Viongozi wa ukawa na tabia ya kuku.

Viongozi wa ukawa na tabia ya kuku.

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Joined
Nov 22, 2012
Posts
1,985
Reaction score
1,286
Kiroho safi niwapongeze viongozi wa vyama vya CHADEMA, CUF na NCCR kwa mashirikiano katika suala hili la mchakato wa katiba mpya. Wanachama na wapenzi wa vyama hivyo na wapenda mabadiliko wanatamani mashirkiano hayo yasikomee kwenye mchakato huu wa katiba tu, lakini yaende hadi kwenye uchaguzi mkuu ujao, kwani wana amini kupigana kwa kila chama kivyake dhidi ya CCM ni moja ya miongoni mwa sababu inayopelekea CCM kuendelea kushinda.

ukawa.jpg
Mapacha Matatu.

Pamoja na kuwapongeza viongozi hawa, na pamoja na imani ya wanachama wao juu ya mdudu huyu aitwaye UKAWA, napenda kutumia jukwaa hili mosi kwa kuonesha mashaka yangu juu ya uthabiti wa nia ya mapacha hawa watatu katika kufuata njia ya mashirikiano na pili kwa kuwataka wanachama wao wavichunguze vitendo vya viongozi wao kabla ya kuwaamini jumla.

Imethibiti pasina kigegezi chochote kuwa nia mahala moyoni na vitendo huja kudhihirisha nia iliyofichikana kwenye moyo, hivyo basi maneno kuwa “tutafanya hivi” au “tutafanya vile” katu hayawezi kuwa “nia” na wakati mwingine huwa ni istizai wazifanyazo waloshika mpini dhidi ya wale walo shika makali. Mshika makali hana budi kumtii mshika mpini kinyume chake ajiandae kutoa mguno.

Viongozi wa vyama nilivyovitaja hawana nia ya dhati ya kuleta mabadiliko ya kisiasa katika nchi yetu. Kitendo chao cha kudhihirisha nia njema kwa kupitia ndimi zao lakini utekelezaji wa nia hizo kuwa sufuri ni kiashiria tosha cha ukosefu wa nia ya dhati. Kama nia zao ni za dhati, basi viongozi hawa watakuwa na tatizo la usaahulifu uliokithiri kama kuku.

SAMWELI SITTA NI SPIKA WA VIWANGO, HIVYO APEWE UENYEKITI.
Ilipodhihirika kuwa si CUF, si CHADEMA na wala si NCCR iliyotoa mtu kugombea uenyekiti wa bunge la katiba nilidhani vyama hivyo vilidhamiria kumfanya Hashimu Rungwe kuwa mwenyekiti wa bunge hilo. Kura alizopata Rungwe ukilinganisha na idadi ya wajumbe toka upinzani zilidhibitisha kile kilichosemwa kuwa vyama vya upinzani vilikuwa vinampigia kampeni Samweli Sitta katika makorido ya bungeni: vimemo vilitembea na Mh Mbowe alitia fora katika kuvisambaza.

Walewale waliokuwa wanampigia upatu Sitta ndio hao hao wanaolalamikia utendaji wa Mwenyekiti huyo wa bunge maalumu. Yaani walisaahu kabisa kuwa Samweli Sitta ni kada wa chama cha mapinduzi kiasi wampigie kampeni. Swali la kukera; kama walisaaahu kuwa Sitta ni CCM watashindwa kusaahu malengo na makubaliano yao chini ya mwavuli ya UKAWA? Machale kundesa, ngastuka.

WINGI WA WAJUMBE WA CCM NA SERA YAO YA SERIKALI MBILI.

Viongozi hawa wamesaahu kuwa kupata katiba mpya kwa amani na utulivu ni hisani ya CCM, bila hisani ya CCM katu hatuwezi kuipata bila mtutu wa bunduki kwanza. Kutokana na wingi wa wajumbe wa CCM kwa vyovyote vile wao ndio walioshika mpini na sisi umeshika makali.

Mfano mzuri sheria ya mabadiliko ya katiba iliyotungwa awali kabla ya marekebisho yake ilikuwa ni mbaya na ililalamikiwa sana. Ubaya ule ulilalamikiwa ndani na nje ya bunge kabla hata haujawa sheria, lakini wabunge wa CCM kwa wingi wao walipuuza hoja nzito za akina Tundu Lissu na hatimaye wakaupitisha ule muswada pamoja na kwamba wapinzani walitoka nje. CCM kwa ihsani yake wakairudisha sheria bungeni ikafanyiwe marekebisho mara baada yaa wapinzani kukutana na rais wa nchi na mwenyekiti wa CCM.

Hapa utagundua pia kuheshimiwa kwa rasimu ya Warioba na makada wa CCM waliopo bungeni ni ihsani tu, wapinzani wamefanya kosa kubwa kudhani CCM wako tayari kuachana sera yao ya serikali mbili, ukweli ni kwamba CCM wanachofanya sasa ni kutumia mchakato huu kuhalalisha ubabe wao waliomfanyia Abdul Jumbe miaka 30 iliyopita na si vinginevyo.

Nafikiri badala ya kuikaba koo CCM ichane na serikali mbili ni bora nguvu hizo zingetumika katika kuleta katiba mpya yenye tume huru ya uchaguzi na yenye kufuta sheria zote mbovu na kandamizi hata kama katiba hiyo itakuwa ya serikali mbili. Tukiitupia jicho historia utagundua ni rahisi CCM kutufanyia ihsani ya tume huru ya uchaguzi kuliko hata ihsani ya serikali tatu.

WAMESAAHU KUWA TUME UCHAGUZI NI ILEILE.

