Utatu Mtakatifu (Riwaya)

BEKA MFAUME

New Member
Jan 27, 2022
1
2
UTATU ‘MTAKATIFU’

The Gangsters​

HAROLD Jeff, aliacha ghafla kumsikiliza mtu aliyezungumza naye. Alifanya hivyo baada ya kumwona mwanamume aliyekuwa ametoka kwenye lifti iliyopo ndani ya hoteli aliyokuwamo. Akajiuliza, alishawahi kuonana naye wapi mtu huyo? Wakati akijiuliza, alikuwa amekaa kwenye kochi lililotazamana na mtu aliyekuwa anazungumza naye. Walikuwa wamekaa katika sebule ya mapokezi ndani ya hoteli nzuri yenye hadhi ya kimataifa iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Akiwa ameacha kumpatiliza mwenyeji wake aliyepanga ndani ya hoteli hiyo, macho ya Jeff yakawa sambamba kuufuata mwelekeo wa mtu aliyetoka kwenye lifti. Akamwona akielekea mlango wa kutokea nje ya hoteli.

Mtu huyo mwembamba, mrefu, mkakamavu, mwenye nywele fupi, aliyevaa miwani meusi ya jua, fulana ya kuchezea gofu yenye rangi ya kijivu na jinzi ya bluu ambayo haikukolea rangi pamoja na viatu vya ngozi vilivyokuwa na soli isiyo na kisigino, alitembea kwa mwendo wa haraka usioweza kumfanya mtu mwingine yeyote anayemwangalia kumtilia wasiwasi. Akaupita mlango wa kioo uliojifungua wenyewe na kutoka nje ya hoteli.

Mtu aliyekuwa akizungumza na Harold Jeff baada ya kugundua Jeff hayupo naye kimazungumzo, akaacha kuendelea kuzungumza. Akaungana na macho ya Harold kuangalia yalipokuwa yakiangalia. Akamwona mtu aliyekuwa akitazamwa na Harold akimalizia kutoka nje ya hoteli na wakati huohuo mlango mkubwa wa kioo uliokuwa umejifungua, ukijifunga nyuma yake.

“Naomba unisubiri!” Harold Jeff alisema kwa haraka kumwambia mwenyeji wake huku akiinuka. Alishamtambua mtu huyo! Akaufuata mlango uleule aliotokea mtu aliyekuwa akimwangalia.

Kasi aliyotoka nayo Jeff, alitarajia kumwona mtu huyo akiwa hajafika popote huko nje. Aliamini angemkuta analifuata gari kwenye uwanja wa kuegesha magari uliopo nje ya hoteli. Na endapo atakuwa hana usafiri wa kuondoka nao, bado aliamini angemkuta akitembea kukatisha eneo la nje ya hoteli kuifuata njia inayoelekea barabarani.

Akashangaa alipokosa kumwona baada ya kutoka nje. Hakuamini! Ikawa kama aliyekwenda kukikabili kinyamkela kilichoyeyuka ghafla katika anga iliyokuwa wazi!

Harold akajishika kiuno katika kustaajabu kwake. Hakuamini kama ni kweli mtu aliyemfuata alikuwa haonekani! Akajipa imani, huenda ameingia ndani ya moja ya magari yaliyoegeshwa hapo nje ya hoteli. Hata hivyo, imani hiyo ilikuwa haba. Ikawa haimsukumi kuamini kama aliweza kuyafikia magari hayo na kuwahi kuingia bila kumwona. Alikimbia? alijiuliza.

Akaamua naye akimbie kuelekea yalipo magari hayo kama kubahatisha. Alipoyafikia, akapunguza kasi. Akawa anatembea kwa haraka kichwa amekiinua juu kuangalia pande tofauti kwa wakati mmoja kama mtu anayehaha. Akawa na matarajio ya kusikia ngurumo ya gari linalowashwa likiwa na mtu huyo.

Hakuisikia! Badala yake akawa anasikia mivumo ya magari yanayopita barabarani na honi za hapa na pale zikipigwa.

Akiwa amesimama katika hali ya kukata tamaa na aliyekosa uamuzi wa nini afanye, zikapita sekunde kadhaa pasipo kuona hata mtu mmoja akija katika eneo hilo. Ukimya uliokuwapo, ukamfanya achezwe na machale baada ya kuingiwa na hisia, huenda mtu huyo yupo katika eneo hilo akiwa anamwangalia!

