Somo la pili
Uchu wa Mzee Mikidadi
*******
Nilipomaliza darasa la sita, nilichaguliwa kuingia la saba katika shule ya boda, mbali sana na kwetu. Kufika kule nikafanya urafiki na kijana mwenzangu Juma Mikidadi, yeye kwao karibu na pale pale shule. Juma akawa rafiki yangu sana. Basi zikafika siku za pasaka, ambapo watoto watokao jirani huruhusiwa kwenda kwao. Juma hakutaka kwenda kwao peke yake, akaniomba twende wote. Tukaomba ruhusa kwa Mkuu wa Shule, tukaenda kwao kwa mapumziko ya siku mbili.
Mzee Mikidadi si mtu mdogo, tulipofika akatushughulikia sana. Haukupita muda tukaona kuku anakamatwa, kapewa Juma kumchinja. Tukaona kwamba leo uhondo. Saa za kula zikafika, watoto wote tukakusanyika. Likatandikwa jamvi kubwa sana sote tukaenea. Likaletwa sinia la wali, na bakuli la nyama ya kuku; nyama zimejaa tele. Mimi mgeni natazama wenzangu wanavyofanya. Watoto wote wametulia kimya; wanamngoja Mzee Mikidadi.
Mara Mzee Mikidadi kafika. Kashika bakuli anatia mchuzi katika sinia la wali. "Kuleni wanangu, sikukuu yenu hii". Mzee Mikidadi filikichi kinywani, na bakuli kalisogeza miguuni pake. Basi sisi tunaendelea kula wali kwa mchuzi. Tumekula mpaka tunakaribia kushiba; lakini wali kwa mchuzi tu, nyama hatujapewa bado. Lakini Mzee Mikidadi akimaliza matonge mawili anaingilia paja, ama shingo, ama nyama zingine tamu tamu za kuku. Na kutuhimiza haachi, "Kuleni wanangu, sikukuu yenu hii."
Mwisho kabisa vikabakia vibawa, na miguu, na vipapatio. Mzee Mikidadi anaanza kutunyofolea kila mtu kidogo-kidogo, afutike mkono wa kushoto. Hatuna ruhusa kula kinyama hicho mpaka sinia la wali limemalizika. Mzee Mikidadi sasa ameshiba, ananawa na kuondoka. Na sisi tukalimaliza sinia la wali tupate kunyofoa vinyama vyetu.
Ni jambo zuri sana kusisitiza heshima ya watoto wakati wa kula. Haifai watoto wazoee kula ovyo bila ya utaratibu, kama watoto wa kitwana. Lakini haifai vile vile taratibu hizo za kula ziwanyime waoto aina za chakula zinazohitajiwa sana katika kujenga mwili wao. Watoto wanakonda, nywele zinageuka rangi, maradhi hayawaishi, si kwa sababu tu hawapati chakula kilicho bora. Ukiwaangalia watoto namna hiyo matumbo yao yametuna kwa ajili ya kushiba; ila chakula chenyewe hakina faida nyingi mwilini. Nyama na vyakula vingine vyenye mwili watoto hawavipati, hata kama sikukuu hii yao.
Kwetu mtoto hali filikichi ya kuku; eti mwiko. Na kumbe filikichi ina thamani kubwa sana ya chakula cha kujenga mwili. Anakula Mzee Mikidadi, mifupa yake isha komaa, haina haja ya kukua tena!
Watoto wetu ndio watakaoijenga Jamhuri hii; Tanzania hii ni yao wao. Tusiwanyime chakula bora kwa visingizio vya kufunza adabu, au vya mila zinazomfanya Mzee Mikidadi ale nyama yote, na watoto waambulie mchuzi. Kama sikukuu hii ni yao, basi lazima tuwaachie wafaidi, na wapate faida ya chakula katika kujenga miili yao.