Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
WABUNGE wa upinzani na wa CCM, wamekosoa uamuzi uliofanywa na uongozi wa Bunge wa kurejesha Sh. bilioni sita serikalini ilhali baadhi ya shughuli za Bunge zimekwama kutokana na uhaba wa fedha.
Aidha, baadhi ya wabunge hao wamedai Rais Dk. John Magufuli, amekuwa akiingilia majukumu ya mihimili mingine, likiwamo Bunge.
Aprili 11, mwaka huu, uongozi wa Bunge ulimkabidhi Rais Magufuli hundi ya Sh. bilioni sita, ambazo ulieleza kuwa uliziokoa kutokana na kubana matumizi.
Rais Magufuli aliupongeza uongozi huo na kuagiza fedha hizo zitumike kutengeneza madawati, huku akizitaka ofisi na taasisi zingine za serikali kuiga mfano huo.
Katika kikao cha wabunge na uongozi wa Bunge hilo kilichofanyika mjini hapa juzi, kuanzia saa 11 jioni hadi saa 2:15 usiku, wabunge waliukosoa uongozi wa Bunge kwa uamuzi huo kwa vile "shughuli nyingi za Bunge zimekwama kutokana na uhaba wa fedha."
Katika mkutano huo, waandishi wa habari walizuiwa kushiriki kwa maelezo kuwa ulikuwa maalum kwa ajili ya maelekezo kwa wabunge.
Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA), aliiambia Nipashe kwenye viunga vya Bunge jana kuwa wameshangazwa na uongozi wa Bunge kurejesha fedha serikalini wakati kuna mambo mengi ya msingi ya Bunge hayajafanyika, kutokana na ukosefu wa fedha.
"Kamati zingine zimezuiwa kusafiri wa maelezo kwamba hakuna fedha. Kamati ya Mambo ya Nje imezuiwa kusafiri kwa madai kuwa hakuna hela, walitarajia kwenda kuangalia nyumba za ubalozi huko nje, lakini wanaambiwa hakuna fedha, wakati pesa nyingi imerejeshwa serikalini," alisema.
Kadhalika, Mchungaji Msigwa alisema wabunge pia walihoji sababu za kuzuiwa kuonyeshwa moja kwa moja kwa shughuli za Bunge, jambo ambalo alidai limelenga kuminya uhuru wa vyombo vya habari nchini na "kuficha uovu ya serikali."
"Shughuli za Bunge hazionyeshwi moja kwa moja na vyombo vya habari, lakini anachokifanya Rais kinaonekana. Wabunge tulihoji uongozi wa Bunge kuhusu uamuzi huu," alisema.
Msigwa aliongeza kuwa katika mkutano huo, Mbunge wa Mbeya Mjini (CHADEMA), Joseph Mbilinyi 'Sugu', alikwenda mbali zaidi akidai Rais Magufuli amekuwa akiingilia madaraka ya mihimili mingine.
Sugu alikumbushia 'kilio cha wapinzani' kuhusu uteuzi wa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Akson.
Rais Magufuli alimteua Dk.Tulia kuwa mbunge wa kwanza ikiwa ni siku mbili baada ya kuteuliwa na Kamati Kuu ya CCM kuingia kwenye ‘tatu bora’ ya kuwania Uspika, jambo ambalo Sugu alidai linatoa taswira Rais alitumia mamlaka yake kumweka kuwa Naibu Spika.
Mbunge wa Igunga (CCM), Dk. Dalali Kafumu, alisema fedha za Bunge kutumika kununua madawati si jambo baya, lakini wabunge walipaswa kushirikishwa kabla ya kufanyika kwa uamuzi wa kurejesha fedha serikalini.
"Uamuzi wa kutengeneza madawati na kila Mbunge kupewa 600 apeleke jimboni kwake ni mzuri, tatizo wabunge hawakushirikishwa," Dk. Kafumu alisema.
Aliongeza kuwa: “Pia wabunge wa Muungano walihoji jana (juzi) kuhusu kutohusishwa kwao katika mpango huo wakati fedha zilizorejeshwa serikalini ni za Bunge la Muungano, wao hawapewi madawati maana Zanzibar ina Wizara ya Elimu inayojitegemea. Uongozi wa Bunge uliahidi utaangalia namna ya kushughulikia malalamiko yao."
Mbunge mwingine wa CCM ambaye hakuwa tayari jina lake litajwe gazetini, aliiambia Nipashe kuwa haungi mkono uamuzi wa kurejeshwa fedha serikalini kutokana na kusafiri kwa shida akiwa na moja ya kamati za Bunge hivi karibuni.
Chanzo: Nipashe