Kuchezwa na machale akiwa ni ofisa wa ngazi ya kati katika Jeshi la Polisi, kukamuweka katika hadhari ya juu. Akajionya, kama ni kweli mtu huyo atakuwa anamwangalia kama hisia zake zinavyomhadharisha, basi kutakuwa na maana moja; mtu huyo amejificha! Na kama atakuwa amejificha, basi kwa maana ya pili; atakuwa ameshagundua anafuatwa!

Jeff akahisi tembe za jasho zikiumuka mwilini. Hali hiyo ikampa taharuki. Ilikuwa ni dalili ya woga! Lakini pia, akatambua, ilikuwa ni dalili ya hatari kwake! Papohapo akajipa hadhari, chochote kinaweza kikamtokea!

Taratibu na kwa umakini, akaanza kuzungusha macho yaliyojaa hadhari kama anayetarajia kufanyiwa shambulizi la kushtukiza. Mkono wake wa kulia ukawa unanyemelea nyuma ya kiuno kuifuata bastola aliyokuwa ameihifadhi kwenye ala yenye gamba gumu. Akawa amejiandaa kujibu shambulizi lolote la kushtukiza.

Kilichompa wakati mgumu ni kutojua adui yuko upande gani. Hali hiyo ikamkosesha amani. Alikuwa akimjua vyema mtu aliyemfuata hapo. Ni mtu hatari kuliko nyoka aina ya swila mwenye hasira! Kwa kujua anakabiliana na mtu hatari wa aina hiyo, tena mwenye kujua anafuatwa, Jeff alikiri anahitaji msaada. Mtu huyo hakuwa ni aina ya mtu anayeweza kucheza naye akiwa peke yake!

Wazo la kuwapigia simu wenzake likamjia kichwani. Alihitaji msaada wa wenzake! Hata hivyo akajionya. Alijua endapo atasikiwa na mtu huyo akiomba msaada wa wenzake waje hapo, mtu huyo ataanza na yeye kabla ya wenzake hao hawajafika!

Harold Jeff akawa mpole. Akaamua kuondoka katika eneo hilo kwa usalama wake. Akaelekea tena hotelini ambako aliamini angeweza kuwasiliana kwa simu na mkuu wake wa kazi na kuripoti tukio la kumwona mtu huyo. Kabla hata ya kuufikia mlango wa kuingia hotelini, akatoa simu ya kiganjani na kuanza kupiga.

Simu ya upande wa pili ikaanza kuita. Akiwa na matarajio ya kupokewa na mtu anayempigia, ghafla akalisikia gari linaloondoka kwa kasi nyuma yake. Matairi ya gari hilo yakawa yanalalama kwenye lami kama mbwa aliyetishiwa uhai. Akageuka haraka kuangalia. Akaliona gari dogo lililokuwa limetoka kwa kasi eneo la maegesho, likielekea barabarani.

Ni yeye! aliwaza.

****​

“Excuse me!” Jeff aliisikia sauti ya mwanamke yenye lafidhi ya kigeni ikitoka nyuma yake. Alipogeuka, akamwona mwanamke wa Kizungu aliyekuwa anatoka hotelini akiwa amesimama nyuma yake akimwomba nafasi ya kupita.

“Oh, I’m sorry,” Jeff alisema huku akikurupuka kumpisha.

Baada ya mwanamke huyo kupita, Jeff akakumbuka simu aliyokuwa ameipiga. Alipoiangalia kiganjani kwake, akaiona haipo tena hewani. Akampigia tena mkuu wake. Ikachukua sekunde kadhaa kuita bila kupokewa. Alipohisi ingekatika kabla ya kupokewa, akaisikia sauti ya Kareem ambaye ni bosi wake akisema, “Haloh, Jeff.”

“Afande,” Jeff alisema kwenye simu. “Leno yupo Dar!”

****​

Nusu saa iliyopita katika hoteli hiyo, mhudumu wa vyakula na vinywaji chumbani au kwa jina la kigeni, Room service waiter ambaye alikuwa amepokea simu ya mteja anayehitaji huduma ya kitafunwa cha toasted chicken sandwiches na kinywaji apelekewe katika chumbachake namba 430, akawa tayari amefika na mahitaji hayo kwenye chumba hicho.

Akagonga mlango huku akiiangalia namba 430 usoni kwake. Mkononi alikuwa amebeba trei yenye vitu alivyoagizwa. Akashangaa kuuona mlango anaougonga ukijifungua wenyewe taratibu na kuacha uwazi wa inchi moja. Haujafungwa! alishangaa.

Kwenye trei, pamoja na kubeba sandwiches, vingine vilikuwa chupa nzima ya kileo cha aina ya Bacard Rum, glasi moja tupu yenye nembo ya pombe hiyo na buli dogo lenye vipande vya barafu na kijiko maalum cha kuchukulia barafu.

Baada ya kuuona mlango wa chumbani uko wazi, mhudumu huyo akajengwa na dhana, huenda mteja mwenye chumba ameuacha mlango wazi kwa kukusudia ili atakapofika na huduma aliyoagizwa, aweze kuingia nayo moja kwa moja.

Hata hivyo, asingeweza kuingia ndani bila kukaribishwa. Akausukuma mlango ili kuongeza uwazi utakaowezesha sauti yake kufika ndani wakati wa kupiga hodi ili aweze kuruhusiwa kuingia.

“Halooh!” alitamka kwa kulivuta neno hilo huku akiusukuma mlango kwa nidhamu. Mlango ukajifungua kwa uhuru na kuongeza upenyo wa uwazi wa inchi chache kuweza kukiona chumba kwa ndani. Kisha mlango ukagoma kuendelea kufunguka. Mhudumu akahisi huenda mteja mwenye chumba aliweka kizuizi ndani ya mlango ili usijifungue na kubaki wazi muda wote.

Akatumia nguvu kidogo kujaribu kuusukuma. Ukasogea kwa ugumu na kuongeza upenyo wa sentimita chache. Akatumbukiza kichwa chumbani kama anayechungulia kwa dhamira ya kupiga tena hodi. Akaishia tu kutamka neno, “Ho…”

Hakuendelea!

Alikuwa ameiona miguu ya mtu chumbani! Ilikuwa imelala sakafuni ikiwa juu ya busati. Ikawa inazuia mlango usifunguke. Akatumbukiza kichwa zaidi ndani. Akamwona vizuri mtu huyo. Na akatambua, alikuwa akiuangalia mwili wa mtu aliyeuawa!



****​

Ilibakia kidogo aliangushe trei lililokuwa mikononi kwake kwa kihoro. Paji la mtu aliyelala humo chumbani lilikuwa na tundu lililokuwa likivuja damu iliyosambaa kwenye busati. Ilishaanza kuingia weusi kutokana na kuanza kuganda.

Mhudumu akajiondoa pale mlangoni kwa kurudi kinyumenyume huku miguu yake ikinyata kama vile sehemu anayoikanyaga ilitegwa mabomu. Akiwa na hadhari aliyoanza kujipa kuwa awe makini na vidole vyake vya mikono visiguse mlango au eneo jingine lolote la hapo, akaangalia nyuma kwa haraka kama vile alitarajia angemwona mtu anayekuja.

Akaitoa chupa yenye kileo kutoka kwenye trei na kuishika vyema mkononi kwake kwa ajili ya usalama ili isianguke na kuvunjika. Kisha akafyatuka kutoka alipokuwa. Akakimbia kuelekea kwenye lifti! Alipoifikia akabonyeza kitufe cha kuifanya lifti ije katika ghorofa aliyokuwapo. Ikamwonesha lifti ipo ghorofa ya nane wakati akiisubiri. Akageuka nyuma kuangalia kama vile usalama wake ulikuwa hatarini. Akili haikumpa uvumilivu wa kuisubiri lifti ifike. Akachukua uamuzi wa haraka usiojiuliza mara mbili.

Akaifuata ngazi iliyokuwa jirani ambayo inatumika kwa dharura pindi lifti zikiwa hazifanyi kazi. Akateremka nayo kwa kasi hadi ghorofa iliyofuata. Huko nako hakusimama! Chupa ya kileo ikiwa imeshikwa na mkono mmoja huku mwingine ukiwa umeikamata trei iliyobeba baadhi ya vitu alivyoagizwa, mhudumu huyo aliendelea kukimbia kuteremka na ngazi hiyo hadi chini.



****​

Harold Jeff alirudi alipokuwa amemwacha mwenyeji wake. Akakaa bila kugusia kilichokuwa kimemtoa nje. Akamtaka mwenyeji wake aendelee na mazungumzo waliyokuwa wameyasimamisha. Hata hivyo, pamoja na mwenyeji wake kuendelea na maongezi, Jeff ilibidi ajilazimishe kuonesha anamsikiliza.

