Vyama viwili vya siasa vyafutwa

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,314
33,108
Vyama viwili vya siasa, vimefutwa katika daftari la Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya usajili.

Vyama hivyo ni People's Democratic Movement (PDM) na Democratic National Congress (DNC).

Wakati vyama hivyo vikifutwa, pande mbili za viongozi wa Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD) zenye mgogoro, wanakutana na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, kujadili kuhusu hatima ya chama hicho leo.

Tendwa alisema jana kuwa PDM na DNC, vilifutwa baada ya zoezi la uhakiki wa wanachama wake kubaini kwamba, havijatimiza masharti ya usajili katika muda unaotakiwa na sheria.

Hadi sasa jumla ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, ni 18, kikiwamo kipya cha Alliance for Tanzania Farmers (AFP) kilichopatiwa usajili huo Novemba 3, mwaka jana.

Vyama vingine vyenye usajili wa kudumu, ni CCM, CUF, Chadema, UMD, NCCR-Mageuzi, NLD, UPDP, NRA, Tadea, TLP, UDP, Demokrasia Makini, Chausta, DP, APPT-Maendeleo, Jahazi Asilia na Sau.

Wakati huo huo, pande mbili za viongozi wa UMD zenye mgogoro, zinakutana na Tendwa ofisini kwake ili kujadili kuhusu hatima ya chama hicho leo.

Pande hizo ni pamoja na ile ya Mwenyekiti wa UMD, Salum Ali na Katibu Mkuu wake aliyetangazwa kutimuliwa, Abdi Mshangama.

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliuandikia uongozi wa UMD barua Mei 12, na kuzipa pande hizo za mgogoro muda wa wiki mbili, kuanzia Mei 14, mwaka huu, zishirikiane kuandaa mkutano wa uchaguzi, vinginevyo chama hakitaruhusiwa kushiriki Uchaguzi Mkuu na kitafutiwa usajili wa kudumu.

"Msajili ameelekeza kwamba hahitaji upande wowote umfukuze yeyote katika kipindi hiki, bali pande zote mbili zishirikiane kuandaa mkutano wenu wa uchaguzi. Hivyo anawapa wiki mbili tu 14-28/05/2010 kwa utekelezaji wa maelekezo haya baada ya hapo kama mtakuwa hamjatekeleza basi chama chenu hakitaruhusiwa kushiriki uchaguzi mkuu na baada ya hapo atakifutia usajili wake wa kudumu," ilieleza sehemu ya barua iliyosainiwa na Muhidin Mapeyo kwa niaba ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom