Vigogo DECI wahamisha nyaraka

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,722
21,775
Vigogo DECI wahamisha nyaraka

*Wataja zilipo fedha za wateja
*Wanachama wahaha kuzuia gari
*Polisi waingilia kuwatawanya
*Waafiki kusitisha maandamano


Tuesday, 02 June 2009 16:42

Na wandishi wetu


HOFU imetanda kwa wanachama wa Kampuni ya Development Enterpreneurship for Community Initiative (DECI) kufuatia viongozi kuonekana wakihamisha nyaraka za wanachama hao kutoka ofisi za makao makuu, Mabibo Dar es Salaam jana na kuzipelekwa kusikojulikana.

Viongozi hao waliwasili ofisini hapo saa 5:30 asubuhi wakiwa kwenye gari dogo Toyota Corola namba T455ADM na kuanza kutoa nyaraka na kuziweka kwenye gari hilo, kitendo kilichofanya wanachama waliofurika eneo hilo, kuingiwa hofu na kuhoji kulikoni?

"Nani amewaambia kutoa nyaraka zetu? Kwani wao ni Serikali, wanataka kuzipeleka wapi,hakiondoki kitu hapa!" Alisikika mwanachama mmoja kutoka kundi hilo akihoji.

Baada ya muda,viongozi wawili kati ya wanne walioingia katika ofisi hizo, walitoka na kuanza kuondoka na gari hilo hali iliyozua mtafaruku mkubwa na wanachama hao kuziba barabara ili gari hilo lisipite,kushinikiza kujua zinakopelekwa nyaraka hizo.

"Hakuna kupita na gari hapa! Rudisha huko, mpaka mtuambie mnapeleka wapi nyaraka zetu ? Na nini hatma ya fedha zetu, mnatutania sana! Rudisha gari huko!" Alisikika akilalamika mwanachama mwingine aliyekuwa mstari wa mbele kuzuia gari hilo.

Polisi waliokuwa eneo hilo waliingilia kati kutawanya wanachama hao baada ya vurugu hizo kuonekana kupamba moto huku kusisitiza kuwataka kuacha gari hilo liende.

"Kama mnataka amani tupeni maelezo kuhusu zinakopelekwa nyaraka zetu na hatma ya fedha zetu, vinginevyo hakuna amani hapa! Tumevumilia tumechoka, hakuna amani tumesema!" alilalamika mwanachama mmoja huku zogo la maneno likitawala kutoka na kila mmoja kulalamika. Hali hiyo iliwafanya maofisa waliokuwa ndani ya gari kuingiwa hofu na kuonekana kupepesa macho huku na kule.

Hata hivyo, vurugu hizo zilidumu kwa muda mfupi na Polisi walifanikiwa kuwatawanya wanachama hao baada ya kuwatisha kwa silaha kitendo kilichowafanya kuondoka barabarani na gari hilo kupita.

Awali,wanachama hao walikuwa wamejikusanya katika makundi huku wakijadili mambo mbalimbali ikiwemo maandamano makubwa waliyopanga kufanya leo.

Akizungumza na gazeti hili mmoja wa viongozi wa wanachama hao, alisema kuwa wamepata taarifa kwamba Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda amekataa kuyapokea maandamano hayo lakini hata hivyo msimamo wao uko pale pale.

Taarifa zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya wanachama hao zilidai kuwa baadhi ya wanachama waliopanda fedha nyingi wakiwemo viongozi wa Serikali walisharudishiwa mbegu zao baada ya kuibuka sakata hilo na wanaumia sasa watu wa chini.

Wanachama hao walisema wamepoteza imani kwa Serikali iliyopo kutokana na kutosikilizwa matatizo yao ambapo awali ilitangaza kuwa imekamata akaunti za DECI lakini kauli ya Waziri wa Fedha na Uchumi Bw. Mustafa Mkulo imewachanganya baada ya kudai serikali haihusiki na fedha za kampuni hiyo.

Majira lilipata tetesi kutoka kwa watu wa karibu wa DECI kuwa kuhamishwa kwa nyaraka hizo, kunatokana na kumalizika mkataba wa pango hivyo viongozi hao wanalazimika kuhamisha vyombo vyao.


Wakati huo huo, viongozi wa kampuni hiyo wameibuka na kueleza kuwa fedha zote za wanachama hao ziko salama salimini.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Serikali kupitia Waziri wa Fedha na Uchumi Bw. Mkulo, kutoa tamko kupitia vyombo vya habari kuwa haihusiki na fedha za DECI hali ambayo imeibua hasira kwa wanachama wa kampuni hiyo.

