Wachina wajizolea dhahabu ya Chunya watakavyo

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,015
Sakata la Wachina wanaojizolea dhahabu Chunya 'lanoga'

Felix Mwakyembe, Mbeya
Raia Mwema
Juni 16, 2010

bul2.gif
Serikali yakiri kutopata kitu


bul2.gif
Wananchi wadai kuathirika kisaikolojia na kiafya



bul2.gif
Mkuu wa Mkoa aagiza wananchi wawashughulikie wakionekana




HATIMAYE Serikali imesitisha shughuli za uchimbaji madini ndani ya Mto Zira na Lupa katika Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya zilizokuwa zikifanywa na Kampuni ya Kichina ya EPOCH Mining; ikiwa ni wiki mbili tu baada ya gazeti hili la Raia Mwema kufichua habari hizo katika ripoti yake maalumu.

Hata hivyo, wakati Serikali ikichukua hatua hiyo, bado kuna hoja kadhaa zinazohitaji maelezo ya kina; nazo ni pamoja na nani atahusika na hasara itokanayo na uharibifu mkubwa wa mazingira uliokwishafanywa na kampuni hiyo, na nani atawajibika kutibu uharibifu huo uliokwishafanyika na kampuni hiyo.

Nyingine ni kwa namna gani jamii itafahamishwa kiwango halisi cha dhahabu walizokwishajichotea Wachina hao, na nani atawajibika kulipa stahili mbalimbali za kodi kwa mamlaka husika kwa dhahabu waliyokwishajichotea.


Maswali mengine ni pamoja na ni nani hasa aliyewapa kiburi Wachina hao cha kuvamia raslimali za nchi kinyume cha sheria na taratibu za nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, anathibitisha kuhusu serikali kutofaidika na mradi huo pale anaposema: "Serikali haijapata kitu na wala hatujui wamechimba kiasi gani."

Wakati mkuu huyo wa mkoa akibainisha hayo kwenye mkutano wake na wananchi wa Kijiji cha Ifumbo alipotembelea eneo hilo, wiki iliyopita, Ofisa Madini Mkazi, Wilaya ya Chunya, Juma Sementa, anaelezea hatua walizokwisha chukua akisema: "Mbali ya kusimamishwa, kampuni hiyo itawajibika kuyatibu mazingira ya mito hiyo ambayo wameyaharibu na kwamba wamekubaliana na sharti hilo. Kazi ambayo inatarajiwa kuwachukua sio chini ya miezi mitatu. Ni zoezi litakalowachukua muda mrefu kidogo…. kuyarudisha yale mawe sio mchezo. Ni zoezi litakalowagharimu sana." Ni wazi kwamba Serikali inayo majibu ya hoja hizo, lakini hofu ya wadau wa mazingira ni utekelezaji wa kweli wa maagizo hayo, na wakati huo huo bado inabaki hoja moja muhimu ambayo ni madhara ya kijamii na kisaikolojia yanayowakabili wananchi waishio kwenye vijiji vilivyomo kwenye Bonde hilo la Mto Lupa.

Katika kipindi ambacho wageni hao wameishi huko, yapo madai ya kuwepo madhara ya kiafya kama vile watu wanaougua matumbo baada ya kunywa maji yanayodaiwa na wanavijiji hao kuwa na kemikali na kinyesi. Madai mengine ni unyanyasaji watoto. Madhara ya kijamii, kisaikolojia na kiafya ndiyo kilio kikubwa hivi sasa kwa wananchi katika vijiji hivyo kiasi cha kufikia uamuzi wa kupambana na wageni hao; kama anavyoeleza mwanakijiji wa Ifumbo, Elias Ngwaya:
"Kwenye mkutano mkuu tuliazimia kupigana nao moja kwa moja. Kazi zao hazieleweki. Ndugu mwandishi wa habari, nikwambie ukweli kwamba wananchi walifika siku moja na mashoka na mapanga na kuwafukuza. Hivi sasa tunapanga tuwavamie twende kuwafukuzilia mbali……." Mwananchi mwingine wa kijiji hicho, Charles Abraham analalamika akisema: "Hawa Wachina hawana vyoo. Wanajisaidia kwenye mito na porini. Ukiwauliza wanasema; Sepacho (Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Chunya) kawaleta."


