicho vuta nikuvute ilikuwa kwa mgombea Waziri Kiongozi Mstaafu na baadhi ya wajumbe wa Kikao hicho ambapo walilazimika kuvutana kwa zaidi ya saa mbili, baada ya mgombea huyo kutakiwa ajieleze, kwanini alifanya sherehe baada ya kurejesha fomu na kutumia maskani ya CCM kinyume na maelekezo yaliyokuwa yameelekezwa na chama wagombea kutotumia majengo yake.
  Hata hivyo Dk. Bilal imedaiwa alilifafanua kwa umakini suala hilo kwa kuwaeleza kuwa mkusanyiko huo hakuutayarisha yeye ni wanachama wenyewe waliamua kukusanyika na yeye kuwashukuru kwa kujitokeza kwao, jambo ambalo haoni kama ni kosa.
  Aidha wajumbe wa kikao hicho walitaka kufahamu msimamo wake na vitisho vinavyotolewa na wana CCM Zanzibar kuhusu kutopiga kura kama jina lake halitarudi, lakini Dk. Bilal alijieleza kwa kina na kutaka wajumbe wasimhusishe na masuala yasiyomhusu kwa vile yeye amekuwa akitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia taratibu na kanuni za chama.
  Hata hivyo, wagombea wengine walipata mteremko wa kujieleza na kuondoka bila ya kuulizwa masuali akiwemo Mfanyabiashara Mohammed Raza, lakini mgombea Muhamadi Yussuf Mshamba alibanwa kidogo na kikao hicho kuhusu tathmini yake aliyoitoa ya kueleza kuwa Zanzibar haina mipango mizuri ya kiuchumi wakati kuna mpango wa kukuza uchumi na kupunguza Umasikini kwa wananchi wa Zanzibar (MKUZA).
  Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zimesema Makamo Mwenyekiti wa CCM rais Amani Abeid Karume, amewataka viongozi wa chama kujenga umoja ili kuhakikisha chama kinashinda katika uchaguzi mkuu ujao.
  Alisema hivi sasa kuna makundi ya wagombea lakini chama baada ya kuchagua mgombea mmoja wa nafasi ya urais wa Zanzibar makundi yote yavunjwe na nguvu zote zielekezwa kwa kukihakikishia chama ushindi.
  Wakati huo huo, habari za awali zilieleza kuwa
  Ofisi za Makao Makuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui mjini Zanzibar, jana zilikuwa chini ya ulinzi mkali wa askari wa Kutuliza Ghasia (FFU) na Usalama wa Taifa, wakati wagombea 11 waliojitokeza kuwania urais wa Zanzibar kupitia CCM walipokuwa wakihojiwa na Kamati Maalum ya Halmshauri Kuu ya chama hicho Zanzibar.
  Askari hao walionekana wakiwa wamejipanga katika lango kuu la kuingilia ofisi hizo na kuruhusu magari ya wajumbe wa NEC tu, huku watu wengine wakizuiwa wakiwemo waandishi wa habari na wapambe wa wagombea.
  Miongoni mwa walioathirika na hali hiyo ni wapambe wa wagombea ambao walishindwa kuwasindikiza wagombea wao na hivyo idadi kubwa kuamua kuchukua uamuzi wa kusafiri kuelekea Dodoma kupiga kampeni za mwisho kabla ya mchujo wa mwisho kufanyika.
  Hali ilikuwa ngumu zaidi kwa waandishi wa habari ambao walishindwa kufanyakazi zao vizuri baada ya kuzuiwa kulisogelea eneo hilo.
  “Waandishi hamruhusiwi kuingia ndani ya Makao Makuu ya CCM na tunawaomba muondoke kabisa eneo hili hadi hapo mtakapohitajika”, alisema Afisa mmoja wa Usalama wa Taifa, wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili.
  Wagombea hao walianza kuwasili ofisi hizo majira ya saa 3:00 asubuhi wakiwa na wapambe wao.
  Viongozi wote wa kitaifa wa CCM walihudhuria mkutano huo wa jana kasoro Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk. Salmin Amour Juma ambae hakuonekana kabisa katika kikao hicho kizito ingawa anadaiwa yuko Zanzibar.
