Utawala huu Unafalsafa ya Kuendeleza Vitu na Si Watu.

Utawala huu Unafalsafa ya Kuendeleza Vitu na Si Watu.

Shebbydo

JF-Expert Member
Joined
Feb 12, 2015
Posts
1,176
Reaction score
1,939
Habari, Wana Jf

Naanza kwa kumkumbuka Muasisi wa taifa hili hayati Baba wa Taifa Mwalimu JK Nyerere ambaye aliridhia kutumia hata uchumi wetu kwa ajili ya kuwakomboa Waafrika wenzetu kusini mwa Afrika. Kilichomsukuma Mwalimu ni ubinadamu. Hakuwa na furaha ya kuona Tanzania ikipepea kimaendeleo ilihali Wazimbabwe wakiendelea kukandamizwa na utawala dhalimu. Hakuwa tayari kuendelea kusikia vilio vya Waafrika wenzetu huko Afrika kusini vilivyotokana na ukatili wa Makaburu. Ni kwa sababu tu aliamini katika ubinadamu, alipenda binadamu waendelee kuliko vitu viendelee.

Lakini leo hii taifa hili lina viongozi wa aina ya kipekee. Viongozi ambao wapo tayari kuwaona vijana wa Kitanzania wakihangaika ambao wamesoma katika mazingira ya shida ya shule zisizokuwa na walimu wa kutosha. Shule zisizokuwa na vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Lakini wamepambana kwa kudesa hadi wamefikia kuwa na sifa za kujiunga na elimu ya juu, wakiamini kuwa elimu ndiyo silaha pekee ambayo itawapa ushindi katika "mapambano dhidi ya mazingira" katika ulimwengu wa zama za sayansi na teknolojia. Leo kijana kafika chuo kikuu lakini anakutana na changamoto za mkopo unaotolewa na serikali yake uliojaa vigezo na masharti zaidi hata ya ule wa mfanyabiashara anapotaka kukopa taasisi ya fedha. Mkopo wenye masharti ambayo yanawagawa wanafunzi katika mafungu kama nyanya. Ukiuliza tatizo ni nini hawataki kusema jibu sahihi kuwa serikali haina pesa za kutosha kuwasomesha vijana wote wa elimu ya juu. Wanatoa maelezo yasiyokuwa na jibu la moja kwa moja eti mkopo huo watapata wenye vigezo. Laiti kama kungekuwa na pesa ya kutosha kungekuwa na vigezo gani zaidi ya mwanafunzi kuwa amepata nafasi ya kujiunga na elimu ya juu? Ni mjinga gani ambaye ana uwezo wa kujisomesha lakini leo hii abaki akizunguka katika ofisi za bodi ya mkopo ilihali ameshindwa kufanya usajili katika chuo alichochaguliwa? Kwa nini msiwe wakweli kwa kusema bajeti ya bodi ya mkopo ni "limited" hivyo siyo wote wanaweza kupata mkopo? Watanzania wakakaa wakijua wazi kuwa nchi yao haina uwezo wa kuwasomesha japo ina neema ya mito, maziwa, bahari, mbuga za wanyama, mlima mrefu kupita yote Afrika na madini ya kila namna hadi yale yasiyopatikana nchi yoyote duniani.

Katika kutafakari kwangu nagundua jambo jipya, nalo ni vipao mbele. Utawala huu unajali vitu kuliko watu. Upo tayari kuona Watanzania wanakufa kwa tauni lakini ukajenga madaraja marefu yanayopita angani. Utawala huu upo tayari kuona Wananchi wake wanakosa elimu ambayo itasaidia kuindeleza jamii kwa ujumla lakini ukanunua vitu ambavyo vinatakiwa kuja kuendeshwa na Watanzania walio na elimu. Je, kama Watanzania hawatakuwa na elimu ya kuviongoza vitu hivyo na nani atawaongozea? Au watabaki kuwa wapagazi katika nchi yao.

Namalizia na msemo huu, kupanga ni kuchagua. Ukiwa na shilingi laki moja nyumbani kwako ukaamua kununua baiskeli ili ikurahisishie safari zako, ukaacha kumsomesha mwanao, fahamu kwamba huyo mwanao atakuwa mzigo kwako. Siku moja atapanga kukuua ili arithi hiyo baiskeli. Laiti ungelimsomesha akaja kujitegemea, angekununulia gari katika uzee wako ambao huwezi tena kuendesha baiskeli.
 
nimenasa vitu muhimu hapo kwaajili ya kunufaisha familia!!!!! upo sahihi kwani hii Tz imenunua vitu vya samani ndani ya mwaka mmoja ila imeshindwa kusomesha watoto wake nazan ni uhamisho wa Elimu bure!
 
Back
Top Bottom