Vigogo wa kampuni 13 za EPA bado kukamatwa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Vigogo wa kampuni 13 za EPA bado kukamatwa

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by BAK, Nov 8, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Nov 8, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,654
  Likes Received: 82,387
  Trophy Points: 280
  Date::11/8/2008
  Vigogo wa kampuni 13 za EPA bado kukamatwa
  * DPP asema tulieni kazi ndiyo imeanza

  Kizitto Noya
  Mwananchi

  WAKATI kasi ya kuwachukulia hatua za kisheria watuhumiwa wa ufisadi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zikipamba moto; serikali bado ina kazi nzito ya kukata kiu ya Watanzania kufuatia kubakiza kuzifikisha mahakamani kampuni 13 kati ya 22 zinazodaiwa kuchota Sh133 bilioni katika akaunti hiyo.

  Mpaka sasa wamiliki wa kampuni tisa kati ya 22 zinazotuhumiwa kuchota fedha hizo, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti wiki iliyopita kujibu tuhuma zinazowakabili.

  Wakati wananchi wakisubiri kwa hamu kuona vigogo zaidi wa ufusadi wa fedha hizo wanafikishwa mbele ya sheria, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Elineza Feleshi amewataka kutulia kwa sababu kazi ndiyo imeanza na kusisitiza kwamba, hakuna atakayepona.

  Mapema wiki hii Rais Jakaya Kikwete alisema kwa sasa serikali haitoingilia suala la EPA na kwamba, sasa limewachiwa katika mikono ya DPP.

  Watuhumiwa wa ufisadi huo waliofikishwa mahakamani ni pamoja na mfanyabiashara maarufu nchini, Jeetu Patel na ndugu zake Devendra Patel na Amit Nandy ambao kwa pamoja wanadaiwa kutumia kampuni ya Bencon International Limited of Tanzania kuchota Sh2.5bilioni.

  Ripoti ya Kampuni ya Ernest&Young iliyokagua akaunti ya EPA imeonyesha kuwa Jeetu na makampuni yake tisa, alichota Sh10.3 bilioni kwa nyakati tofauti kutoka benki hiyo akitumia nyaraka na kumbukumbu za kughushi.

  Kampuni nyingine zinazodaiwa kuchota fedha kwenye akaunti hiyo na kufikishwa mahakamani wiki iliyopita na wamiliki wake kwenye mabano ni Kernel (Johnson na Mwesiga Lukaza) na Bina Resort na Itoh (Ketan Chohan).

  Nyingine ni Changanyikeni Residential Complex Ltd (Bahati Mahenge, Manase Mwakale, Davies Kamungu, Godfrey Mosha na Eddah Nkoma Mwakale) na Mibale Farm (Rajabu Farijala, Japheth Lema na Rajabu Malanda).

  Farijala na Malanda pia wanatuhumiwa kuhamisha mali kutoka Kampuni ya BB Grancel ya nchini Ujerumani kwenda Kampuni yao ya Money Planners Consultants, kughushi na kuhamisha hati ya Msajili wa Makampuni na Majina ya Biashara (Brela) kwenda kampuni yao ya Kilolo and Brothers.

  Katika hatua nyingine, Lema alifikishwa mahakamani hapo kujibu tuhuma nyingne za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia Kampuni yake ya Njake Enterprises kutoka kampuni ya C. Itoh ya nchini Japan.

  Mashtaka hayo ya ufisadi wa EPA, pia yamewaunganisha wafanyakazi wanne wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambao wanashtakiwa kwa uzembe uliofanikisha wizi huo.

  Wafanyakazi hao ni Ester Leon, Iman Mwakosya, Sophia Joseph na Mwesiga Lukaza ambao wamehusishwa na tuhuma za wizi uliofanywa na Rajabu Malanda kwa kughushi hati ya Kampuni ya Manner Planner Consultants na kuhamisha deni kutoka Kampuni ya B. Grancers Limited ya Ujerumani na Kampuni ya Monner Planner ya Tanzania na Kampuni ya BG Monner.

  Wizi wa fedha za EPA ndani ya BoT, ulifanyika kwa nyakati tofauti na makampuni 22 ikiwamo kundi la makampuni 13 yaliyojichotea Sh 90.3 bilioni.

  Makampuni yaliyoko kwenye kundi hilo na ambayo hayajafikishwa mahakamani ni Vb & Associates LTD of Tanzania, Venus Hotel LTD of Tanzania na Maltan Mining LTD of Tanzania.

  Makampuni mengine ni Bora Hotels & Apartment LTD, B.V Holdings LTD, Ndovu Soap LTD, Navy Cut Tobacco (T) LTD na, Kagoda Agriculture LTD.

  Makampuni tisa yaliyobaki na ambayo hayajafikishwa mahakamani yanatuhumiwa kuiba Sh42.6 bilioni kutoka kwenye akaunti hiyo.

  Makampuni hayo ni G&T International LTD, Excellent Services LTD, Liquidity Service LTD, Clayton Marketing LTD, M/S Rashtas (T) LTD, Malegesi Law Chambers (Advocates), Kiloma and Brothers.

  Makampuni mengine mawili ambayo ni Rashtas (T) na G&T International LTD, kumbukumbu zake ikiwemo nyaraka za usajili katika daftari la Msajili wa Majina ya Makampuni na Biashara (BRELA), hazikuweza kupatikana.

  Fedha za EPA zina historia ya tangu miaka ya 80, lakini ilipofika mwaka 1999 deni hilo lilifikia dola 623 milioni, kati ya hizo dola 325 milioni zilikuwa ni deni la msingi na dola 298 ni riba. Baadaye deni hilo lililongezeka na kufikia dola 677 milioni za Marekani.

  Hata hivyo, chini ya Mpango wa Kununua Madeni (Debt Buy Back Scheme) wa mwaka 1994 kati ya serikali na Benki ya Dunia (WB), waliokuwa wanaidai BoT waliombwa wakubali kulipwa sehemu tu ya fedha wanazodai, wapo waliokubali na wengine kukataa na kuongeza kwamba hadi mwaka 2004, taarifa zinaonyesha kuwa jumla ya dola 228 zililipwa chini ya mpango huo.

  EPA ni akaunti ya madeni ambayo ilitumika wakati wa Mfumo wa Ujamaa, ambayo akaunti yake ilikuwa katika iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) chini ya usimamizi wa BoT.

  Mwaka 1985, EPA ilihamishiwa moja kwa moja BoT, na ndipo mwaka juzi kulipoibuka utata wa tuhuma za ufisadi katika akaunti hiyo kwa mahesabu ya mwaka 2005/06, ambayo utata huo ulisababisha Ernst&Young kufanya ukaguzi kuanzia Septemba6 mwaka jana na kukabidhi ripoti yake kwa CAG mapema Desemba mwaka huo huo.
   
Loading...