USONI KWA OKWI NA NYUSO NYINGINE MBILI

Jospina

JF-Expert Member
Apr 19, 2013
2,421
1,387
-Siku Tanzania inacheza na Uganda kwenye pambano lililo ishuhudia Taifa Stars ikiungana na Cranes kwenye safari ya Misri kuna kitu niliwaeleza watu niliotazama nao pambano hilo.

-Niliwaambia kuwa iwapo Emmanuel Okwi atapangwa ni wazi atakuwa kwenye wakati mgumu sana, mimi huwa ninasema Okwi ni mtanzania mwenzetu kwa sababu amekuja Tanzania akiwa mdogo ana marafiki wengi tu na wengine wala si mashabiki wala wachezaji wa Simba.

-Ametengeneza maisha akiwa hapa, akigeuka nyuma kuangalia mali zake pengine anaona kabisa baadhi hazihusiani na mshahara wake bali ni zawadi toka kwa rafiki zake wa kitanzania, kama ni hivyo unatarajia angepata wapi nguvu za kuishambulia Stars na kufunga katika mechi ambayo haikuwa na umuhimu wowote kwa taifa lake la kwanza Uganda?

-Hata kama angeamua kucheza kwa nguvu bado akili na mwili vingekosa ushirikiano. Maisha waliyompa Simba tangia anatua hapa Tanzania inawezekana ndio yaliyomfanya ashindwe kucheza Afrika ya Kaskazini na Ulaya au hata Yanga aliporejea nchini.

-Amekuwa akipewa “first class treatment” ndani ya klabu yake huku na yeye akilipa fadhila uwanjani. Unakumbuka kisa cha Amisi Tambwe kutemwa Simba? Inasemekana ni ile safari ya Mtwara ambapo timu ilisafiri kwa basi isipokuwa Okwi tu ndio alikatiwa tiketi ya ndege. Kuna taarifa kuwa Tambwe alilalamikia kitendo hiki na hivyo kuwaudhi vigogo wa Simba wakati huo, mwisho wa yote Tambwe alitemwa ilikuondoa uchochezi dhidi ya kipenzi chao.

-Siku za karibuni inaelekea maisha yamebadilika ndani ya Simba, Okwi haoni kama anathaminiwa tena kama zamani ulipokuja uvumi wa kutakiwa Afrika Kusini inawezekana alitarajia hekaheka za uongozi kuhakikisha wanambakiza lakini haikuwa hivyo.

-Kwa sasa tunasikia majina mbalimbali yakitajwa kuja kuchukua nafasi yake. Yote haya yanamuondolea furaha,hata kama alikuwa “injured” lakini ni wazi hana furaha pia anahitaji kuwekwa sawa kisaikolojia. kwa umri wake sidhani kama bado anahamu sana ya kwenda kucheza soka nje ya Tanzania.

-Hata huko kutakiwa Kusini inawezekana ni kitu kilichotengenezwa tu ilikujiongezea mshahara au ukubwa wa “signing fee” iwapo mkataba unaelekea ukingoni lakini mambo yanazidi kwenda tofauti. Anaona ufalme wake unamomonyoka kwa kasi, anaona kuna nyota wengine wanaoimbwa sana kuliko yeye.

-Asipopata washauri wazuri anaweza kupotea kabisa kwani si rahisi kuurejesha ule ufalme wake wa miaka mingi kwa sura ile ile. Anatakiwa atumie ule msemo kwa Kiingereza unaomtaka mtu kujitathmini na kuanza upya mambo yanapokwenda tofauti yaani “Walking into a new beginning,” inawezekana Haruna Niyonzima ameufanyiakazi msemo huu.

-Simba SC inatakiwa iimarishe kitengo chake cha saikolojia kwa sababu kuna mengi yamekuwa yanatokea ambayo yanaashiria uwepo wa tatizo fulani. Mtazame Paul Bukaba, anaonekana siku hizi hana furaha kabisa na anazidi kupoteza kujiamini. Kuna mechi fulani ya hivi karibuni alifunga goli muhimu sana lakini hakuonesha furaha yoyote ukilinganisha na siku za nyuma huu ni ujumbe.

-Inawezekana anahofia hatma yake ndani ya kikosi cha Simba kufuatia makosa fulani fulani ambayo amekuwa anafanya kwenye mechi za hivi karibuni au kuna kauli amekuwa anatamkiwa au kusikia kupitia watu.

-Hata Juuko Murshid wa The Cranes huwa amechangamka kuliko huyu wa Simba, anahitaji kupata watu wa kumuonesha thamani yake ndani ya kikosi iliarejeshe furaha kikosini. Yusuf Mlipili na Mohamed Ibrahim pia kwa nyakati tofauti wamewahi kupatwa na matatizo ya kisaikolojia kiasi cha kufikia kutoweka klabuni.

-Nimefuatilia na kugundua walikuwa na matatizo ya kimsingi. Kuna wachezaji wenye mioyo migumu inayohimili matatizo na misukosuko kama vile Jonas Mkude, alipitia wimbi zito lakini alibakia yule yule pasi rula.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom