Utetezi wa Mabadiliko Ya Kweli - 1 "Kosa la Ndugu Zetu"

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,742
40,874
Kama Nilivyoahidi...



Na. M. M. Mwanakijiji


Ndugu zetu waliotaka nchi ikubali mabadiliko yale walituambia kuwa wamefanya hivyo katika mtindo wa ‘kubadili gia angani’. Walitaka tuamini kuwa kubadili kwao “gia” angani lilikuwa jambo bora zaidi na la hekima na kuwa wale wote ambao tuliamini katika mabadiliko ya kweli tulipaswa kushangilia na kujiunga na msafari huo uliobadili gia angani kwa sababu tu tulikuwa pamoja tulipoanza safari.


Katika dakika hizi tano naomba kupendekeza kuwa ndugu zetu walichokifanya ni kikubwa zaidi na cha kutisha zaidi; walichokifanya ni kile ambacho baadhi yetu hatujaweza kukielewa na kukisamehe hadi hivi sasa. Ndugu zetu hawa kama wangebadili gia kweli naamini mwendo wa safari ungebadilika; kwamba labda tungeenda mwendo wa kasi zaidi wakati ule na kwenda kuchukua ushindi mnono kwenye sanduku la kura. Ndugu zetu hawakubadili gia angani; hawakuwa na ujasiri wa kubadili gia hizo na kwa hakika walichokifanya ni kile ambacho hadi leo hawajakubali kuwa ni kosa kubwa zaidi la kisiasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana kufanywa na chama cha siasa.


CHADEMA na washirika wake katika UKAWA – lile dubwasha lililovuruga juhudi za kupata Katiba bora mpya ya nchi yetu - walichokifanya mwaka jana siyo kubadili gia kama viongozi wao walivyodai – walichokifanya ndugu zangu - KUBADILI SAFARI ANGANI!


Tulipoanza safari hasa baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010 ni kutambua kuwa CCM isingeweza kuondolewa madarakani chini ya kanuni na sheria zile zile; tulitambua wakati ule kuwa ili kuiondoa CCM madarakani kulihitajika mabadiliko ya ndani ya chama (mfumo, sera na mwelekeo) ili kukabiliana na CCM. Tulitambua pia kuwa kulikuwa na haja ya kushinikiza mabadiliko makubwa ya mfumo wetu wa uchaguzi ili kuweza kupambana na CCM katika uwanja sawia; uwanja ambapo sheria na taratibu zinafunga pande zote sawasawa. Bahati mbaya sana hili halikutokea.


Hata hivyo tulitegemea pia kuwa pamoja na kutokufanyika kwa mabadiliko haya upande wetu ungeweza kusimamisha watu kugombea ambao walikuwa wanaelewa safari yetu tuliyoianza na kuwa kuwa wagombea wetu wangekuwa na mvuto wa hoja na sera wa kuweza kuwashinda wagombea wa CCM katika nafasi zozote zile. Hili tuliliamini. Lakini zaidi tuliamini kuwa mabadiliko ya kweli ni lazima yaeleweke; baadhi yetu tuliamini kabisa kuwa mabadiliko ya kweli ni zaidi ya kutaka tu kuiondoa CCM madarakani! Hili nitalieleza katika kipindi kingine.


Safari yetu tuliyoianza ilikuwa ni dhidi ya ufisadi, uongozi mbovu, vita dhidi ya ubadhirifu na dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka. Safari yetu ilikuwa inahusu kuiletea Tanzania uongozi unaoongozwa na uadilifu na ambao unaelewa mahitaji ya Watanzania. Safari yetu tulipoianza ilikuwa inahusiana na kuleta mabadiliko katika utendaji kazi wa watumishi wote wa umma. Ilikuwa ni safari ya mabadiliko ya kweli.


CCM wakijua hatari iliyokuwa mbele yao hasa baada ya kuchakachua uchaguzi wa 2010 walijua mambo kadhaa yasingebadilika basi uhai wao na uwepo wao madarakani ulikuwa ufikie kikomo mwaka jana: kwanza kama CHADEMA ingemsimamisha mgombea wake wa 2010; hili CCM walilijua na walilielewa vizuri kweli; na kwa muda mrefu tangu 2010 walianzisha propaganda kali ya “kutokukubalika” kwa Dr. Slaa na kuwa “kama CHADEMA inataka kushinda uchaguzi isimsimamishe Dr. Slaa!”


Kinachonishangaza ni kuwa ndugu zetu hawa wamesahau kabisa hili; na wengi walikuwa wanajua hili linafanyika haikuwa siri. Ukiingia JF kuna mada nyingi hasa kati ya 2010-2015 ambapo makada mashuhuri wa CCM kwenye mtandao walikuwa wanarusha kila aina ya makombora ili “kuishauri CHADEMA” isimsimamishe Slaa! Tafuta mada zivuatazo ujionee nini ninachokisema. Huu ni mfano mmoja tu:


Dr. Slaa Katika Mkakati Maalum wa Kuing’oa CCM Madarakani


Sababu zilizokuwa zinazotolewa sana dhidi ya Slaa kwa mtu anayeangalia sana utaona ni sababu ambazo leo zinatolewa dhidi ya Magufuli! Walimkwepa Slaa kutoka CHADEMA hawakujua wana mtu mwingine ndani mwenye fikra na mwelekeo wa mabadiliko labda makali zaidi ndani ya CCM! Hili somo la wakati mwingine…


Wenzetu walipojaribiwa walishindwa kusimama! Wakaamua kuuza cha kwao kizuri na kukopa kibovu cha jirani! Wakaamua kubadili safari angani. Wakaacha safari dhidi ya mambo hayo yote wakaja na safari yenye lengo moja tu “mengine yote baadaye”. Wenzetu katika safari yao hiyo mpya walisema tu “tuitoe CCM mengine yote baadaye”. Tulipowauliza tukishaitoa nini kitafuatia wakatuambia “haijalishi nini kitafutia! Tuitoe kwanza!” Tulipowabana watuambie sasa CCM ikitoka nini kinafuatia wakasema kwa maringo “haijalishi hata mawe yakiingia hakuna shida la maana ni CCM itoke kwanza”. Wenyewe waliamini kuwa wanazungumza kwa hekima na uzalendo! Katika lengo lao la kutaka kuitoa CCM wakaangukia mikononi mwa chembe za ufisadi zilizokuwa CCM wakazikumbatia kwa furaha na kuzizungushia mikono kwa fahari! Wakatuambia ati “haya ndio mabadiliko!” Safari yao ikabadilika! Na sisi wengine tukashuka bila aibu tena kwa fahari!


Kwanini tupelekwe ambako hatukupanga kwenda? Kwanini tushabikie safari ya mahali ambapo hatukujui!? Ni kweli tulianza safari pamoja na tuliamini tuko pamoja lakini wenzetu walipoamua kubadili safari vipi na sisi tuendelee kwenye safari isiyo yetu?


Ndugu zangu, safari ambayo sisi wengine tuliianza inaendelea; kitu pekee ambacho wengi wetu hatukufikiria kinawezekana, na kwa miaka milioni moja tusingeamini kinawezekana ni kuwa mabadiliko tuliyoyapigania yanaoongozwa na mtu kutoka CCM! Lakini cha kusikitisha zaidi ni kuwa wale ambao tulianza nao safari wao sasa ndio wamekuwa wapingaji wakuu wa mabadiliko ambayo wao wenyewe waliyaimba kwa karibu miaka ishirini sasa! Wale ambao walitaka viongozi wabovu washughulikiwe leo wamekuwa wakitetea kinachoitwa “haki” za viongozi wabovu; wale ambao walitaka Rais anayetumia madaraka yake vizuri leo wanahoji kwanini anatumia madaraka hayo!


Ndugu zangu, safari hii inahitaji kutetewa; inahitaji kusimamiwa kwani tayari tumeshaona kila dalili za upingaji na upinzani wa matokeo ambayo Watanzania wanayataka. Wapo wengine hadi wameanza kuimba sifa za viongozi waliopita; wengine wakisema wazi ati wanawamiss viongozi wale; yaani wanataka turudi kule ambako tulishaaga!


Tukumbuke, wenzetu hawa, ndugu zetu na marafiki zetu; tumetofautiana nao kwa sababu hawakubadili gia angani, bali kwa sababu walibadili safari angani! Walitaka kutupeleka ambako tuliapa hatutokwenda. Tulishuka na kudandia gari - hata kama ni mkweche - lakini linatupelekea tulikopanga kwenda! Tutashughulika na huu mkweche tukiwa safarini!


Nitaendelea, siku tano, hoja tano, dakika tano! Utetezi wa Mabadiliko ya Kweli:


Je, Magufuli ni Dikteta, Je, anatumia madaraka yake vibaya? Je, anavunja sheria? Je, Magufuli hili na lile…



Kesho nitaanza kujibu maswali hayo, In Shaa Allah!


M. M. Mwanakijiji (Zama Mpya - Ya OZ News Network)
 
Kama Nilivyoahidi...



Transcript ya hoja yangu ya leo, itawajia baadaye, ikimpendeza Mungu.


Kuna vitu nakubaliana navyo kwenye hii hotuba yako, lakini pia kuna vitu sikubaliani navyo. Mfano ni pale unapompigia debe Slaa kuwa ndiye mgombea tu aliyefaa kwenye urais lupitia Chadema.

Mimi ningefurahi kama swala la kugombea lingeachwa huru kabisa ili kila anayetaka kuchukua form achukue, kusiwe na kukatishana tamaa na kusutana eti fulani akionyesha nia inakuwa ni uroho wa madaraka. Mwisho wa siku tuwe na watu hata mia wa kuwachuja na kuwapigia kura za kuwapitisha kwenye tiketi ya chama.

Kugombea urais ni haki ya kila mtanzania mwenye sifa za kugombea, sii hati miliki ya Slaa wala Lowasa.
 
Msubiri jingalao na Simiyu Yetu waje wakupongeze, mimi hata kusikiliza naogopa kupoteza mb zangu wakati najua huna mpya
 
Yaani wewe Mwanakijiji kwa jinsi ulivyokuwa unaheshimika humu, siamini kama ndio wewe unaedharaulika kiasi hiki.

Yaani umekuwa wa hovyo kabisaaa. Heshima yote uliyojijengea umeamua kuitupa msalani...kwa lugha ya mtaani wanasema umefulia.
 
Ni kwa sababu ya kuachana na kile alichokiamini na kukipigania kwa miaka mingi kwa hali na mali katika kutetea maslahi ya Tanzania na Watanzania, leo kaamua kuwa upande mmoja na wakurupukaji na madikteta ni lazima achuje.

Mwanakijiji umechuja sana. Sijui kwa nini!!!
 
Back
Top Bottom