"Lakini sote tunajua kuwa mitambo yao inaua viumbe hai na kuharibu kingo za mito. Aidha, wamesababisha magonjwa ya kipindupindu. Kilianzia kijiji cha Ikukwe ambako tayari watu wawili wamekufa akiwemo Mwene Mwanda." Hoja hizi za wananchi waishio kwenye bonde hilo la Mto Lupa hazijajibiwa na barua kutoka Ofisi ya Maji, Bonde la Ziwa Rukwa iliyosainiwa na afisa wake, L.W. Mbuya ya tarehe 31/05/2010 ikiwa na Kumbu. Na. LRB/S.10/16/Vol II/87.

Katika barua yake hiyo yenye kichwa cha habari :"Kusitisha Shughuli za Uchimbaji wa Madini Ndani ya Mto Zira na Lupa", Mbuya anaagiza akisema: "Maafisa kutoka ofisi ya Maji Bonde la Ziwa Rukwa walifanya ukaguzi katika vyanzo vya maji na kukuta Kampuni yako ya EPOCH MINING ikifanya shughuli za uchimbaji madini ndani ya Mto Zira na Lupa iliyo wilayani Chunya katika Bonde la Ziwa Rukwa ambapo kisheria ni makosa kufanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji na kutumia maji bila kuwa na kibali." Maelezo ya Afisa huyo wa Maji, Bonde la Ziwa Rukwa yanathibitisha kile kilichoripotiwa na Raia Mwema juma lililopita kuhusu kuwepo kwa kampuni hiyo ikiendesha uchimbaji dhahabu ndani ya mito wilayani Chunya kinyume cha sheria ambapo walibainika kutokakuwa na kibali cha matumizi ya maji na kile cha tathmini ya mazingira.

Katika barua yake hiyo, Mbuya ananukuu sheria za maji na mazingira akisema: "Sheria ya maji namba 11 ya mwaka 2009 kifungu namba 34 na 43 pia sheria ya mazingira namba 20 ya mwaka 2004 kifungu namba 157 (1), haziruhusu kufanya shughuli zozote za kibinadamu zinazosababisha uharibifu na uchafuzi wa vinazo vya maji," kisha anamalizia kwa agizo akisema: "Kwa mujibu wa kanuni na sheria zilizotajwa hapo juu, kuanzia sasa unatakiwa kusitisha mara moja shughuli hiyo ya uchimbaji madini ndani ya mito hiyo kwa sababu shughuli hizo ni kinyume na sheria ya maji."

Barua hiyo inayowasitisha Wachina hao kuendelea na uchotaji wa dhahabu kwenye mito ya Wilaya ya Chunya, hata hivyo, haielezei wajibu wa kampuni hiyo katika kuyatibu mazingira iliyokwisha kuyaharibu wala kuonyesha adhabu wanayostahili kutokana na hatua yao ya kuvunja sheria za nchi na malipo (kodi) kwa mali walizochuma.

Miongoni mwa uharibifu uliofanyika kwenye mito hiyo ni pamoja na uharibifu wa uoto wa asili kwenye kingo za mito ambapo kampuni hiyo imeng'oa miti. Miti mikubwa walitumia mashine kuikata na haieleweki walikokuwa wakipeleka magogo ya miti; tena bila ya kibali cha afisa maliasili.

Wamehamisha na kufunga mto kutoka kwenye mkondo wake wa asili, maji yametuama na machache kutoka katika maji yale yaliyopita kwenye mitambo yao yanapenya yakitafuta njia nyingine, tofauti na ile ya asili na ndio hayo maji yanayoenda kutumiwa na wananchi.

Pengine majibu yanaweza kupatikana kupitia Wizara ya Nishati na Madini kutokana na maelezo ya waziri wake, Wiliam Ngeleja, kwamba kuna uchunguzi unaoendelea kubaini sababu za kampuni hiyo kuvunja sheria za nchi ili hatua ziweze kuchukuliwa.

"Leseni imesimamishwa, na sasa uchunguzi unaendelea kubaini sababu za kampuni hiyo kuvunja sheria. Baada ya hapo ndipo serikali itaweza kuchukua hatua za kisheria. Unajua ile leseni ilisitishwa hata kabla ya stori kutoka," anasema Waziri Ngeleja katika mahojiano kwa njia ya simu na Raia Mwema akiwa Dodoma.

Na alipoulizwa iwapo sitisho analozungumzia ni lile lililotolewa na Mamlaka ya Bonde la Ziwa Rukwa alifafanua akisema: "Hiyo ni hatua kwa upande wa Wizara ya Maji ambao ndio wasimamizi wa maji, sisi kwa upande wetu (Wizara ya Nishati na Madini) nasi tumewasimamisha kuendelea na uchimbaji kama wasimamizi wa madini." Lakini kinachoshangaza wananchi hivi sasa, ni misimamo ya viongozi mbalimbali wa Serikali inayotolewa baada ya habari ya kampuni hiyo ya Kichina wilayani Chunya kuchapishwa Raia Mwema, purukushani za aina yake zimeibuka.

Kila kiongozi wa Serikali sasa anataka kuonyesha makucha yake. Ni kama vile Wachina wale waliibuka tu kwenye hiyo mito au waliteremka kwa ‘ungo' pasipo kuonekana; wakati ukweli ni kwamba walipita kwenye barabara zetu hizi hizi wakiwa na magari makubwa yaliyobeba makontena yakiwa na vifaa vya mitambo yao! Miongoni mwa viongozi wa Serikali walioenda kujionea wenyewe mara baada ya habari hiyo kuchapishwa na Raia Mwema, ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Deodatus Kinawiro kabla bosi wake wa mkoa, John Mwakipesile naye kutembelea mradi huo Juni 10, mwaka huu.

Katika maelezo yake, Mwakipesile anakiri wao kama viongozi kutofahamu lolote kuhusu mradi huo, anasema: "Uharibifu ni mkubwa. Hii ni aibu hata kwa serikali yao wenyewe ya China. Hapa Serikali haijapata kitu. Hatujui mpaka sasa wamechimba kiasi gani!"

Lakini mkuu huyo wa mkoa hakuishia hapo bali alienda mbali zaidi akiagiza: "Sio kusimama tu kuchimba, hawa waondoke kabisa eneo hili hadi hapo tutakapo wasiliana na Wizara. Hawa wana maarifa zaidi lakini hawajatuzidi akili, waondoke, mkiwaona wachapeni."

Madhara mengine yatokanayo na shughuli za kampuni hiyo ni uharibifu wa miundombinu kama anavyobainisha Jane Manase wa Kijiji cha Ifumbo anaposema: "Wamebomoa madaraja, walipitisha mitambo yao, sasa madaraja yameweka nyufa. Serikali ya kijiji iliwazuia lakini wanaendelea kupitisha makontena yao." Utafiti ulofanywa huko nyuma na Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) wakishirikiana na kampuni ya Kirusi inayofahamika kwa jina la Russian Technoexport ulibaini kuwepo kwa wastani wa meta za ujazo 2,116,130 za malighafi zenye uwezo wa kuzalisha kilo 1,547.16 ya hiyo dhahabu aina ya alluvial. Ni wazi kwamba kiwango hicho cha akiba ya dhahabu hiyo aina ya alluvial ndiyo iliyoihamasisha kampuni hiyo ya Kichina kupeleka mitambo ile mikubwa kuichimba. Na ni wazi vile vile baada ya kubaini udhaifu uliopo katika usimamizi wa raslimali nchini, hawakuona sababu ya kufuata sheria za nchi wala masharti ya leseni yao; hususani kuhusu ajira.

Wakati wageni hao wakiondoka na utajiri huo, wenye rasilimali hiyo ambao ni wananchi wa vijiji vilivyomo kwenye Bonde la Mto Lupa; hususan vijiji vya Ifumbo na Lupa Market, wameachiwa maumivu ya watoto wao kubakwa na kulawitiwa, uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwemo ukataji miti mikubwa, mashimo yenye kina cha zaidi ya mita kumi tano chini ya mito na umasikini unaojidhihirisha kwenye mazingira ya Shule ya Msingi Lupa Market.

Shule hiyo ya Msingi Lupa Market ipo takribani Kilometa tano kutoka eneo lililokuwa likichimbwa dhahabu na kampuni hiyo ya Kichina. Wanafunzi wake wa madarasa ya kwanza na pili wanasomea chini ya mti wa mwembe kutokana na shule hiyo kuwa na vyumba viwili tu vya madarasa ambavyo vinatumiwa na madarasa ya tatu hadi saba kwa kupokezana.

Kwa mara ya kwanza habari za Kampuni hiyo zilichapishwa kwenye Raia Mwema ya Juni 2, mwaka huu, ikihusu Wachina zaidi ya 13 kuvamia Mto Lupa na Zira katika Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya wakiwa na mitambo ya kisasa kwamba wanajichotea dhahabu kwa gharama ya maisha ya Watanzania masikini waishio kwenye vijiji vilivyomo kwenye mabonde ya mito hiyo.
Wachina hao walikuwa ni kutoka Kampuni ya uchimbaji madini ya Epoch Mining Tanzania Ltd ambayo imeweka mitambo minne, miwili katika kila mto, inayoelea mithili ya pantoni ambayo wenyewe wanaiita ‘meli'.

Mito hiyo ambayo uchimbaji huo wa madini ulikuwa ukifanyika inapita katika vijiji zaidi ya 12. Kwa ufupi, Mto Lupa unaingia katika Mto Zila ambao nao mbele ya safari yake huingia katika Mto Songwe ambao hatimaye hupeleka maji yake kwenye Ziwa Rukwa.

Kwa kutumia mitambo yao hiyo inayoelea, Wachina hao wanapasua miamba na kufukua mawe chini ya mito, huyapandisha juu kwa mkanda maalumu wa vyuma wenye mabakuli ambayo huyachambua mawe na kuyatupa kando, kisha huchekecha na kuyabakiza mawe au mchanga wenye dhahabu.

Hata hivyo, sio kwamba Wachina hao walivamia.
Kampuni hiyo ya EPOCH Mining (T) Ltd inaendesha shughuli hizo kwa kutumia leseni Na. ML 207/2005, iliyotolewa kwa Kampuni ya KAMAKA CO. LIMITED ya jijini Dar es Salaam Machi 10, 2005 na Waziri wa wakati huo wa Madini na Nishati, Daniel Yona.
Leseni hiyo ilihamishiwa kwa Kampuni hiyo ya EPOCH Mining (T) Ltd Desemba 22, 2009 kwa barua iliyotiwa saini na Kamishina wa Madini, Dr. Dalaly P. Kafumu baada ya wamiliki hao wapya wa leseni hiyi kuliopia malipo ya uhamisho ya Dola za Kimarekani 200, (nyaraka zote tunazo).
Meneja wa Mradi huo wa Chunya kutoka Kampuni hiyo, Danny Zhu aliambia Raia Mwema kwamba walianza kazi ya uchimbaji dhahabu kwenye mito hiyo Aprili mwaka huu baada ya kukamilisha upelekaji mitambo na vifaa vingine eneo la mradi.
Akizungumzia suala la uchambuzi wa mazingira (Environmental Impact Assessment E.I.A), Meneja huyo alisema, "Kwanza kibali tumepewa na madini Dar es Salaam, tunayo leseni, ilitolewa mwaka 2009. Hiyo E.I.A siijui, labda bosi wetu Dar es Salaam anajua." Taarifa za kuanzia mwaka 2005 hadi 2008 zilizopo kwenye ofisi za Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, hazionyeshi Kampuni hiyo kwamba iliwahi patiwa cheti na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira kama sheria inavyoelekeza. Mratibu wa NEMC Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Joachim Kessy anafafanua kuwa wataalamu wa kufanya E.I.A husajiliwa na Baraza hilo na kwamba mwekezaji huwaomba hapo na kisha huenda kwenye eneo la mradi kwa gharama za mwekezaji mwenyewe ikiwa ni kwa mujibu wa sheria ya Mazingira Na 20 ya mwaka 2004 cap 191.

~**~**~**~**~**~**~**~**~**~**~**~**~**~**~**~**~**~**~**~**~




Wachina wajizolea dhahabu ya Chunya watakavyo

Felix Mwakyembe
Raia Mwema
Juni 2, 2010

bul2.gif
Waweka mitambo ya kuchimbia dhahabu mitoni


bul2.gif
Waharibu mazingira, wazuia mito



bul2.gif
Hakuna kiongozi au afisa wa serikali anayewafuatilia





WACHINA zaidi ya 13 wamevamia Mto Lupa na Uvira katika Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya. Wakiwa na mitambo ya kisasa, wanajichimbia dhahabu kwa gharama ya maisha ya Watanzania masikini waishio kwenye vijiji vilivyomo kwenye mabonde ya mito hiyo.

Hawa ni kutoka kampuni ya uchimbaji madini ya Epoch Mining Tanzania Ltd ambayo imeweka mitambo minne; yaani miwili katika kila mto. Mitambo hiyo inaelea majini mithili ya pantoni na wenyeji wanaiita meli.

Kuyafikia maeneo hayo ya mito Wachina wanakochimba hiyo dhahabu, unalazimika kusafiri Kilometa takribani 50 kutoka Chunya mjini au Kilometa 45 kutoka katika Kijiji cha Kiwanja, Kilometa chache kutoka Chunya Mjini katika barabara iendayo jijini Mbeya.

Unachepukia hapo katika Kijiji cha Kiwanja na kuanza safari kuelekea kwenye vijiji vya Ifumbo na Lupa Market walipo Wachina hao "wakijivunia mali katika shamba la bibi". Ni shughuli pevu kufika huko; kwani ni kupanda na kuteremsha milima. Bila ya kudokezwa na mtu, sio rahisi kuelewa uwepo wa wageni hao wanaojibebea mali za Watanzania pasipo uangalizi wowote.

Unapozungumza nao unapata ujumbe mzito na ulio wazi. Ni kama vile wanasema: "Tunachojali sisi ni mali, mambo ya mazingira hayatuhusu, hayo ni yenu ninyi."

Mito hiyo wanakofanya uchimbaji huo wa madini inapita katika vijiji zaidi ya 12. Kwa ufupi, Mto Lupa unaingia katika Mto Zila ambao nao mbele ya safari yake huingia katika Mto Songwe ambao hatimaye hupeleka maji yake kwenye Ziwa Rukwa.

Kwa kutumia mitambo yao hiyo inayoelea majini, Wachina hao wanapasua miamba na kufukua mawe chini ya mito na kuyapandisha juu kwa mkanda maalumu wa vyuma wenye mabakuli ambayo huyachambua mawe na kuyatupa kando; kisha huchekecha na kuyabakiza mawe au mchanga wenye dhahabu.

Mkazi mmoja wa Kijiji cha Lupa Market (jina linahifadhiwa) aliambia Raia Mwema kuwa, kwa uelewa wake wa masuala ya uvunaji dhahabu ya alluvia; ile ni mitambo ya kuchenjua dhahabu yenye uwezo wa kwenda zaidi ya mita 15 chini.
"Ile ni mitambo mikubwa ya kuchenjua dhahabu. Inaenda chini hadi mita 15, kwa hiyo hivi sasa hatuna uhakika na uvukaji kwenye maeneo haya. Kabla hawajaanza uchimbaji huo, tulivuka kwa kupita juu ya mawe," anasema mwanakijiji huyo.

Mkurugenzi wa asasi inayoitwa Kalangali Agriculture and Environmental Advocacy, inayojihusisha na Hifadhi ya Bonde Dogo la Mto Lupa, Lucas Malangalila, anasema kuwa uchimbaji dhahabu kwenye mito hiyo unaofanywa na Kampuni hiyo ya Wachina ni ukiukaji wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004.

"Sheria ya mwaka 2004 inabainisha kwamba hakuna shughuli zozote za kibinadamu zitakazoweza kufanyika ndani ya mita 60 kutoka kwenye kingo ya mto kwa kila upande, sasa iweje mtu aingie ndani ya maji na mitambo inayomwaga oil na dizeli wakati mito hiyo ndiyo chanzo pekee cha maji kwa wananchi waishio kwenye vijiji vilivyo kando ya mito hiyo?" anauliza Malangalila na kuongeza:

"Sheria hiyo vile vile inazuia uharibifu wa uoto wa asili kwenye kingo za mito, sasa hawa Wachina wanang'oa miti, miti mikubwa kabisa wanakata kwa mashine kabisa. Sijui wanaipeleka wapi na hawana kibali cha afisa maliasili. Sheria hiyo inakataza kuhamisha au kufunga mto kutoka kwenye mkondo wake wa asili, lakini hawa Wachina wameblock, maji yametuama na machache kutoka katika maji yale yaliyopita kwenye mitambo yao yanapenya yakitafuta njia nyingine, tofauti na ile ya asili na ndio hayo maji yanayoenda kutumiwa na wananchi."

Hofu ya Malangalila kuhusu mradi huo haina tofauti na ya mkazi wa kijiji cha Lupa Market, Nicolaus Amanyisye ambaye anasema: "Maji tunayotumia ni kutoka Mto Lupa, huwa tunafukua pembeni kwa sababu hivi sasa yanayokuja huku kidogo sana, lakini siyo masafi wala salama, yanachafuliwa na Wachina wanaochimba dhahabu, wanachimba katikati ya mto."

Baada ya kutembelea eneo la machimbo na mito yenyewe, nilibaini uhalali wa kilio cha wananchi hao. Maji ya mito hiyo sio safi tena, na wala hayawezi kuwa salama, yanachafuliwa na shughuli za uchimbaji dhahabu unaofanywa na Wachina hao. Mbali ya ufukuaji na ubomoaji miamba iliyo chini ya mito hiyo, mitambo yao inatumia mafuta yanayoonekana yakielea juu ya maji.

Tayari wananchi wameanza kulalamika kuhusu magonjwa ya matumbo lakini wakati huo huo, kwa wale wa Kijiji cha Lupa Market wakikosa huduma ya afya, wanalazimika kutembea Kilometa saba hadi Kijiji cha jirani cha Ifumbo ambako ndiko iliko zahanati.

Hata hivyo, sio kwamba Wachina hao wamevamia, la hasha. Wana hati za kisheria zinazowapa ruhusa ya kufanya shughuli hiyo. Kampuni hiyo ya EPOCH Mining (T) Ltd inaendesha shughuli hizo kwa kutumia leseni Na. ML 207/2005 iliyotolewa Machi 10, 2005 kwa Kampuni ya KAMAKA CO. LIMITED ya jijini Dar es Salaam na waziri wa wakati huo wa Wizara ya Madini na Nishati, Daniel Yona.

Leseni hiyo ilihamishiwa kwa Kampuni hiyo ya EPOCH Mining (T) Ltd Desemba 22, 2009 kwa barua iliyotiwa saini na Kamishna wa Madini, Dk. Dalaly P. Kafumu baada ya wamiliki hao wapya wa leseni hiyo kulipia malipo ya uhamisho ya Dola za Kimarekani 200 (nyaraka zote tunazo).

Meneja wa mradi huo wa Chunya kutoka kampuni hiyo, Danny Zhu, aliambia Raia Mwema kwamba walianza kazi ya uchimbaji dhahabu kwenye mito hiyo Aprili mwaka huu baada ya kukamilisha upelekaji mitambo na vifaa vingine eneo la mradi.