Akizungumza jana, Makao Makuu ya DECI, Mabibo,Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Bw. Timoth Ole Loiting'ye alisema fedha zote za washiriki hao zimehifadhiwa katika Benki ya NMB kama Tume ya Serikali ilivyoagiza.

"Hatma ya mbegu za wanachama zipo salama Tume iliyoundwa na Serikali imetoa maagizo ya kuweka fedha zote Benki ya NMB, napenda kuwahakikishia wanachama wote kuwa fedha zao ziko salama" alisema Ole Loiting'ye.

Alisema kampuni yake imeamua kuvunja ukimya kutokana na kauli ya Bw. Mkulo kushindwa kutunza siri za Tume kwani makubaliano yao yalikuwa kutunza siri za Tume hiyo hadi hapo itakapomaliza kufanya uchunguzi wa jambo hilo.

Alisema ameshangazwa na kauli zinazotolewa mara kwa mara na Bw. Mkulo ambazo alidai ni za uchonganishi na zinakiuka makubaliano yaliyofikiwa na kabla Tume hiyo kuanza kufanya kazi ya uchunguzi huo.

Bw. Ole Loiting'ye alisema mbali na hilo, wamekuwa wakisikitishwa kauli ya zinatolewa na viongozi mbalimbali wa Serikali kuwaita matapeli na wezi wa fedha za wananchi wakati wao ni watumishi wa Mungu wanaoheshimika katika jamii.

Alisema waliamua kuanzisha kampuni hiyo kisheria kwa nia ya kuwasaidia wananchi kiuchumi kinyume na inavyotafsiriwa na baadhi ya viongozi wa Serikali.

Alisema kauli hizo zimeanza kujenga chuki kati ya Serikali na wanachama wao hata kabla tume ya hiyo iliyoundwa haijatoa majibu ya nini kifanyike baada ya uchunguzi huo.

Aliwataka wanachama hao kuwa na subira kwani tume hiyo iko katika hatua za mwisho na hivi karibuni itatoa tamko la nini kifanyike kuhusu fedha hizo.

Katika hatua nyingine, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova jana aliitisha kikao cha dharura na viongozi wa Kamati ya Muda ya DECI saa 10 jioni ofisini kwake na kukubaliana kusitisha maandamano hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao hicho, Kamanda Kova, alisema wamekubaliana kusitisha maandamano hayo ili kuepusha matatizo yasiyo lazima ambayo yangeweza kujitokeza wakati wa mkusanyiko huo.

"Hakuna sababu ya kuandamana kama viongozi wa DECI walivyoomba kwani nia yao ni kufikisha ujumbe kwa Serikali kwamba wana kilio cha fedha zao ila sisi kama Jeshi, tumepanga kulishughulikia tatizo lao kwa ukaribu zaidi," alisema Kamanda Kova.

Aidha alisema kuwa kufuatia kusitishwa kwa maandamano hayo, Jeshi la Polisi limechukua jukumu la kufikisha ujumbe wa DECI serikalini kama lilivyo upokea leo kabla ya saa 4 asubuhi.

Kamanda Kova aliwataka wanachama wa DECI kutokubali kutumiwa na vyama vya siasa kwa manufaa ya kisiasa na kwamba kufanya hivyo kutawafanya wadumae kiakili na kushindwa kufanya mambo yao wakati huu wanaposubiri uamuzi wa Serikali kuhusu fedha zao.

"DECI haina uhusiano na siasa, mimi nimejitolea, ofisi yangu kuwa mlango wa kupitishia kero zote za DECI ili malalamiko yaweze kufika serikalini kwa muda muafaka na kupatiwa ufumbuzi kwani mimi niko karibu sana na viongozi wa DECI, hivyo naamini kwamba tutadumisha ushirikiano," alifafanua Kamanda Kova.

Alionya kwamba mtu yeyote atakayethubutu kuandamana leo atashughulikiwa kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na kwamba Jeshi la Polisi lina nguvu ya kufanya lolote ila limeamua kufanya mambo yake kwa kushirikiana na wananchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya DECI, Bw. Issack Kalenge aliwataka wanachama wake kuwa watulivu na kukubaliana na maamuzi waliyofikia kwenye kikao hicho na kumshukuru Kamanda Kova kwa makubaliano hayo.

Naye Meneja wa Taaluma na Uelimishaji wa DECI Bw. Arbogast Kipilimba, aliwataka wanachama kuwa na imani na viongozi wao na kueleza kwamba hawajawahi kuwakana wanachama hao ila wanasubiri maamuzi kutoka serikalini.

DECI ina wanachama zaidi ya 700,000 katika matawi mbalimbali nchini ambapo zinahitajika zaidi ya sh. bilioni 50 ili kuwezeza kurudisha fedha za wateja hao.
 
Back
Top Bottom