Viongozi wa Kiafrika waache kutumia dhana ya uzalendo kuharalisha udikteta wao

Ntile II

Member
Nov 19, 2015
22
12
Rai February 2016

Na. Joel Ntile

Mwishoni mwa wiki iliyopita tarehe 30 na 31 ya mwezi wa kwanza ulifanyika mkutano wa 26 wa wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), makao makuu mjini Addis Ababa Ethiopia. Mkutano huo uliweza kuleta hamasa na mvuto wa kufuatilia kile kilichokua kinaendelea mkutanoni hapo, baada ya hotuba ya ufunguzi iliyotolewa na Mwenyekiti wa Umoja huo wa Afrika aliyekuwa anamaliza muda wake Rais Robert Mugabe wa Zimbwabwe kutumia lugha na matamshi makali na ya kijasiri kutetea hoja ya kuwepo uwakilishi wa kiti kwa Waafrika katika balaza la usalama la umoja wa Mataifa (UNSC) na kuzishtumu nchi za ulaya na Marekani kujiona wao ndio wenye haki ya ujumbe katika balaza hilo.

Ni Mwafrika mtumwa wa Kifrikra pekee ndiye atakayepinga hoja ya Rais Mugabe ya kuwepo kwa kiti cha kudumu kwa bara la Afrika katika balaza la usalama wa Umoja wa Mataifa. Kwa kuwa sasa tupo katika zama za ukweli na uwazi, kwamba lazima tukubariane mataifa yote ni sawa na haikubaliki kuona mataifa machache yanajivika vilemba vya ubwana fahari na kujiona wanayo haki ya kuwaamuliwa watu wa mataifa mengine juu ya maisha yao kiulinzi, usalama, siasa, uchumi au kijamii.

Lakini pia katika zama hizi za ukweli na uwazi basi lazima pia tukubariane kwamba tabia ya Kimangimeza miongoni mwa viiongozi wengi wa Kiafrika ya kuutumia uzalendo kama ngao ya kujikingia kifua udikteta wao inahatarisha demokrasia, ustawi wa watu na heri kwa umma. Tumeona wapo viongozi wengi waliopo na waliopita wa kisiasa waking’ang’ania madaraka kwa kutumia nguvu jeshi na wanausalama kwa kuhakikisha wanaendelea kuwepo madarakani milele kwa kujiona kwamba wana hati miliki ya kuyaongoza mataifa yao kwa kuwa wao ndio waliosaidia kupatikana kwa uhuru wa mataifa yao au ukombozi kutoka tawala dhalimu zilizowatangulia.

Mzee Wetu Robert Mugabe mimi namheshimu na kukubaliana nae kwa mambo mengi sana kama Mpigania uhuru, Mmajumuhi wa Afrika, Mwanafalsafa, Mwanaharakati, kiongozi wa kitaifa na mwanamapinduzi wa Afrika.
Nakubaliana sana na mzee Rais Robert Mugabe katika sera yake ya Uzawa ambayo mimi nitaiunga mkono daima kwa kuwa Ubeberu unatuaminisha kwamba mzawa na mwekezaji wana haki sawa katika matumizi ya rasilimali za Taifa lakini ukweli ni kwamba kimsingi mzawa ndie mwenye hakimiliki ya rasilimali za taifa lake lakini tofauti na sasa ambapo mwekezaji ndie anayepewa kipaumbele katika umiliki wa rasilimali za taifa kama vile ardhi, madini, wanyamapori nk.

Binafsi kumheshimu kwangu Rais Robert Mugabe wa Zimbwabwe hakuondoi kuusema ukweli wa tabia ya viongozi wengi wa Kiafrika kutumia dhana ya uzalendo kuhalalisha udikteta, ambapo ni kinyume na demokrasia na malengo ya kuwa na Afrika huru. Sisemi kwamba demokrasia ni kitendo cha kubalisha majina ya viongozi au vyama, La hasha! Ila nataka ieleweke kwamba tupo katika zama ambazo watu wanaelewa na wanaweza kutofautisha hizi dhana mbili Uzalendo na Udikteta.

Demokrasia ni utawala halisi wa watu, yaani watu wana mamlaka ya kuchagua viongozi wa serikali wawatakao na kuwa na mamlaka kamili juu ya serikali zao. Sasa sio sahihi umma wa Waafrika wazuiliwe maamuzi yao kwa kisingizio cha upigania uhuru wa Kiongozi au uchama kwa kisingizio cha chama tawala kidumu daima. Hakika waafrika lazima waungane kwa pamoja kupinga aina hii ya uhafidhina (Conservatism) wa vikundi vyaa viongozi au vyama vya aina hii.

Uzalendo haimaanishi kuunga mkono vyama au viongozi waliopigania uhuru hata kama wamesaliti agenda ya mapambano ya ukombozi wa Mwafrika kisiasa, uchumi na kijamii. Lakini pia uzalendo si kuwatukana au kuwakataa tu wazungu kwa maneno wakati familia za viongozi haohao wanaoitwa wa kizalendo zinakwenda kufanya shopping Singapore au Dubai na watoto wao wakisoma na wakimiliki akaunti za benki katika mataifa hayo hayo ya ulaya wanayoyatukana.

Katika taifa la Kidemokrasia lenye viongozi wazalendo lazima waruhusu mapambano ya Kifikra, ambayo yataanza kwa majadiliano kwa kuletwa hoja anzilishi, kisha hoja kinzani na hatimaye hoja mmbadala ambayo kama taifa itakuwa ndio msimamo wa pamoja. Lakini ipo tabia ya viongozi wengi wa Kiafrika hawa wanaojiona ni wazalendo ya kuona kuwa hoja kinzani yoyote ni uasi na si uzalendo. Hii imepelekea kuuaminisha umma kwamba kila anayewapinga ni mhaini na mwenye hoja mmbadala ni mchochezi. Kwa mzalendo yeyote hii sio sawa na kinyume kabisa na Agenda walizozokuwa nazo wapigania uhuru hao na vyama vyao vilivyokuwa vya ukombozi.

Uzalendo ni kutekeleza mambo yaletayo heri kwa umma, kuwa na mapenzi mema na watu wote katika taifa bila kujari utofauti wa kidini, itikadi au kabila. Uzalendo ni mapambano ya kimageuzi ili kuhakikisha kunakuwa na maendeleo ya kiuchumi ambayo yatachagizwa na umma wenyewe wa Waafrika hatimaye kuwe na usawa katika utoaji wa huduma za afya, elimu, maji na huduma za haki na kisheria.

Lakini pia si kweli kwamba ili uwe kiongozi mzalendo yakupasa kuwa dikteta, hapana. Kiongozi mzalendo yampasa kuwa na misimamo radiko (Radical) na sio dikteta wa kuhodhi maamuzi ya umma kwa malengo ya kuhifadhi madaraka yake.
Leo hii tunaona viongozi kama vile kina Rais Yowel Musseven wanavyokandamiza wapinzani wao wa kisiasa na kuaidi kwamba hawataachia madaraka kwa hoja nyepesi kuwa wameitoa nchi mbali. Wapo wengine wengi sana.Mfano kuna kauli za viongozi wa chama tawala visiwani Zanzibar nao wamewahi kutoa kauli kama hizo za kudai kwamba wao ndio walipofanikisha ukombozi wa visiwa hivyo ndio maana hawataachia madaraka kwa wapinzani wao wa kisiasa.
Sasa hiki kinachoendelea sasa kwa ujumla katika bara la Afrika twaweza kukiita ni Demokrasia ya kiafrika, ambapo mwananchi anapewa mamlaka yake kwa mkono wa kulia na kunyang’anywa kwa mkono wa kushoto, hivyo basi Waafrika tunahitaji Afrika ya kidemokrasia na sio hiki kinachoitwa Demokrasia ya Afrika ambapo watawala wanatumia dhana ya uzalendo kuhalalisha udikteta ndani ya mataifa yao ili wahifadhi madaraka yao.
Heshima, utu usawa na maendeleo ya kiuchumi katika bara la kiafrika havitaletwa na vitendo vya baadhi ya viongzozi na vyama vya kisiasa kung’ang’ania madaraka kwa kutumia nguvu ya dola pasipo kuangalia nguvu ya hoja na matakwa ya umma ni yepi kwa sasa. Hivyo basi lazima tuijenge Afrika ya kidemokrasia itakayopelekea kupatikana kwa viongozi wazalendo halisi watakatupelekea katika Afrika ya amani nay a kimapinduzi kwelikweli.

Kwa mawasiliano; Simu: +255754255744/ 255652068952
Baruapepe: mwankina1993@gmail.com
 
Neno democrasia linatakiwa lieleweke vizuri kuwa ni RELATIVE.
Afrika has its democracy!
 
Back
Top Bottom