Ushindi wa Lema, usigeuzwe ajenda ya CCM

MLUGO

Member
Dec 29, 2012
12
14
Ccm tumezoea sana kudandia, soma hii uone jinsi tunavyoweza kudandia vya wengine-attachmen
--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
USHINDI WA LEMA, USIGEUZWE AJENDA YA CCM .

NIMESHANGAZWA na wema wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya Mahakama ya Rufaa kumrejeshea ubunge, Godbless Lema, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini (CHADEMA).

Jambo ambalo limekuwa ni ajenda kwa CCM kuliko hata CHADEMA yenyewe. Mwanafalsafa mmoja nchini ambaye kwa sasa si lazima nimtaje, aliwahi kusema kuwa CCM ni chama kinachotaka kuendelea kutawala kila siku, ni chama kinachotaka zaidi madaraka bila kujua uwajibikaji na wajibu wale kwa wananchi. Ni chama ambacho hakikidhi mahitaji yake kwa wananchi wake, hivyo kwa kuwa wanajua lengo lao ni madaraka, wapo tayari kuahidi chochote, au kusema lolote ili waonekane wapo karibu na jamii, kiwe kinawahusu au hakiwahusu.

Ndiyo maana kinaposhindwa kutekeleza ahadi zake hukimbilia kwenye huruma ya wananchi kwa kufanya matukio ambayo si ya kisiasa kuwa ya kisiasa, mfano misiba, magonjwa, au hata sherehe.
Iliwahi kutokea siku moja Richard Bizubenhout kutoka Tanzania alishinda shindano la Big Brother Africa, baada tu ya kuwasili nchini, aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati, aliwahi na kusema ushindi wa Richard ulitokana na
utekelezaji mzuri wa sera za CCM.

Tunashindwa kuelewa kama wale wanaoshinda kutoka nchi mbalimbali kama wao kuna CCM, au sijui kama sera za CCM zinahusika vipi na suala la mashindano ya Big Brother. Binafsi sijui, nawaachia Watanzania mtafakari, pengine ni ilani ya chama hicho ndiyo iliyomfanya Mtanzania huyo kuibuka kidedea katika shindano hilo au la. Kwa mtiririko huo huo, na akili hizo hizo, siku chache zilizopita baada ya Mahakama ya Rufaa kumrejeshea ubunge, Lema chama hicho kimekuja na propaganda za kitoto zinazoenezwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho hicho, Nape Nnauye, na Naibu Katibu Mkuu Bara Mwigulu Nchemba.

Nitangaze mgongano wa kimaslahi kuwa Mwigulu Nchemba, ni kijana mdogo kutoka Singida kama mimi, ni mdogo kwa umri wangu, lakini pamoja na udogo huo sitegemei kuwa mambo madogo kama haya anashindwa kujua kuwa yanampotezea umaarufu
katika jamii na hususan katika siasa ambako amewekeza.
Nimebaini kuwa Watanzania tumefikia mahali tumechoshwa na propaganda za Nape na Mwigulu. Hata kama ni siasa, lakini vijana hawa sasa hawafanyi siasa, wanaendesha kwa propaganda za kijinga zaidi zinazoamsha hasira, wanaweza kuchangia kutokea
kwa vurugu.

Kwa suala la Lema kwa watu wenye akili timamu wangekaa kimya kabisa. Wasingejitokeza hata kulisemea. Linaumiza, linaamsha hasira mbaya kati ya wavuja jasho na wavuna jasho, linahusu uchumi wa nchi, linahusu upotevu wa rasilimali nyingi za nchi bila kuwepo sababu ya msingi.
Mwigulu anasema: "CHADEMA ni watu wa aina yao, waliposhindwa katika kesi Arusha walisema Ikulu imeingilia na majaji hawajui Kiingereza. Sasa leo wameshinda wanafurahi na kuona kwamba sasa majaji wanajua Kiingereza na hawakuigusa Ikulu
kwamba imeingilia, maana pale ilipotolewa hukumu umbali wake ni hatua chache na Ofisi ya Ikulu kuliko Arusha." Akamalizia kwa kusema hukumu hiyo inatokana na utawala bora wa serikali ya CCM.
Nimfundishe hapa kidogo, hukumu ya Lema kushinda, haiweki Kiingereza kwa majaji, Mwigulu pamoja na kutaka kupotosha hoja, maelezo ya Wakili Tundu Lissu kuhusu majaji kwa kifupi yalisema:

"Ibara 109 ya Katiba kipengele cha 6-8 kinasema; mtu anaweza kuwa jaji iwapo tu ana shahada ya sheria kutoka katika chuo kinachotambuliwa kisheria, awe ameshakuwa hakimu, awe ameshakuwa wakili na kusajiliwa na sifa zote hizo ziambatane na
utumishi wa miaka kumi mfululizo.

"Lakini sifa zote hizo lazima mtu anayeteuliwa kuwa jaji awe nazo kwa miaka 10 mfululizo. Sasa badala ya kuzungumzia masuala hayo kwa ujumla jumla, ningependa wanaonijibu watamke wazi wazi Jaji Mbaruku Salumu Mbaruku alisoma chuo kipi na akapata shahada ya sheria iliyompa sifa ya kuwa jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar kabla ya kuteuliwa kuwa jaji wa Mahakama ya Rufaa hadi sasa, hata Katiba ya Zanzibar 94 (3) inasema; ili mtu achaguliwe kuwa jaji, ni lazima awe na shahada ya chuo kikuu. "Huyu jaji ambaye anasoma sasa alipataje kuwa jaji kabla ya kuwa na shahada ambayo ndiyo sifa ya msingi?" . Hivi hapa Mwigulu Nchemba na Nape mnahitaji mwekezaji kuelewa hili?

Bila kuathiri propaganda zenu, ninaomba tu niwakumbushe wananchi waliosahau, au kuwajulisha wale ambao hawajui kuwa baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, CCM kupitia Katibu Mkuu wake wa wakati ule, Yusufu Makamba, waliandika barua yenye kumbukumbu namba CCM/OND/636/VOL.11/122 ya Novemba 9, 2010. Barua iliyokuwa inakwenda kwa makatibu wa CCM wa mikoa na wilaya kuwaamuru wote walioshindwa katika uchaguzi wapinge matokeo, na kwamba chama kingewasaidia gharama za uendeshaji wa kesi hizo.

Katika barua hiyo ambayo Mwanafalsafa ninayo nakala yake, Makamba aliwaagiza makatibu wa CCM wa mikoa kwa kushirikiana na makatibu wa wilaya na kata kuwasaidia wagombea walioshindwa kwenye uchaguzi kuandaa hoja za malalamiko na vielelezo kwa ajili ya kupeleka mahakamani.

Makamba kwa niaba ya chama alisisitiza kuwa: "Makao makuu itachangia gharama za mawakili kwa wagombea ambao hawana uwezo kifedha." Nape na Mwigulu utawala bora si unapaswa kuanzia ndani ya chama chenu mnachokiongoza? Inaonekana wazi kuwa masuala hayo yasiyokuwa ya msingi yalipitia hata kwa mwenyekiti wa chama hiki, na kukubali kupoteza pesa za Watanzania kwa
fikra ndogo za chama chenu.
Kuja muda huu kuwahubiria watu kuhusu utawala bora wakati taifa limepoteza na bado linapoteza pesa nyingi kwa kesi za uchaguzi, tabia hii isiyo ya kizalendo inaonesha kuwachokoza Watanzania.
Ni vema mkawasaidieni kwanza watu waliofungua kesi kwa kufuata ushauri wenu walipe madeni wanayodaiwa, Lema ameanza kutafuta madalali kunadi nyumba za waliomshitaki kwa kufuata ushauri wenu huu haramu.
Silinde anamsakama Dk. Siame hadi anamtangaza magazetini, mtu aliyewahi kuwa naibu waziri anajificha kwa kuogopa deni, kwa kuingizwa mkenge na Chama, Sugu anamsaka Mpesya hadi mkuu wa wilaya hafanyi kazi kwa utulivu, kisa anadaiwa madai ya kesi ya uchaguzi.

Waliofungua kesi kupinga matokeo ni wanachama wa CCM kwa maelekezo ya chama chenu, tena Mwigulu ukiwa mjumbe muhimu wa sekretarieti, wema wenu ulikuwa wapi au umeanza lini, mbona hamkushauriana ndani ya sekretarieti mkaandika barua ya kutoa maelekezo yasiyo na mashiko na tija kwa uchumi wa taifa?
Mlipomshauri mzee Makamba atume barua kwa makatibu na kuwaelekeza wanachama wenu kufungua kesi mlitarajia nini? Ndio utawala bora kwa mujibu wa akili za chama hicho?

Kama kweli serikali ya CCM inafuata utawala bora, mbona mlifanya sherehe Arusha baada ya jaji kutoa hukumu kinyume, na kuifanya kesi ije hadi Mahakama ya Rufaa pamoja na kushauriwa na mawakili wa CHADEMA kuwa kwa sheria za Tanzania wapiga kura wanapaswa kufungua kesi ikiwa haki zao tu ndizo zimeathiriwa na si kushitaki kwa niaba ya mgombea?
Je, Lema angerejeshewa ubunge wake bila mawakili wake kusimama kidete kutetea haki? Bahati nzuri ni kuwa yote mnayofanya, mnawafanyia Watanzania, ndugu zenu wanaona hayo hata hao watu mnaowafanyia hayo wana majirani, wana ndugu, wana
marafiki na wanapofika huko wanasimulia. Wanauliza huu ndio utawala bora tunaosimuliwa na CCM?
Wapo wanaojua kuwa mnachezea pesa huku wanafunzi wakikosa madarasa na wengine wanakaa chini, walimu hawajalipwa mishahara mizuri, na askari wanajua mnachezea hela, mnawacheleweshea posho zao, wanafunzi vyuo vikuu wanajua mnachezea pesa na wao hawapati mikopo kwa wakati, wengine hawapati kabisa. Propaganda ya kadi ya Dk. Slaa imekosa mashiko, sasa viongozi wa CCM wanakuja na hoja ya kuwa washauri wa Lema, au watoaji wa ufafanuzi wa hukumu za Mahakama ya Rufaa. Kwa minajili ipi? Kuitisha mikutano na waandishi kwenda kuzungumzia ufafanuzi wa hukumu ya Lema, hii si kazi mliyopewa na wananchi.

Hivi kweli Mwigulu suala la kufafanua hukumu za mahakama umelianza lini? Unajua kufafanua? Umesoma sheria?
Wananchi wanasubiri wanapoona wameitwa wakasikie hoja za maji, malipo ya wazee wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wangetegemea mzungumzie jinsi elimu inavyoshuka, kwanini watoto wapo shuleni hawajui kusoma na kuandika! Kwanini watoto wa Kitanzania wanakaa chini wakati nchi yetu inasafirisha magogo nje? Watanzania wana hamu ueleze kuhusu meli ya Katibu Mkuu wa CCM iliyosafirisha pembe za ndovu na kwanini hazijataifishwa kama meli za uvuvi haramu? Hayo ndiyo Watanzania wanahitaji kuyasikia, suala la kujifanya mna wema kwa kumshauri Lema, halina nafasi, linaonesha jinsi viongozi wa CCM walivyo wadandiaji wa hoja, hasa za CHADEMA, Wakiona wananchi wiki hii wanajadili jambo fulani sana, basi nao wanakurupuka kutafuta mwanya wa kujiingiza angalau na wao waseme.

Huu si ukomavu. Nimewashangaa zaidi Mwigulu na Nape kwa kujidai kuwa ni wasemaji wa Ikulu. Ikulu kama ilitajwa na Lema katika kesi yake, iwe haikutajwa, Ikulu ina wasemaji wake, yupo Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni Sefue, pia yupo Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu.
Huku kwa Mwigulu na Nape kuanza kuisemea Ikulu, ni kuidhalilisha na kuipa maana ndogo kuwa kila kiongozi wa CCM ni msemaji wa Ikulu.
 

Attachments

  • USHINDI WA LEMA.pdf
    69.4 KB · Views: 96
wenzio hawajielewi.yaan kila mtu pale hajui mipaka yake wala wajibu wake kwa chama wala serikali. mawaziri wanapishana, wengine wanahutubia upuuzi mbele za watu wa mataifa, wengine wameiba majina ya wafuu yaan ni kama mpira wa mchangan hajulikan namba tisa wala tano. labda kipa ambaye ni sawa na raisi japo hata beki anaweza kudaka ikapigwa faulo tu sio penat.
 
Hii ni kweli mkuu, watafute ajenda za kuwaambia wananchi, si kudandia maamuzi ya mahakama na kufanya ndo deal!
 
jamaa f.a.l.a sana, anadhani mahakama ni kitengo cha propaganda ya ccm
 
CCM wameishiwa hoja kabisa, wamekosa wasemaji wenye busara. Wanategemea kujibu hoja za CDM kwa matusi, kwa hiyo wamewapa madaraka makubwa vinara wa matusi kama Mwigulu, Lusinde... Wanadhani wanajijenga kumbe wanajibomoa. Hivi hawa jamaa wanadhani watanzania ni kuku wasioweza kujudge akili zao? Ni vema wakae wakijua kuwa kwa ujinga wanaouongea wao wakiwa viongozi waandamizi wa chama, wananchi tunawadharau na tunakidharau hata chama chenyewe kuwa kimepata viongozi wasiokuwa na akili. Hawa ndio wanaokizika Chama kabisa na sio kukiokoa kama wanavyodhani. Tangu lini hoja zikajibiwa kwa matusi na uzushi? Je hiyo ndiyo mbinu ambayo mwenyekiti wao aliimaanisha kwenye mkutano wao mkuu wa mwezi Novemba kuhusu namna ya kupambana na Upinzani?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom