Vigogo CCM wataka Bunge kufumuliwa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Vigogo CCM wataka Bunge kufumuliwa

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Kakke, May 18, 2012.

 1. Kakke

  Kakke JF-Expert Member

  #1
  May 18, 2012
  Joined: Dec 4, 2010
  Messages: 1,797
  Likes Received: 389
  Trophy Points: 180
  Mwandishi Wetu

  Toleo la 239
  16 May 2012


  [​IMG]


  • Wapendekeza kuanzishwa Baraza la Seneti na Bunge lenye mfumo mpya
  • Kikwete apigia debe urais kuhojiwa mahakamani

  KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi iliyokutana mjini Dodoma mapema wiki hii imependekeza, pamoja na mambo mengine, kufumuliwa kwa muundo wa sasa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Raia Mwema limeelezwa.
  Muundo wa sasa ni wa wabunge wa aina tatu: wa majimboni, vitimaalumu na wanaoteuliwa na Rais kwa mujibu wa madaraka yake ya kikatiba.
  Badala yake, yameibuliwa mapendekezo kwamba lianzishwe Baraza la Seneti ambalo litaundwa na wajumbe wa aina mbili; ya kwanza ikiwa ni ya marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar..
  Aina nyingine ya wajumbe wawe ni watakaopatikana kwa njia ya kuchaguliwa, wakiwa ni mjumbe mmoja kutoka kila mkoa.
  Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika vya gazeti hili vilivyoshiriki vikao vya majadiliano katika Kamati Kuu, mjini Dodoma mwanzoni mwa wiki hii, utaratibu huo wa kuanzishwa kwa Baraza la Seneti unalenga kuwatumia marais wastaafu kwa maslahi ya nchi.
  “Tunakoelekea tunaweza kuwa na marais wastaafu wengi iwe kutoka CCM au kutoka vyama vingine vya siasa kama vitaweza kuchaguliwa na wananchi kuingia Ikulu. Busara inaelekeza kwamba marais hawa wastaafu ni vizuri kuwatumia katika kushauri namna ya kuongoza nchi. Hii ndiyo mantiki kubwa ya kupendekeza kuwapo kwa Baraza la Seneti,” kilieleza chanzo chetu cha habari.
  Nchi mbalimbali zimekuwa na mabaraza ya maseneta, ikiwamo Marekani, Uingereza na hata Sri-Lanka iliwahi kuwa na Baraza la Seneti. Uzoefu katika nchi hizo unaonyesha kuwa mara nyingi unapokuwapo mfumo wa Baraza la Seneti ni lazima kuwapo na Baraza la Wawakilishi (Bunge) ambalo wajumbe wake hupatikana kwa kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi, tofauti na ilivyo kwa Baraza la Seneti.
  Katika baadhi ya nchi, Baraza la Seneti linaundwa na wakongwe na wabobezi katika masuala mbalimbali ya utawala na utumishi wa umma lakini pia wajumbe wengine huteuliwa kuingia kwenye Baraza hilo kutoka katika Bunge au Baraza la Wawakilishi.
  Nchini Uingereza, kwa mfano, Baraza la Wawakilishi limekuwa likitambulika kama House of Lords (Bunge la Mabwanyenye) na Bunge la kawaida ambalo wabunge wake huchaguliwa, limekuwa likiitwa House of Commons (Bunge la Makabwela). Marekani pia imekuwa na Baraza la Seneti, sambamba na Baraza la Wawakilishi.
  Tofauti ya vyombo hivyo ni kwamba, Baraza la Seneti linategemewa mno katika kutoa misimamo mizito inayokidhi maslahi ya umma kwa kuzingatia kigezo cha uzoefu wa wajumbe wake. Lakini Bunge au Baraza la Wawakilishi jukumu lake ni kuwasilisha maslahi ya wananchi moja kwa moja kutoka katika majimbo.
  Kamati Kuu ya CCM pia imependekeza kwamba Katiba mpya ya Jamhuri Muungano wa Tanzania itamke idadi ya wabunge au wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ili kufuta michakato wa kuanzishwa kwa majimbo mapya ya uchaguzi mara kwa mara bila hata baadhi ya majimbo kukidhi vigezo vilivyopata kuanishwa.
