Waathirika mafuriko Dar njiapanda | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Waathirika mafuriko Dar njiapanda

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, Dec 31, 2011.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Dec 31, 2011
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,611
  Trophy Points: 280
  Ni kwa kukosa maandalizi maeneo walikotengewa
  [​IMG] Viongozi wa maeneo hayo waikana serikali
  [​IMG] Wananchi nao waionya inachochea mgogoro  [​IMG]

  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, akipokea msaada wa vyakula kutoka kwa Brigedia Jenerali Cyril Ivor Mhaiki, wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Msaada huo ni kwa ajili ya waathirika wa mafuriko jijini Dar es Salaam.(PICHA: OMAR FUNGO)


  Wakati walioathirika na mafuriko wakipinga kuondolewa mabondeni, viongozi wa serikali wa eneo la Mabwepande, wilayani Kinondoni,

  mkoani Dar es Salaam walikotengewa, wamesema hadi sasa hakuna maandalizi yoyote yaliyokwisha kufanywa kwa ajili ya kuwahamishia watu hao baada ya kuwatoa kwenye makambi wanakohifadhiwa hivi sasa.
  Miongoni mwa maandalizi, ambayo viongozi hao wanasema bado hayajafanyika, ni pamoja na kuwashirikisha viongozi na wananchi wa eneo hilo.

  Wanasema hali hiyo mbali ya kutishia kuibua migogoro, pia inaweza kuhatarisha usalama wa afya za wakazi wa eneo hilo.
  Kauli hiyo ilitolewa na viongozi hao ikiwa ni siku mbili tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, kuwataka waathirika hao waliohifadhiwa katika kambi za shule za msingi na sekondari kuondoka mara moja ifikapo Januari 5, mwakani.

  Amri hiyo ilitolewa na serikali kwa lengo la kuwapisha wanafunzi wa shule hizo, ambazo zinatarajiwa kufunguliwa Januari 9, mwakani.
  Akitoa amri hiyo, Sadiki alisema serikali haina mpango wa kuwapa fedha za kwenda kujengea nyumba kwenye viwanja ilivyowapa katika maeneo hayo kwa kuwa sio wajibu wake.

  DIWANI, MWENYEKITI: HATUJASHIRIKISHWA

  Diwani wa Kata ya Mabwepande (CCM), Clement Boko, alisema anashangazwa na serikali kuamua kutangaza kuwagawia waathirika hao viwanja bila kushirikisha viongozi na wananchi wa eneo hilo.

  Boko alisema anavyofahamu siku zote ni kuwa eneo ambalo serikali imelitangaza kuwatengea waathirika hao, lilipimwa kwa ajili ya shughuli za Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).

  Alisema hata hivyo, hadi sasa IFM bado haijamaliza kulipa fidia na wameamua kuchukua eno lingine huko Msata Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.

  Mbali na hilo, alisema pia eneo la Kwa Kitomari, ambalo linatajwa kuwa kambi ya muda, tayari limevamiwa na zaidi ya wakazi 2,000.
  “Katika hili mkuu wa wilaya atanisamehe. Niko upande wa wananchi. Mchakato mzima haujaletwa. Hivyo, tunataka tuhakikishiwe kwanza ndio tutatoa ushirikiano,” alisema Boko.

  Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mabwepande, Abdallah Kuja, aliungana na diwani huyo kulaumu mpango wa kutaka kuwahamishia waathirika hao katika eneo hilo kutowashirikisha.
  Alisema alipewa taarifa za ujio wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, kufanya mkutano wa hadhara, ikiwa ni hatua za awali za kuelekea kwenye zoezi hilo.

  Alisema katika taarifa hiyo, Rugimbana aliwatangazia wananchi wote wenye maeneo kufika kwa ajili ya kuanza mchakato wa zoezi hilo ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza baadae.
  “Kwa kweli hatujapata taarifa rasmi za waathirika hao kuletwa kuja kuishi huku. Hivyo, hatuna majibu rasmi,” alisema Kuja.

  WAKAZI WATISHIA

  Baadhi ya wakazi waliovamia eneo la Kwa Kitomari, wametishia kuanzisha mgogoro upya.
  Walisema wataanzisha mgogoro huo iwapo serikali haitajali mahitaji yao, ikiwa ni pamoja na kuwatambuwa kuwa nao pia ni waathirika. Walieleza wasiwasi kuhusu zoezi hilo wakisema lina sura ya kuibua mgogoro.

  Hivi karibuni Sadiki alitangaza uamuzi wa kuwaondoa kwa nguvu wakazi wanaoishi mabondeni iwapo watagoma kuondoka kwa hiari yao.
  Pia ilitangaza kuwaondoa kwenye makambi ya waathirika kabla ya kufunguliwa kwa shule Janjuari 9, mwakani.
  Mara zote serikali imekuwa ikieleza kukamilisha upatikanaji wa viwanja katika eneo la Mabwepande, ambako ilisema imetenga Sh. bilioni 3 kwa ajili ya kuwalipa fidia wamiliki wa mashamba na upimaji wa ardhi katika eneo hilo.

  Hata hivyo, agizo la serikali la kuwataka wamiliki wa nyumba walioathiriwa na mafuriko kuondoka mabondeni, limekuwa likipata upinzani mkali, baada ya wakazi hao kushikilia msimamo wa kutoondoka maeneo hayo, wakipinga kupewa viwanja vitupu, huku wakiwa hawana uwezo wa kugharimia ujenzi wa nyumba kwenye makazi mapya waliyotengewa na serikali.

  Wakati wamiliki hao wakipinga suala hilo, waathirika wa mafuriko hayo waliokuwa wapangaji katika nyumba hizo pia wamesema wako tayari kuondoka kambini wakati wowote, lakini watarejea katika nyumba walizokuwa wakiishi mabondeni, kwa vile hawana uwezo wa kuishi kwenye makazi mapya.

  Baadhi ya wamiliki wamekuwa wakisema serikali inapaswa kutumia busara katika kuwahamisha kwenye eneo hasa la Jangwani kwa kuwa mpango wake huo unaweza kukwama iwapo itatumia nguvu.

  Walisema iwapo serikali haitasikiliza madai yao ya kutaka kuwezeshwa gharama za ujenzi wa nyumba kwenye makazi mapya wanakotakiwa wahamie, watafufua amri ya mahakama ya kuzuia kuvunjwa nyumba zao.

  Walidai maombi ya zuio hilo yaliwasilishwa na wamiliki wa nyumba 274 wa eneo la Jangwani mwaka 2008 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

  Walida maombi hayo yalikubaliwa na mahakama hiyo na kwamba, hadi sasa zuio hilo la mahakama bado halijatenguliwa.
  Nao wapangaji katika eneo hilo, walisema wako tayari kuondoka makambini kabla ya tarehe iliyotangazwa na serikali, lakini watarejea kwenye nyumba za mabondeni walizokuwa wakiishi kabla ya kukumbwa na mafuriko.

  Walisema wanashindwa kuwabana wamiliki wa nyumba kuwarejeshea sehemu ya fedha za malipo ya kodi zao ili waweze kupanga kwenye nyumba nyingine, kwa kuwa nao pia wameathirika.

  Walisema ambacho serikali na baadhi ya watu hawakijui ni kwamba, katika wapangaji waliokuwa wakiishi mabondeni, wapo wengi waliokodi nyumba nzima.

  Hivyo, wakasema busara iliyotumiwa na serikali kuwanunulia wamiliki viwanja vya kujenga nyumba mpya, ingetumiwa pia kwa wapangaji kwa kuwapa japo Sh. 100,000 kila mmoja, ili kuwawezesha kupata makazi ya kuanzia maisha mapya.
  Waathirika wengine waliozungumza na NIPASHE jana waliitaka serikali kuwahakikishia makazi mengine hata kama itakuwa kwenye mahema.

  JWTZ YATOA MSAADA WA CHAKULA KWA WAATHIRIKA

  Wakati hayo yakijiri, Brigedi Kamanda, Kanda ya Mashariki wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Brigedia Jenerali Cyril Ivor Mhaiki, jana alimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, msaada wa chakula chenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 24.5 kwa ajili ya waathirika.

  Brigedia Jenerali Mhaiki alikabidhi msaada huo kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange, maafisa wanadhimu kutoka makao makuu ya jeshi, askari na watumishi wa umma wanaofanya kazi jeshini.

  Msaada huo unahusisha mchele magunia 75 yenye jumla ya kilo 75,000; maharage magunia 16 (kilo 1600); sukari magunia 16 (kilo 1,600) na majani ya chai kilo 224.

  Akikabidhi msaada huo, Brigedia Jenerali Mhaiki alisema JWTZ imeshtushwana mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha kwa siku mbili mfululizo jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu 40 na mali zenye thamani ya mamilioni ya shilingi kuharibika.
  Sadiki akipokea msaada huo, aliishukuru JWTZ akisema tangu kutokea maafa, jeshi hilo halikuanza kutoa msaada huo jana, bali hadi sasa linaendelea kusaidia kazi nyingine zinazohusu maafa hayo.

  RC AIOMBA JWTZ MAHEMA

  Hata hivyo, Sadiki aliiomba JWTZ msaada wa mahema kwa ajili ya kutumiwa waathirika mara serikali itakapokamilisha zoezi la kuwahamishia eneo la Mabwepande.

  CUF WATOA MSAADA WA CHAKULA

  Chama cha Wananchi (CUF) jana kilitoa msaada wa vyakula; ukiwamo mchele, maharage, unga, sukari, sabuni, na mafuta kwa waathirika wa mafuriko katika kambi mbalimbali jijini Dar es Salaam.

  Vyakula hivyo vilitolewa na CUF katika Shule ya Sekondari Green Acres, Shule ya Msingi Gilman Rutihinda, Shule ya Msingi Mnazi Mmoja, Shule ya Msingi Vingunguti kwa Kombo, Shule ya Sekondari Kibasila na Shule ya Msingi Kiburugwa.

  Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro, aliwapa pole waathirika hao na kuitaka serikali kufanya jitihada za haraka za kuwatafutia sehemu ya kuishi na sio kuwabagua kwa kusema kwamba wengine walikuwa ni wapangaji.

  Mtatiro alisema watu wote waliokutwa na maafa, wanastahili kutafutiwa maeneo ya kuishi kutokana na kuwa wote wameathirika, hivyo serikali iache kuwagawa kwa kusema kuwa wengine ni wapangaji hivyo hawatapatiwa maeneo.

  “Lazima serikali ijue inawapeleka wapi hawa waathirika wa mafuriko. Na ifikirie kwa makini suala hili kwa kuwa huu sio muda wa kukwepa majukumu na kuanza kuwagawa waathirika kwa makundi kuwa wengine ni wapangaji na wengine ni wenye nyumba. Hakuna kitu kama hicho. Wote wanastahili msaada wa serikali,” alisema Mtatiro.

  NMB YATOA SH. MILIONI 10

  Nayo Benki ya NMB ilikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sadiki, msaada wa hundi yenye thamani ya Sh. milioni 10 kwa ajili ya kuwasaidia waathirika.
  CHANZO: NIPASHE
   
Loading...