Vigogo Chadema ndani ya kashfa nzito

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
VIGOGO wa juu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameingizwa ndani ya kashfa ya kutumia madaraka na ofisi za chama hicho vibaya. RAI lina taarifa kamili.

Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na mmoja wa wakurugenzi wa chama hicho anayeshughulikia masuala ya Bunge (jina tunalihifadhi), wanadaiwa kuomba rushwa kwa baadhi ya makada wa chama hicho ili wawasaidie kupata nafasi ya ubunge wa jimbo na ile ya viti maalumu wakati na hata baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Tayari tuhuma hizo zimeshawasilishwa kwenye Kamati Kuu ya chama hicho na inayotarajiwa kukutana wakati wowote kuanzia sasa.

Mwalimu anatajwa kufanya hivyo katika kipindi alichokuwa akikaimu nafasi ya Ukatibu Mkuu, ambapo anadaiwa kuwaomba rushwa baadhi ya makada wao waliokuwa wakitaka ridhaa ya chama ya kuwania ubunge.

Wakati Mwalimu akipewa tuhuma hizo, mwenzake anadaiwa kuwaomba rushwa baadhi ya makada wa kike wa chama hicho ili awasaidie kupata nafasi ya ubunge wa viti maalumu.

Taarifa kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu waliokutana Machi mwaka huu, jiji Dar es Salaam kabla ya kwenda jijini Mwanza kwenye kikao cha Baraza Kuu, zililiambia RAI kwamba Mwalimu anadaiwa kufanya hivyo kwa nia ya kujinufaisha.

Tuhuma hizo zilifikishwa mbele ya Kamati Kuu ya Chadema na Mbunge wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.

Ilidaiwa kuwa Mwalimu aliomba kiasi cha Sh. Milioni 10 kwa Mbunge wa jimbo la Ndanda, Cesil Mwambe.

RAI lilimtafuta Mwambe kuzungumzia suala hili, hata hivyo hakukubali wala kukataa, lakini zipo taarifa zisizo na shaka zinazothibitisha mbunge huyo kuwasilisha madai yake kwa maandishi ikiwa ni sehemu ya kiambatanisho kwenye madai ya Mbilinyi.

Kiambatanisho hicho cha ushahidi kinaonyesha namna ambavyo Mwalimu, alitoa maelekezo ya kuwazuia viongozi wa Chadema kumnyima ushirikiano Mwambe, kutokana na kukaidi ombi lake.

Mbilinyi alipoulizwa na gazeti hili kuhusu malalamiko aliyopeleka kwenye Kamati Kuu, alikiri kufanya hivyo na kusema kuwa kazi hiyo ameiachia kamati hiyo kuwachukulia hatua zinazostahili viongozi hao kwa mujibu wa taratibu na katiba ya chama hicho.

“Taarifa nimeshafikisha hivyo kama hadi sasa umeona kimya ujue kabisa siku viongozi wakiamua kutoa uamuzi wa jambo hilo naamini hata ninyi (waandishi) mtajua,” alisema Mbilinyi.

Kwa upande wake Mwalimu alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu kama litakuwa mikononi mwa Kamati Kuu ni wazi hana mamlaka ya kulitolea ufafanuzi.

“Siwezi kutolea ufafanuzi taarifa ambazo mnasema zimeshafika kwenye Kamati Kuu, kwa sababu Mwenyekiti ndiye mwenye mamlaka wa kuzungumzia jambo hilo. Hata hivyo siamini kama kweli nimemuomba Mwambe hizo fedha,” alisema Mbilinyi.

RAI liliwasiliana na Mkurugenzi aliyehusihwa katika tuhuma hizo bila mafanikio, mara zote alizokuwa akipigiwa simu alikuwa akiikata na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi, hakujibu.

Alipotafutwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ili kuzungumzia madai hayo, nae hakuweza kupatikana si ofisini kwake wala kwenye simu.

Chanzo Rai
 
Back
Top Bottom