  Katika suala la vitimaalumu imependekezwa kuwa kila chama kipate wabunge wa vitimaalumu kwa kuzingatia asilimia ya majimbo ya uchaguzi waliyoshinda.
  Matokeo ya urais kuhojiwa kortini
  Katika kikao hicho, taarifa zaidi zinaeleza kuwa Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti CCM na ndiye aliyekuwa akiongoza vikao vya chama hicho, alikuwa mstari wa mbele kuwashawishi wajumbe kuridhia kwamba, Katiba mpya itambue na kuruhusu mchakato wa kuhoji matokeo ya kura za urais mahakamani.
  Azimio hilo pia linatajwa kupitishwa na Kamati Kuu na kusisitizwa kuwa ni lazima uwekwe muda maalumu kwa wanaotaka kuhoji matokeo ya urais mahakamani ili kesi husika ziweze kumalizwa na Mahakama katika muda mfupi
  Lakini kwa upande mwingine, gazeti hili limeelezwa kuwa yapo mambo ambayo Kamati Kuu imependekeza yaendelee kuwapo katika Katiba mpya kama yalivyo katika Katiba ya sasa, ikiwa ni pamoja na haki ya kupiga kura na kuwapo kwa mihula ya uongozi wa kuchaguliwa na kwamba, wananchi ndiyo waachwe waamue muhula uwe wa miaka mingapi.
  Kwa sasa muhula wa uongozi wa kuchaguliwa ni miaka mitano katika nchi nyingine mihula ya kukaa madarakani inapishana kati ya miaka mine hadi saba.
  Tume ya Maadili
  Kwa mujibu wa habari hizo, CCM kupitia Kamati Kuu yake imependekeza pia kwamba Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma itambuliwe katika Katiba mpya na kwamba ijengewe mifumo huru ya kufanya kazi bila woga.
  Kwa sasa tume hiyo imekuwa ikiripoti kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na imekuwa chini ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utawala Bora kama ilivyo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
  Utaratibu wa sasa kwa muda mrefu umekuwa ukilalamikiwa kwamba hautoi fursa kwa tume kuwa huru katika kuwashughulikia viongozi wa umma wanaokiuka sheria ya maadili na wengine wamekuwa wakishinikiza kuwapo kwa uwazi wa kisheria katika utendaji kazi wa tume hiyo.
  Ni mapendekezo ya CCM
  Hata hivyo, hayo na mengine yanatajwa kuwa ni mapendekezo tu ya CCM kama taasisi na chama tawala na kwamba, hayazuii Watanzania kwa ujumla wao kuwa na maoni mengine tofauti.
  Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, CCM kinatarajiwa kuwaelimisha wanachama wake kuhusu masuala ya msingi wanayodhani ni muhimu kuwamo katika Katiba mpya ili kupata uungwaji mkono kutoka kwa umma na hatimaye masuala hayo yawe sehemu ya Katiba mpya.
  Kudhibiti mfumuko wa bei
  Katika hatua nyingie, jana Jumanne, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM-Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu vimeitaka Serikali kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa muhimu nchini, na hasa chakula.
  “Kutokana na kuwapo kwa hali ya kupanda mno kwa bei za bidhaa nchini ambako kunasababishwa na mambo mbalimbali, ikiwamo mavuno duni na kupanda kwa bei za nishati ya mafuta duniani, Halmashauri Kuu imeamua pamoja na Serikali kuendelea kuchukua hatua za muda mrefu na wa kati kukabiliana na tatizo hili, CCM inaiagiza Serikali kuchukua hatua za haraka za muda mfupi ikiwamo kuangalia upya baadhi ya kodi katika vyakula pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika sukari,” alisema Nape naye katika mazungumzo yake hayo na waandishi wa habari mjini Dodoma

  CHAZO raia mwema
   
Loading...