Akili yake haikuwa tena kwenye mazungumzo yaliyokuwa yamemleta hapo hotelini. Kugundua uwepo wa Leno kuwa yupo jijini, kulimpa wakati mgumu. Na kule kumwona akitoka kwenye hoteli hiyo kuliiyumbisha akili yake. Hakuamini kama atakuwa amepanga kwenye hoteli hiyo. Aliamini, Leno hakuwa mtu wa kuishi kwenye hoteli zenye shughuli nyingi na za bei ghali kama hiyo.

Hakuwa mtu wa kuhitaji starehe kiasi cha kukaa kwenye hoteli za kifahari. Muda wote alikuwa mbioni, asiyependa kuonekana au kuchanganyika na watu wengine. Kwa muda wote Jeff akawa anajiuliza, Leno ametoka kumwona nani katika hoteli hiyo?

Akili yake haikupata utulivu. Alihitaji kupata jibu, Leno alikuja kufanya nini katika hoteli hiyo? Akaamua kumkatisha mwenyeji wake aliyekuwa akizungumza. “Naomba radhi kidogo,” alisema huku viganja vyake vikiwa vimejikita magotini. “Nina shida ya dharura na mapokezi.”

Baada ya kusema hivyo alivikita zaidi viganja vyake magotini na kusimama. Akaelekea mapokezi.

Alimkuta msichana mrembo, mwembamba aliyestahili kuwapo katika idara hiyo. Na pengine ni uzuri wake ndio uliomfanya awekwe sehemu hiyo.

“Karibu,” msichana huyo alisema baada ya kumwona Jeff akiikaribia meza ya mapokezi. “Nikusaidie nini?”

Jeff akatoa kitambulisho chake cha kazi na kukionesha. Aliamini kujitambulisha kwamba yeye ni ofisa wa polisi kungefanya apate ushirikiano wa haraka. “Kuna mtu ametoka kwenye lifti kama dakika kumi zilizopita…” alianza kusema, lakini akasita kuendelea baada ya kumwona mfanyakazi wa hoteli mwenye sare za uhudumu wa vyakula na vinywaji akiwasili mapokezi kwa taharuki.

“Chumba namba mia nne thelathini kuna mtu ameuawa!” mfanyakazi huyo alimwambia msichana aliyekuwa akizungumza na Jeff.

Jeff akalazimika kuwa mpole. Akatulia na kumwangalia mfanyakazi huyo aliyekuwa amemtoa msichana wa mapokezi kwenye mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea kati yao.

“Niwie radhi kidogo,” msichana wa mapokezi alimwambia Jeff.

“Usijali, endelea,” Jeff alisema huku akiwa makini usoni.

Msichana akamgeukia mhudumu wa vyakula wa vyumbani. “Umesema chumba namba mia nne thelathini kuna nini?”

“Mteja wa chumba hicho ameuawa!” mhudumu huyo ambaye trei yake yake vitu alivyokuwa amevibeba vikiwa juu ya kaunta ya mapokezi alisema huku akionekana hajaondokwa na taharuki. “Nilikuwa…”

“Subiri kwanza!” msichana wa mapokezi alimkatisha mhudumu huyo. Akainua simu kutoka juu ya kaunta na kupiga. Baadaye akasema kwa sauti ya chini, “Security, kuna matatizo chumbani, naomba uje haraka hapa mapokezi!”



****​

Dakika kumi baadaye, Jeff akiwa na mawasiliano ya simu na Kareem, alisema, “Leno ameshaua hapa hotelini. Safari hii amemuua IGP!”



RIWAYA HII INAENDELEA KATIKA KITABU KIPYA CHA UTATU ‘MTAKATIFU’ KILICHOANDIKWA NA GWIJI WA UANDISHI WA RIWAYA NCHINI TANZANIA – BEKA MFAUME.

KAKINUNUE KATIKA DUKA LA TPH MTAA WA SAMORA.

GEORGE, JIRANI NA MZUNGUKO WA SANAMU LA ASKARI MTAA WA SAMORA.

DUKA LA KONA YA RIWAYA LILILOPO NYUMA YA JENGO LA AIRTEL KINONDONI BLOCK 41.

MWANZA, MBEYA, ARUSHA NI WIKIENDI HII.
au wasiliana naye kwa simu no. 0754893247
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom