Wabunge wa CCM mnaishi nchi gani?

Wabunge wa CCM mnaishi nchi gani?

sulphadoxine

JF-Expert Member
Joined
Nov 1, 2010
Posts
2,257
Reaction score
649
Vipi hamjui ni lazima serikali iwajibike kwa wananchi na si hiari?



WABUNGE wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Kiti cha Spika, wasitulazimishe Watanzania kuamini kwamba tunaishi peponi, mahala ambapo hakuna kero yoyote kwa sababu Mungu na Malaika zake hawatendi makosa, bali wakati wote ni waaminifu na wakweli milele yote!


Ni ukweli usiopingika kwamba hakuna mwanadamu awezaye kufanya mema tu hapa chini ya jua na asitende pia ovu lolote. Kama yupo mtu wa namna hiyo basi ruksa kwake kujiita Mungu au malaika, ndiyo maana siyo ajabu watu kukosoa na kushauri njia mbadala kila inapotokea kujikwaa juu ya jambo fulani na vile vile kupongezana kwa kila lililo jema.

Hata hao wanaoitwa wapinzani, itakapotokea wakati mmoja na wao kushika madaraka inawezekana kabisa (ikiwa na wao watakosa busara na hekima) wakawa pia hawapendi kusikia kauli yoyote ya kukosolewa zaidi ya zile za kusifu na kupongeza tu, labda tuombe tu kuwepo na kiti huru cha spika ambacho kitakuwa na usawaziko kwa maslahi ya taifa na wala siyo ya chama fulani.

Kwa mtu ama kiongozi mwenye akili timamu, ikiwa anakubali kupongezwa kwa mema anayotenda lazima pia awe radhi kukosolewa kwa maovu yake, ili kasoro hizo zimsaidie kujirekebisha pale ambapo mambo yanaonekana kwenda kombo katika utawala ama shughuli zake za kila siku, kwani inaelezwa kwamba serikali nyingi bora duniani ni zile zinazokubali kukosolewa na kupokea ushauri mbadala (baada ya kuufanyia utafiti wa kina) bila kujali umetoka kambi pinzani.

Lakini hilo linaonekana kuwa jambo geni kabisa kwa wabunge wa CCM, Kiti cha Spika na baadhi ya viongozi wa Serikali, kwani wao wanaamini kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), inatawaliwa na Kiongozi mwenye sifa za Kimungu, wabunge na mawaziri wake ni kama Malaika, Kiti cha Spika kinakaliwa na Malaika Gabriel (Jibril), hivyo Watanzania wanapaswa kuamini kuwa wanaishi peponi, mahala ambapo hakuna kero bali ni kuimba na kusifu tu milele!

Nasema hivyo kufuatia matukio yasiyo ya kawaida ambayo yamekuwa yakijitokeza siku za hivi karibuni ndani ya chombo muhimu na moja kati ya mihimili mikuu ya nchi, namaanisha Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ambako wananchi wanataraji kusikia kutoka humo majibu ya utatuzi wa kero zao, utungaji wa sheria, ikiwa ni pamoja na kuishauri na kuisimamia serikali ili ifanye yale ambayo Watanzania wanataka kufanyiwa.

Bila kumung'unya maneno, siyo siri sasa upendeleo ni dhahiri kabisa ndani ya Bunge letu kiasi cha mtoto mdogo kubaini hilo, huku kiti cha spika kikionekana kuwa ndiyo chanzo cha vurugu Bungeni.

Sasa hivi ukifuatilia Bunge linatia kinyaa kabisa na kuonekana kama kikao cha Halmashauri kuu ya CCM, ambako wabunge wa upinzani ni kama waalikwa tu ambao ama hawapaswi kuzungumza kabisa au kuchangia lolote linalohusu kukosoa ama kushauri, ikiwa tu hawataki kuisifia serikali hata pasipostahili!

Kama vile ambavyo upo utamaduni wa kuwasadikisha wananchi kwa njia ya kusomewa makaratasi kwamba uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi ingawa hauyagusi moja kwa moja maisha ya watu, ndivyo vivyo hivyo wabunge wa CCM wanaonekana kuwa na kampeni kali za kuwasadikisha Watanzania kuamini kuwa ingawa wapo duniani lakini watambue wanaishi peponi ambako hakuna kero hata moja!

Wanasahau kuwa matendo ndiyo hukidhi haja maridhawa zaidi kuliko maneno, mfano; mimi pia ni mzazi, wakati fulani niliwalaumu wanangu sana na kuwaona kama hawana shukurani, lakini kumbe sikufikiri vyema. Nilisahau kuwa mtu hasifiwi kwa kutimiza wajibu bali kwa jambo la ziada ambalo siyo wajibu. Nilifikiri nitasifiwa na familia kwa kuwanunulia chakula na mavazi, lakini nilichoambulia ni “pole kwa kazi na majukumu” badala ya “hongera.”

Kibaya zaidi nilikosolewa na kulaumiwa sana kila nilipochelewesha hata kitoweo nyumbani, sembuse kurudi mikono mitupu!

Kama ningekuwa na tabia kama ya Wabunge wa CCM, basi nyumbani pangechimbika, ningelazimisha familia inisifie hata kwa jambo lililo wajibu wangu. Tunapaswa kutambua kwamba wajibu siyo hiyari wala zawadi kwamba mtu asipotenda hapaswi kulaumiwa au akitenda eti atarajie sifa na pongezi. No! haipaswi kuwa hivyo, we tenda wema wende zako, usingoje shukurani, hiyo ndiyo tabia ya “wajibu”, inafanana na “Lazima”na haina tofauti sana na “sheria.”

Ndio, wananchi tukishakupigia kura, ukaingia madarakani (hata kama ni kwa kuiba kura) katiba ya nchi inakulazimisha kutumikia. Hiyo ni kazi uliotafuta na hivyo usitegemee kusifiwa.

Kwani nani kawaloga wabunge wa CCM kiasi cha kudhani kuwa Chama na Serikali havipaswi kukosolewa hata chembe kwa namna yoyote ile? Mimi nilifikiri kasumba hiyo ni pale tu wapinzani wanapokosoa au kushauri, kumbe ni haramu kufanya hivyo pia kwa wabunge wanaotokana na CCM!

Eh, hii ni hatari sana kwa maendeleo ya taifa, pole sana mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola na wenzako wachache kama Deo Fili Kunjombe kwa kuthubutu kuitikisa misingi ya mbingu, oh sorry ya chama, kinyume na maandiko ‘matukutu’.

Kama ni suala la wapinzani kuisifia serikali ya Chama cha Mapinduzi, hilo mbona lina ushahidi mkubwa sana ingawa siyo jambo la kujivunia kwa sababu wananchi ndiyo wanapaswa kupaza sauti zao za kusifia wajibu (kama kuna ulazima wa hilo) mbele ya viongozi wa Serikali badala ya kuwalazimisha wabunge wa upinzani kufanya hivyo.

Binafsi nimewahi kuwashuhudia kwenye Luninga wabunge wa upinzani wakishiriki kazi za ufunguzi wa barabara mpya za lami zinazounganisha mikoa, ambako baadhi ya wabunge hasa wa Chadema kama Freeman Mbowe, Zitto Kabwe, Joseph Serasini na wengineo kwa nyakati tofauti walisikika wakiipongeza Serikali kwa ujenzi wa barabara hizo, licha ya kuvumilia hotuba za vijembe, kejeli na dhihaka toka kwa waziri wa Ujenzi, John Magufuri. Ni sifa zipi nyingine za ziada wanazozitaka wabunge wa CCM?

Ni kweli kabisa Serikali ya CCM imefanikiwa kwa kiasi fulani kuboresha miundombinu hasa ya barabara zinazounganisha mikoa, hata wapinzani wanaliona hilo ingawa hawalazimiki kusifia kwa sababu ni wajibu wa serikali na wala siyo hiyari.

Lakini maendeleo ya nchi siyo barabara tu, kuna huduma za maji safi na salama, elimu na matibabu bora kwa wote, umeme n.k, ikiwa ni pamoja na kudhibiti wizi, ufisadi na rushwa ili rasilimali za nchi ziwanufaishe Watanzania wote. Kwa mfano, utasifia nini katika elimu wakati matokeo ya mwaka jana yalikuwa mabaya kuliko malezo yoyuote nitakayotoa. Utasifia nini wakati tumekuwa na matokeo ambayo tunapeleka sekondari wanafunzi ambao hawajui kusoma na kuandika?

Kwa ajili ya kero hizo na nyingine, wabunge wa upinzani hawapaswi kufumbwa midomo wasizipaze sauti zao kuwatetea wananchi ndani na nje ya Bunge, woga na unafiki wa kuikosoa, kuishauri na kuisimamia serikali ndiyo unawafanya baadhi ya wabunge kuyapa mgongo matatizo chungu mzima yanayowakabili wapiga kura wao majimboni, na kubaki wakipoteza muda kukitetea chama na kuporomosha matusi!

Mara… ooh siongei na mbwa, naongea na mwenye mbwa, mara ooh… wanaume fanyeni bidii kuongeza wake wawili wawili ili kuwasaidia wanawake wasio na waume, mara…ooh Serikali ifunguwe kituo cha kuwafundisha wanaume jinsi ya kutongoza, mara eti ooh… bangi ihalalishwe ili kuinua uchumi wa nchi n.k, Jamani! Yaani ujinga na upuuzi mtupu! Nani kawatuma hayo? Acheni hizo bwana!
 
Back
Top Bottom