Zhu anakanusha kuharibu mazingira ya mito hiyo kwa maelezo kuwa wanachokifanya ni kukusanya mchanga na hawatumii madini ya zebaki.
Akizungumzia suala la tathmini ya athari ya uharibifu wa mazingira kuhusu mradi huo (Environmental Impact Assessment - EIA), meneja huyo alisema: "Kwanza kibali tumepewa na mamlaka husika Dar es Salaam. Tunayo leseni iliyotolewa mwaka 2009. Hiyo EIA siijui mimi. Ni nini? Labda bosi wetu Dar es Salaam anaijua."

Mwaka anaouzungumzia meneja huyo kwamba leseni hiyo ilitolewa ni ule unaoonyeshwa kwenye bartua ya uhamisho wa leseni hiyo kutoka kwa KAMAKA Company LTD na kwenda EPOCH Mining (T) Limited.

Gazeti la Raia Mwema lilibaini kuwepo kwa hati ya idhinisho ya EIA ambayo, hata hivyo, ni ile iliyotayarishwa na KAMAKA CO. LIMITED ambao ni wamiliki wa awali wa leseni hiyo kabla haijahamishiwa kwa kampuni hiyo ya Kichina, na nyaraka hiyo haionyeshi iwapo ilipitiwa upya na Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC).

Hata hivyo, taarifa za kuanzia mwaka 2005 hadi 2008 zilizopo kwenye ofisi za Kanda ya Nyanda za Juu Kusini hazionyeshi kampuni hiyo kwamba iliwahi kupatiwa cheti na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) kama sheria inavyoelekeza.
Mratibu wa NEMC Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Joachim Kessy, aliliambia Raia Mwema kuwa, wataalamu wa kufanya EIA husajiliwa na baraza hilo, na kwamba mwekezaji huwaomba hapo, na kisha huenda kwenye eneo la mradi kwa gharama za mwekezaji mwenyewe, na kwamba hiyo ni kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 Cap 191.
"Baada ya kufanyika kwa EIA, inatakiwa ku- consult wadau wengine; kama vile wanakijiji. Hawa ni lazima washirikishwe kwenye maamuzi, na baada ya kukamilisha hatua hizo ndipo waziri anatoa cheti kwa mwekezaji," alisema mratibu huyo. Alipoelezwa na mwandishi kuwa wanavijiji wa Ifumbo na Lupa Market kunakoendeshwa uchimbaji huo wanalalamika, Kessy alijibu:
"Kama wanavijiji wanalalamika, ina maana hawajafikia muafaka. Kabla ya kupewa cheti huwa inafanyika public hearing ambayo inawajumuisha wananchi, NEMC na mwekezaji. EIS ni sehemu tu ya mchakato wa kupata EIA. Sheria hairuhusu mwekezaji kuanza kazi kabla ya kupata EIA."
Taarifa hizo zilizopo kwenye ofisi ya Kanda ya NEMC kuhusu EIA zinaonyesha kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2005 hadi 2008 vilitolewa vyeti kwa makampuni manane tu kwa mkoa wa Mbeya. Mchanganuo unaonyesha cheti kimoja kilitolewa mwaka 2005, vyeti sita mwaka 2008 na cheti kimoja tena mwaka 2008. Katika makampuni hayo yaliyopatiwa vyeti, si KAMAKA wala EPOCH iliyomo kwenye orodha hiyo.
Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 inabainisha kwamba baada ya Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya mapitio ya Taarifa ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) litawasilisha mapendekezo yake kwa waziri mwenye dhamana kwa uamuzi wa ama kuikubali au kuikataa ambapo anatakiwa kutoa uamuzi huo ndani ya siku sitini.
Kutokana na vifungu namba 91 na 92 vya sheria hiyo, ni wazi kwamba kampuni hiyo ilitakiwa kuwa na cheti cha EIA kilichotolewa na waziri mwenye dhamana ya mazingira; jambo ambalo viongozi wote waliohojiwa, wawe wa kampuni hiyo au wa mamlaka za serikali, hawathibitishi kwamba lilifanyika.
Mkanganyiko wa wawekezaji hao wa Kichina unajibainisha zaidi kutokana na taarifa zinazowatilia shaka kutoka ofisi za madini wilaya ya Chunya na Kanda kama alivyobainisha Kamishina Msaidizi wa Madini, Kanda ya Kusini Magharibi, John Shija aliposema:

"Taarifa tulizonazo wana leseni ya uchimbaji iliyotolewa mwaka 2005. Lini wameingia kwenye eneo la uchimbaji (site) hilo sijapata taarifa zao, lakini nimesikia juzi kutoka kwa wenzetu ofisi ya Chunya kwamba wanachimba na wanaharibu mazingira".

"Jumamosi ya wiki hii nitaenda site kuona hali halisi kujiridhisha, na iwapo hawana cheti toka NEMC nitamshauri Kamishina wa Madini asitishe leseni yao," alisema Shija.

Mbali ya uharibifu huo wa mazingira, kampuni hiyo ya Kichina inakiuka masharti ya leseni kwani haina mfanyakazi hata mmoja Mtanzania kwenye mradi huo. Waliopo wote ni Wachina; wengi wakiwa hawajui kabisa lugha ya Kiswahili wala Kiingereza. Hata salamu tu mnawasiliana kwa ishara.
Hali hiyo ya kutoajiri Watanzania ni kinyume na masharti ya leseni; hasa kifungu namba saba kinachotaka mwekezaji kuajiri na kufundisha Watanzania wenye viwango vya elimu sahihi.


Kuhusu ajira, Zhu anasema: "Hakuna mfanyakazi Mtanzania. Wale ni mafundi, na ile mitambo inahitaji uangalizi wa hali ya juu; hivyo hakuna Mtanzania tuliyemwajiri."

Wakati Wachina hao wakijichotea dhahabu kutoka kwenye vijiji hivyo, Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, kwa upande wake, haipati chochote kutoka kwenye mradi huo kwa maana ya kodi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Maurice Sepanjo aliambia Raia Mwema kuwa hata wao wameshitushwa na kasi ya uchimbaji dhahabu kutoka kwenye mito hiyo wakati awali walidai kuwa wanafanya utafiti (exploration).
"Nimefika huko, wanadai kufanya exploration, lakini ukiangalia ile mitambo na shughuli wanazofanya pale sio exploration bali ni uchimbaji kabisa. Halmashauri hailipwi kodi ya aina yoyote, labda huko wizarani wao ndio wenye kufahamu. Sidhani hata TRA wanakusanya chochote. Wanaenda hadi mita 30 chini, nimetaarifu ofisi ya madini hapa Chunya na Kanda. Wale wa Kanda wameahidi kufuatilia",
alisema mkurugenzi huyo.












Hiyo ndiyo Tanzania - Shamba la Bibi. Wanavuna na kutuachia mashimo na uharibifu mwingine mkubwa tu wa mazingira; huku wenyewe tukiambulia patupu. Lakini swali linalosumbua wananchi hivi sasa ni: "NANI ANAWABEBA WAWEKEZAJI HAO TOKA CHINA?"
hs3.gif
 
Ndugu yangu Bubu Ataka,
Tatizo kubwa ni Umaskini wa Akili. Umaskini wa akili ni mbaya kuliko aina nyingine yoyote ya UMASKINI.
Hapo utakuta wale tuliowapa jukumu la kusimamia sheria, kanuni na taratibu wamenunuliwa kwa kiasi kidogo sana cha pesa, say US$ 10,000 tu, basi akapofushwa macho na kuacha Wachina waharibu mazingira watakavyo.
Lakini haya mambo yataisha lini? Mbona saa ya ukombozi toka lindi la umaskini wa akili liko mbali?

"HAMNA UMASKINI MBAYA KAMA UMASKINI WA AKILI''. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
 
Waacheni wavune shamba la bibi. Si ndio baadaye mnakuja kuwasifu eti 'China ni taifa linaloendelea kwa kasi zaidi' bila kudhani wanaendelea at our own expense. Wajinga ndio waliwao.
 
Update on this aritcle posted few minutes ago.
 
Back
Top Bottom