Hivi vyama, hivi vimesaahu kuwa tume itakayoendesha zoezi la kura ya maoni ni ileile inayolalamikiwa tangu mwaka 1995 kwa kundesha uchaguzi kishabiki badala ya kihaki? Tangu mwaka 1995 wapinzani wanalalamika kuonewa na kuibiwa chini ya tume hii, je wanategemea muujiza au uchawi kwenye zoezi la kura ya maoni?

Ikitokea bunge maalum la katiba likiandika rasimu yenye serikali tatu, basi CCM itazunguka nchi nzima kupiga kampeni ya kukataliwa hiyo rasimu. Ikiwa tangu mwaka 1995 tume hii inaipendelea chama dola itashindwa kukipendelea kwenye kura ya maoni? Kwavyovyote vile CCM itashinda na katiba ya mwaka 1977 ambayo ni katiba mbaya kabisa itarudi mzigoni. Hapa utaona ni bora wapinzani washike hayo makali vizuri ili bunge maalumu litoke na rasimu itakayoungwa mkono na CCM lakini rasimu ambayo itakuja na tume huru ya uchaguzi na kufuta sheria kandamizi.

WAMESAAHU KUWA WATANZANIA NI WALEWALE.
Pamoja na kwamba tume ya uchaguzi ni ilele lakini watanzania ni walewale, watanzania ambao hawana ujasiri wa kuiwajibisha serikali yao kama walivyo wamisri au watunisia.

UKAWA wametoka nje na kufanya mikutano ya hadhara na maandamano. Wanasema na kulalamika mbele ya watanzania kuanzia saa kumi jioni hadi saa kumi na mbili jioni. Wakimaliza wao hao UKAWA na watanzania wanalala. Likitokea sakata la Dengue lililo muua daktari au akitokea babu wa Loliondo na kikombe chake watanzania wanasaahu kila kitu walichoambiwa Jangwani na Dr. Slaa.

UKAWA warudi bungeni washirikiane na CCM japo kwa kutupatia katiba ya tume huru ya uchaguzi, kisha watumie majukwaa kutoa elimu ya uraia yenye lengo ya kubadilisha fikra mgando za baadhi ya watanzania badala ya kutumia majukwaa hayo kuimba ufisadi wa CCM tu.

CUF CCM B
CUF iliitwa CCM B na viongozi wa CHADEMA mara baada ya chama hicho kuunda serikali ya mseto na CCM. Mbowe, Dr Slaa na wanachama wa CHADEMA waliita CUF, CCM B huku wakijua fika mashirikiano yale ni ya kikatiba na si ya kichama. Huenda yatakuwa ni maswali ya kukera ila sina budi kuyauliza hapa: Ni CUF ipi ni CCM B na CUF ipi inayounda UKAWA? Au CHADEMA sasa imeamua kushirikiana na CCM B? Au mara hii wameshasaahu? Kama wamesaahu hili watashindwa kuusaahu UKAWA?

CUF CHAMA KINACHOTETEA USHO-GA.

CHADEMA chini ya mwavuli wa kambi rasmi ya upinzani bungeni ilisema kuwa CUF ni chama cha kileberali, chama ambacho pamoja na mambo mengine kinatetea haki za ma-shoga. Yalisemwa mengi, ila katika majukwaa na mitandao ya kijamii viongozi na wanachama wa CHADEMA waliituhumu CUF kama chama kinachotetea masho-ga hasahasa kwa kauli yao ya “HAKI SAWA KWA WOTE”

Mimi bado nipo na maswali yangu ya kukera: Hivi ile kauli mbiu ya” HAKI SAWA KWA WOTE” ya CUF imefutwa? Hivi sasa hivi CUF si chama cha Kiliberali? Hivi viongozi wa CHADEMA wamesaahu maneno yao haya? CUF imesaahu ilivyochachamaa pale bungeni kuitwa watetezi wa mash-oga? Haya wamesaahu? Kama wamesaahu watshindwa kuusaahu UKAWA?

MBOWE NA GARI LA SERIKALI.
Mbowe alitangaza kuwa asingetumia gari la serikali kwa lengo la kupunguza matumizi ya serikali na kutekeleza ilani ya CHADEMA kivitendo. Hata hivyo kiongozi huyo hata sasa anatamba mitaani na gari hilo ambalo alisema asingelichukua. Hivi alipoenda kulichukua alisaahu ahadi yake? Kama alisaahu, je atashindwa kuisaahu UKAWA?

KAFULILA NI SISIMIZI, TENA AMEFULIA.
Mh Kafulila alipotoka CHADEMA aliitwa majina mengi mabaya na viongozi wa CHADEMA. Dr Slaa alimfananisha Kafulila na sisimizi, kamavile binadamu asivyoweza kumvumilia sisimizi na ndivyo CHADEMA ya Dr Slaa ilivyoshindwa kumvumilia Kafulila. Leo hii Kafulila ni waziri kivuli na Mbowe ndio kioongozi wa kambi. Hivi usisimizi wa Kafulia umeisha lini?

MWISHO.

Kama vyama hivi vimesaahu mambo muhimu niliyoyainisha hapo juu vitashindwa kuusaahu huo UKAWA? Hivi katiba ya sasa katiba itakayo andikwa upya hata kama ina serikali mbili ipi bora? Izingatiwe hiyo mpya wapinzani na wananchi wameshirikishwa. Tusijidanganye, CCM hawana nia ya katiba mpya yenye kuleta mabadiliko makubwa, hivyo basi shabaha yetu hayo mabadiliko madogo yawe na tija kwetu kwenye uchaguzi ujao.

Njano5.
0784845394.
 
Tatizo tumekuwa wepesi mno kusahau, halafu wengi hatujui kuwa licha ya kukata kote kote, Msumeno mkali mno, na ukiweka mkono kujaribia, wakati unatoa mguno, utakuwa ulikwishaumia.
 
Back
Top Bottom