Vituko Pemba: Furaha yenu ni mauti kwetu

Dr. Chapa Kiuno

JF-Expert Member
Sep 11, 2009
443
18






rC.jpg

USIPOZIBA ufa utajenga ukuta; ngoja ngoja yaumiza matumbo; mdharau mwiba mguu huota tende, ni baadhi tu ya methali zinazoeleza busara walizotuachia wahenga katika kukabili mazingira tunamoishi.
Tumezikumbuka methali hizi kutokana na vituko vinavyoendelea kila uchao katika moja ya maeneo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pemba, ambako yapata miezi karibu sita sasa, watu hawafanyi kazi yoyote ya kuzalisha, badala yake wanakula, kulala na kuzungumza siasa zisizojenga.
Katikati ya vituko hivi ni suala la uandikishaji wapiga kura katika Daftari la Kudumu, ambalo ndilo litakaloamua ni nani kati ya wakazi wa kisiwa hicho watashiriki upigaji kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
Tuseme tu kwamba kwa hali ya mambo tunayoona yakiendelea Pemba, huku wahusika wakuu ambao wangeweza kubadili au kuingilia kati ili hali irejee katika utaratibu wa kawaida wakijifanya mbuni zika kichwa mchangani, isipodhibitiwa sasa, hakika tunakaribisha matatizo ambayo kama methali hizo tulizotaja zinavyoashira, yatatushinda nguvu.
Kama Taifa tuna mapungufu mengi, lakini pengine kati ya hayo, upungufu wetu mkubwa ni dhana au kufikiria kwamba kama kuna matatizo, kama haya ya Pemba, basi tukiyanyamazia, muda ukapita, yatajitibu yenyewe au umma utayasahau! Hakika ni kutokuona kudhani kwamba matatizo haya ya Pemba yatakwisha kwa staili ya kuyanyamazia.
Tunajua kwamba chumbuko la matatizo haya ni vyama viwili vya siasa; Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) ambavyo kila kimoja kinafanya kila aina ya jitihada kuhakikisha kwamba kinapata ufuasi mkubwa huko, hata kama ufuasi huo utakuja kwa gharama za vurugu.
Ni maoni yetu kwamba vyama hivi viwili vimeshindwa kujinasua katika mtego huu wa kichochezi ambao tangu mwaka 1995, tuliporejea katika mfumo wa siasa za vyama vingi, umeifanya Pemba na hata Unguja, kuendesha mambo ya kila siku ya maisha ya kawaida ya wananchi na ya kiutawala kwa misingi ya u CCM na u CUF.
Viongozi wakuu wa vyama hivi wamemwaga sumu ya u CCM na u CUF miongoni wafuasi wao, na sasa inaelekea kwamba sumu hii imeanza kukolea ikiacha wananchi kuishi kwa visa na visasi kwa kuwa tu wanaabudu katika itikadi tofauti.
Tuwaombe wananchi wa Pemba waelewe kwamba Pemba ni muhimu kuliko mtu mmoja mmoja. Kwamba sote tutaisha lakini Pemba, na kwa maana hiyo Tanzania, itabaki. Kwamba tunao viongozi wanaotutangulia katika kutafuta maslahi yetu na ya vyama, lakini tusifike katika kiwango cha kuamini kwamba maslahi yetu binafsi na ya vyama ni muhimu kuliko maslahi ya Taifa tukaruhusu vitendo ambavyo ni vya uvunjaji nchi.
Tuwaombe pia viongozi wa kambi hizi mbili, kwamba maslahi ya nchi ni juu ya maslahi yao binafsi na ya vyama vyao. Watu hufa na vyama hufa, lakini nchi hudumu. Mchezo wanaofanya viongozi wetu ni mauti kwa nchi. Furaha yao ni mauti kwa nchi. Watuepushe na vituko hivi Pemba.
 
Tuwaombe pia viongozi wa kambi hizi mbili, kwamba maslahi ya nchi ni juu ya maslahi yao binafsi na ya vyama vyao. Watu hufa na vyama hufa, lakini nchi hudumu. Mchezo wanaofanya viongozi wetu ni mauti kwa nchi. Furaha yao ni mauti kwa nchi. Watuepushe na vituko hivi Pemba.

Mola aliepushe balaa hili linalopikwa kwa nguvu zote.

Poleni sana ahali zangu kule Konde, Utaani na pujini bila kusahau Ole.
 
Back
Top Bottom