  Miongoni mwa viongozi waliohudhuria kikao hicho ni Rais Mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi, ambae alionekana akiwa mchangamfu wakati akiingia, Waziri Mkuu Mstaafu Salim Ahmed Salim, Makamu wa Rais Dk. Ali Mohammed Shein, Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha, Naibu Waziri Kiongozi Ali Juma Shamuhuna na Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho.
  Mwenyekiti wa kikao hicho Rais Amani Abeid Karume aliwasili saa 4:00 asubuhi wakati wajumbe wote wakiwa wamewasili wakiwemo wagombea.
  “Tulipokea barua ya wito na kutakiwa tuhudhurie kikao hiki jana jioni ndio maana tumefika, sifahamu kama tutahojiwa kabla ya majina kupelekwa Dodoma”, alisema mgombea mmoja wa nafasi ya Urais wa Zanzibar ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
  Wakati hayo yakitokea, habari zinasema kuwa Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk. Salmin Amour Juma alifanya mazungumzo zaidi ya saa nne na Rais Jakaya Kikwete nyumbani kwake Dar es Salaam wiki iliyopita.
  Taarifa za uchunguzi zimedai kwamba Dk. Salmin ndie aliyesafiri kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam kwa madhumuni ya kufanya mazungumzo na kiongozi huyo wa ngazi ya juu katika chama cha CCM na kwamba suala la mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar linadaiwa lilitawala mazungumzo yao.
  Chanzo kimoja cha habari kilicho karibu na kiongozi huyo mstaafu kimesema kwamba mazungumzo yao yalikuwa marefu na yaligusa zaidi hali ya kisiasa ya Zanzibar katika kumpata mgombea wa nafasi ya urais baada ya Rais Amani kumaliza muda wake.
  “Baada ya kupokea ombi kutoka kwa Rais Kikwete la kutaka kuonana nae, Dk. Salmin alimwambia yeye ndie atakayemfuata asipate taabu,” kilisema chanzo hicho kutoka nyumbani kwa Rais huyo mstaafu wa Zanzibar maeneo ya Migombani.
  Wagombea watatu jana mchana walikuwa wa kwanza kutoka katika kikao hicho wakiongozwa na Waziri Kiongozi Mstaafu Dk. Mohammed Gharib Bilal, ambae alikuwa wa kwanza kuondoka eneo hilo na kufuatiwa na mfanyabiashara Mohammed Raza Dharamshi na baadaye Naibu Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mohammed Aboud.
  Kikao hicho hadi jana jioni kilikuwa kikiendelea kuwapitia wagombea waliobaki kwa kuangalia sifa na vigezo vinavyotakiwa.
  Wagombea karibu wote walionekana wachangamfu hasa walipokuwa wakiingia katika kikao hicho.
  Wagombea 11 wanaowania kusimamishwa na CCM kuwania urais wa Zanzibar ni Makamu wa Rais Dk. Ali Mohammed Shein, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Haroun Ali Suleiman, Mwanadiplomasia Muhammadi Yussuf Mshamba, Balozi Ali Karume, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Omar Sheha na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Hamad Bakar Mshindo.
  Wengine ni Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, Naibu Waziri Kiongozi Ali Juma Shamuhuna, Waziri Kiongozi Mstaafu, Mohamed Gharib Bilali, Mfanyabiashara Mohammed Raza Dharamshi na Naibu Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mohammed Aboud.
  Wakati hayo yakiendelea, wanachama wa CCM Zanzibar wamekuwa katika mjadala mzito kuhusu nani atakuwa mgombea wa urais wa Zanzibar, huku waziri Kiongozi Mstaafu Dk. Mohammed Gharib Bilal akitawala mijadala hiyo kati ya wagombea waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.
  Mwanachama wa CCM tawi la Mgandini wilaya ya mjini Unguja Juma Soud Said ambae ni mkazi wa Kwamtipura alisema yeye binafsi anapendelea Dk. Mohammed Gharib Bilal kwa sababu ni kiongozi mwenye uzoefu na wanafahamu uwezo wake katika masuala ya utawala.
  Kwa upande wake, mwanachama mwingine, Simai Makame tawi la Kwamtipura, alisema kwamba ni mapema kutoa msimamo kuhusu wanamtaka nani hadi hapo chama kitakapotoa maamuzi ya mwisho.
  “Mimi sina la kuamua bali kama halikuja jina la Bilal basi nitafuata maamuzi ya wana CCM yatakayoamuliwa wakati huo”, alisema.
  Hata hivyo, mwanachama wa CCM Imamu Mganga, tawi la Kwamtipura Zanzibar, alisema ni vizuri kati ya wagombea waliojitokeza akapatikana mgombea ambae hajawahi kupata nafasi ya juu ya uongozi.
  Alisema idadi kubwa ya viongozi waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ya urais wa Zanzibar wamewahi kuwa viongozi wa juu na wameshindwa kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi.
  Alisema Zanzibar hivi sasa wananchi wake wanakabiliwa na matatizo ya umasikini kutokana na sera mbovu za kiuchumi, hivyo ni wakati muafaka kuchaguliwa mtu ambae hajawahi kushika nafasi ya juu ya uongozi katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili alete mabadiliko.
  Mwanachama mwingine Ramadhan Abdallah wa tawi la Kilimahewa alisema mgombea yoyote atakaeteuliwa na chama ndie atakaemuunga mkono kwa vile mamuzi ya chama ndio ya mwisho.
  Alisema kwa kuwa vikao vya CCM vinahudhuriwa na wazee wenye busara mgombea wa urais wa Zanzibar ana imani kuwa atachaguliwa mtu anaekubalika kwa wananchi hasa kwa kuzingatia hivi sasa Zanzibar iko katika ushindani mkubwa wa kisiasa na vyama vya upinzani.
  Aliyekuwa Katibu wa CCM mkoani Tanga, Baraka Shamte, alisema kwamba vikao vya CCM vinahitaji umakini mkubwa katika kumpata mgombea wa nafasi ya Urais wa Zanzibar, baada ya kujitokeza wanachama wengi kuwania nafasi hiyo.
  Alisema CCM itakuwa katika wakati mgumu wa uchaguzi mwaka huu, iwapo itashindwa kusoma alama za nyakati na kuchagua mgombea ambae sio chaguo la wanachama walio wengi wa CCM Zanzibar.
  Wakati hayo yakiendelea visiwani Zanzibar, habari zinasema makundi ya wana CCM wenye mpango wa kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015, yameanza kufanya kampeni kali kwa wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM kuhakikisha kuwa watu wanaowaunga mkono wanapitishwa na vikao hivyo vya juu vya chama kuwania urais wa Zanzibar.
  Habari hizo zinaeleza kuwa wagombea hao wameunda mitandao kwa ajili ya kuwashawishi wajumbe wanaotoka Zanzibar na Tanzania Bara wapitishe majina ya wagombea wao ili wakishinda waje kuwasaidia kuungwa mkono upande wa Zanzibar wakati wa uchaguzi wa 2015.
  Chanzo cha uhakika kutoka moja ya kambi hizo, kimeliambia gazeti hili kuwa kampeni hizo ambazo zinafanyika kupitia vikao vya siri na kumfuata mgombea mmoja mmoja, na kwamba kampeni za wazi zilionekana wakati wa kikao cha NEC kilichofanyika mjini Dodoma hivi karibuni.
  Julai 9, kitendawili cha nani kuwa Mgombea Urais wa Zanzibar kitateguliwa mjini Dodoma.
  Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar unatarajiwa kufanyika Oktoba 31, baada ya Rais Aman Abeid Karume, kumaliza muda wake kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar.
  Habari hii imeandiskwa na Mwinyi Sadallah, Zanzibar na Abdallah Bawazir
  CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
   
 2. Mkosoaji

  Mkosoaji JF-Expert Member

  #2
  Jul 5, 2010
  Joined: Aug 24, 2009
  Messages: 363
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Kazi ipo visiwani. Huu upepo unampuliza vizuri Shein.
   
Loading...