UTATA wa Magazeti ya Mtanzania na Habari leo, juu ya Elimu ya bure Tanzania, Je upi Mtazamo wako?

Dr Matola PhD

JF-Expert Member
Oct 18, 2010
59,506
103,168
Mtanzania.JPG

ELIMU BURE IMEKWAMA – HAKIELIMU

MPANGO wa Serikali kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ulioanza kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka jana, umeshindwa kufanikiwa kutokana na changamoto mbalimbali.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya HakiElimu kuhusu utekelezaji wa mpango wa elimu bure, umebaini sababu kadhaa ikiwamo fedha za ruzuku kutofika shuleni kwa wakati na kutozingatia idadi ya wanafunzi kama ilivyotarajiwa.

Akizindua utafiti huo Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa HakiElimu, John Kalage, alisema uchambuzi wa matokeo unaonyesha kuwa baadhi ya shule zenye wanafunzi wachache zinapata fedha zaidi kuliko shule zenye wanafunzi wengi.

Akitolea mfano alisema Shule ya Msingi Mulemba iliyopo Muleba mkoani Kagera yenye wanafunzi 828, ilipokea Sh 3,918,000 ilhali Shule ya Ilolo iliyopo Mpwapwa mkoani Dodoma yenye wanafunzi 874, ilipokea Sh 3,400,000.

Alifafanua kuwa kabla ya utekelezaji wa mpango wa elimu bure uliowaelekeza wazazi kutotoa michango mingine ya shule na kupiga marufuku masomo ya ziada katika waraka wa elimu namba tano wa mwaka juzi, pia shule za msingi zilipaswa kupata kiasi cha Sh 10,000 na sekondari Sh 25,000 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka kwa uendeshaji wa shule, ununuzi wa vitabu, vifaa vya mitihani na ukarabati.

“Asilimia 40 ya ruzuku kwa shule za msingi na asilimia 50 kwa shule za sekondari inapaswa kubaki Tawala za Mikoa kwa ununuzi wa vitabu, asilimia 60 kwa shule za msingi na asilimia 50 kwa shule za sekondari, inayobaki kupelekwa moja kwa moja shuleni kugharamia ukaratabi, vifaa, mitihani, utawala na michezo.

“Utafiti unaonyesha kuwa katika kipindi cha Januari hadi Juni, mwaka jana, Serikali ilipaswa kupeleka kiasi cha shilingi 3,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi, lakini ilipeleka wastani wa shilingi 2,700 ambayo ni sawa na asilimia 93 na kupeleka ruzuku kwa sekondari kwa wastani wa asilimia 100,’’ alisema.

Kalage alisema shule zenye wanafunzi wachache kati ya 200 hadi 300 zinapata wastani wa Sh 100,000 hadi 150,000 kwa mwezi na haziwezi kutatua matatizo ya msingi ikizingatiwa ruzuku zinatumwa shuleni kila mwezi, huku walimu wakishindwa kutatua changamoto hiyo.

Pia alisema ruzuku zinazopelekwa shuleni hazikidhi mahitaji ya shule na hiyo imedhihirika kutoka kwa walimu wakuu 95, kwamba fedha wanazozipata hazitoshi kukidhi mahitaji mbalimbali.

Kalage alisema hata baada ya kuanza kutekelezwa kwa mpango wa elimu bure, wazazi bado waliendelea kubanwa kwa kuchangishwa gharama mbalimbali za uendeshaji wa shule kwa watoto.

Alizitaja gharama hizo kuwa ni pamoja na zile za kulipa walinzi, kujenga madarasa na kulipa wapishi na hiyo ilitegemea na wazazi wenyewe kwa kuwa wengine wanachanga na wengine hawachangi.

“Hii inahusishwa moja kwa moja na matokeo ya utafiti kuhusu uelewa wa wazazi kwenye namna ya elimu bila malipo, kwa sababu asilimia 51.3 ya wazazi wanaelewa kuwa elimu bila malipo maana yake wazazi kutochangia gharama zozote za elimu ya watoto wao katika shule za umma,’’ alieleza.

Kalage aliendelea kusema kuwa mpango wa elimu bure umesababisha ongezeko la wanafunzi wa darasa la kwanza hasa kwa shule za msingi ambapo kuna ongezeko la asilimia 43 na asilimia 10 kwa shule za sekondari.

Pia alisema elimu bure imesababisha walimu kuelemewa kwa kuwa awali ilikuwa kwa wastani mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 45, lakini kwa sasa mmoja anafundisha wanafunzi 164.

MAONI YA WADAU WA ELIMU

Mchambuzi wa masuala ya kijamii, Jenerali Ulimwengu, akichangia katika uzinduzi wa utafiri huo, alisema kuwa huwezi ukatenganisha suala la elimu na siasa kwa kuwa chimbuko la elimu bure lilianzia katika kampeni za siasa.

Alisema anashangaa Rais Dk. John Magufuli kukataza kuendelea na mikutano ya siasa hadi hapo mwaka 2020 wakati ingekuwa muda mwafaka kuweza kuendelea kukosoa kutoa mawazo na kuchangia hilo.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Bashiru Ally, alisema elimu ni gharama, hivyo kila mwanachi mwenye uwezo kwa kushirikiana na Serikali anatakiwa kuwekeza katika elimu.

Chanzo: Mtanzania

Gazeti la habari leo, limekuja na mtazamo tofauti...

Habari Leo.JPG


Mpango wa elimu bure wafanikiwa 100%

TAASISI ya HakiElimu imeipongeza serikali kwa jitihada zake za kuhakikisha ruzuku zinazopelekwa shuleni kwa ajili ya wanafunzi kutekeleza sera ya elimu bure katika shule za msingi imefika asilimia 93 huku kwa shule za sekondari zikipata ruzuku zaidi ya matarajio kwa asilimia 15.

Aidha, imeeleza kuwa kumekuwapo na changamoto kadhaa katika utekelezaji wa sera hiyo iliyoanza mwanzoni mwa mwaka huu, ikiwamo kushindwa kueleweka kwa wadau wa elimu na hata kwa wazazi ambapo asilimia 45 ya walimu wakuu waliamini gharama zote za shule zingelipwa na serikali.

Akizungumza katika uzinduzi wa ripoti ya utafiti kuhusu elimu bure jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, John Kalage alisema utafiti huo ulifanyika katika wilaya za Mpwapwa, Njombe, Sumbawanga, Kilosa, Korogwe, Tabora Mjini na Muleba ukihusisha shule 28 za msingi na 28 za sekondari.

Kalage alisema wahusika wakuu katika utafiti huo ni walimu wakuu na wakuu wa shule, wazazi pamoja na walimu ambapo washiriki 910 walifikiwa.

Kuhusu ruzuku kwa wanafunzi, alisema kabla ya utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo, shule za msingi zilipaswa kupata Sh 10,000 na sekondari Sh 25,000 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka kwa ajili ya uendeshaji wa shule, ununuzi wa vitabu, ununuzi wa vifaa vya mitihani na ukarabati wa shule.

Alisema utafiti umebaini katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka jana, serikali ilipaswa kupeleka Sh 3,000 kwa shule za msingi, lakini ilipeleka wastani wa Sh 2,789 kwa shule za msingi sawa na asilimia 93 huku kwa shule za sekondari ikipeleka kwa wastani wa asilimia 100.

Hata hivyo, alisema licha ya jitihada za kupeleka ruzuku kufanikiwa, lakini ruzuku inayopelekwa katika shule haitoshi kukidhi mahitaji ya shule ambapo asilimia 95 ya walimu wakuu waliohojiwa walikiri kuwa fedha hiyo haitoshi kwa ajili ya kukidhi manunuzi mbalimbali.

Aliongeza kuwa hata baada ya kuanza kutekelezwa kwa sera ya elimu bila malipo, mzazi bado anaendelea kuchangia gharama mbalimbali za uendeshaji wa shule kwa ajili ya watoto ambapo kila wazazi wawili waliohojiwa mmojawapo ameshachangia michango mbalimbali ya shule.

Alibainisha kuwa matokeo ya utafiti huo uliofanywa kwa kipindi kilichoanzia Januari hadi Juni, 2016, Dk Richard Shukia alisema katika walimu wakuu wa shule za msingi waliohojiwa kuhusu elimu bure, asilimia 23 walisema ni ile elimu inahusisha kutokutolewa kwa ada peke yake huku asilimia 32 ya wazazi wakiendelea kuchangia elimu.

Hata hivyo, alieleza kuwa sera hiyo imesababisha kuwepo kwa msongamano madarasani na pia kuongezeka kwa uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi kwa darasa la kwanza hadi kufikia mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi 164 ka wastani badala ya wanafunzi 45 wanaotakiwa.

Chanzo: Habari leo
 
Matola bwana pole.

Maana umenikumbusha Mtaa mmoja Mbeya anaitwa kwa Binti Matola,huyu mama alisaidia sana Kwenye kuleta Uhuru Mkoa wa Mbeya. Sijui kama leo bado tuna akina Binti Matola maana hata mie sijui kama Nina uwezo wa kujitoa kwa ajili ya Nchi yangu hata kwa kutoogopa kifo.

Sasa huyo wa Juu ni wale tulio nategemea wawe akina Binti Matola wa leo lakini wanaitwa watoto wa Tumbo.Hao ni Tumbo kwanza Taifa baadaye.

Hakuna akina Binti Matola na akina Bin Matola yaani watoto waliorithi ubinti Matola ni Lema na Lissu wengine sijui.
 
siku hiz kabla yakusoma habar lazima ujiulize kwanza imeandikwa na nan na ipo gazet gan...la sivyo unaingia chaka!!
 
Matola bwana pole.Maana umenikumbusha Mtaa mmoja Mbeya anaitwa kwa Binti Matola,huyu mama alisaidia sana Kwenye kuleta Uhuru Mkoa wa Mbeya.Sijui kama leo bado tuna akina Binti Matola maana hata mie sijui kama Nina uwezo wa kujitoa kwa ajili ya Nchi yangu hata kwa kutoogopa kifo.

Sasa huyo wa Juu ni wale tulio nategemea wawe akina Binti Matola wa leo lakini wanaitwa watoto wa Tumbo.Hao ni Tumbo kwanza Taifa baadaye.

Hakuna akina Binti Matola na akina Bin Matola yaani watoto waliorithi ubinti Matola ni Lema na Lissu wengine sijui.
UHURU? Mkoani? MBEYA? LILIKUA KOLONI LA MZUNGU WA TAIFA LIPI?
 
Halafu tukienda kwa watafiti wakatwambia ukweli, lile gazeti linalosema uongo lifungiwe...
 
Back
Top Bottom