Ushauri wangu wa vijana kuhusu Siasa

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,339
51,879
MAUSIA YA TAIKON WA FASIHI KWA HABARI YA SIASA
WARAKA WA TANO KWA MWANANGU

Mimi Baba Yako,
Ndiye Taikon wa Fasihi mwana wa Tibeli, nyota ing'aayo yenye mbawa mbili.
Nalikuandikia haya.

Ikiwa siku za mwanadamu zinahesabika basi zihesabu siku zako pekee wala usihesabu siku za mtu mwingine. Ikiwa mali za mwanadamu zinahesabika basi zihesabu mali zako pekee wala usihesabu mali za mtu mwingine. Ikiwa macho ya mwanadamu yanaona basi usione mambo ya wengine bali yaone mambo yako mwenyewe kwani kwa kufanya hivi ndivyo utakavyoishi kwa raha kama Mungu wa Baba yako alivyokuagiza. Kwa maana mwenye hekima hufanya hesabu yake mwenyewe na mpumbavu hufanya hesabu za mtu mwingine akiiacha hesabu zake. Haya na niseme sasa.

Basi Baba yako ndiye Taikon wa Fasihii, nalijiingiza katika mkondo wa Siasa, sio kwa kutaka utukufu, sio kwa kutafuta heshima, na wala sio kwa kutafuta mali au mamlaka na utawala, bali nalijiingiza huko ili nipate hekima na maarifa ya watawala na watawaliwa. Ili nipate jumla ya mambo yaliyoko huko. Haya na nianze kusema sasa.

Mwanangu, maisha ni siasa, na siasa ndio maisha. Siasa ni kutawala na kutawaliwa. Huwezi epuka kimoja wapo, sharti utawale ili usitawaliwe na kama utashindwa kutawala basi usikatae kutawaliwa kwani hayo ndio maisha, na maisha ndio siasa halisi.
Kama utafanikiwa kutawala basi usiogope kuwatawala waliokupa nafasi hiyo. Tawala kadiri ya uwezavyo, nawe usiache nafasi ya kurudi kuwa mtawaliwa.

Basi kama utakuwa Mtawaliwa ndani ya maisha yako, sikia haya;
Usikubali kutoa maisha yako kwa ajili ya mtawala. Wala usije ukadhani kuwa mtawala yupo kwa ajili yako. Hivyo usijetoa maisha yako rehani kwa mtawala usijeangamia kama mpumbavu. Kwa maana sio sifa mtawaliwa kufa kwa ajili ya mtawala bali ni upumbavu. Tena ukae ukijua kuwa mtawala hataweza kufa kwa ajili yako, na kama akifanya hivyo basi imetokea sio kwa kukusudia wala sio kwa dhamiri yake. Naye ataitwa shujaa na kukumbukwa katika historia; lakini nani atakukumbuka wewe utawaliwaye siku ukifa kwa ajili ya Mtawala. Ni dhahiri utakufa kifo cha kipumbavu na hakuna atakayekukumbuka na hata jina lako halitakumbukwa tena.

Tena usipambane na mtawala ikiwa huna uhakika wa kumshinda, wala usijiingize katika vita ya mtawala kama huna sababu inayohatarisha maisha yako mwenyewe. Wala usifuate mkumbo wa wengine usije angamia kwa upumbavu wako.
Wengine wakisema mchana, wewe sema usiku, tena wakisema usiku; wewe sema mchana. Hivyo ndivyo utakavyoishi katika maisha yako.

Watawala hutega miba njiani ili wapitao wachomwe. Nawe uonapo mwiba njiani hiyo ni bahati yako, usipige kelele kwa kusema; Tazama mwiba ule, oneni mwiba ule, mtawala kauweka mwiba' usijekusema hayo usije kupotea kama moshi angani. Kama umeuona mwiba basi kaa kimya, uruke ili usikuchome, kisha endelea na safari yako, na kama njia uipitayo inamiba mingi basi badilisha njia. Nilishawahi kukuambia kuwa, usipite njia aitengenezayo mtawala hasa aliyejitambulisha kama mwanasiasa, ni heri uchonge njia yako mwenyewe. Lau kama utakuwa mvivu au na uwezo mdogo basi pita njia hiyo kwa tahadhari.

Kama utaweza kuhesabu siku zako za kuishi basi hutakufa kabla ya wakati, lakini kama utahesabu siku za wenzako ni dhahiri hata siku yako ya kuangamia hutoijua. Basi jihadhari na mambo yasiyokuhusu usijeangamia upesi kwa kifo kisichokuhusu.

Usiishi ili upate sifa kwa mtawala, kwa maana hakuna sifa utakayoipata kwa mtawala itayaomzidi yeye mwenyewe. Kila mtawala hupenda kupata sifa. Bali ishi ili ujipatie sifa yako wewe mwenyewe kutokana na kazi njema za mikono yako. Wala usiishi kwa kujipendekeza kwa mtawala, bali jipendekeze katika mambo yako. Kwa maana kila ajipendekezaye kwa mtawala humpa sababu mtawala ya kumtumia.

Kama utakuwa masikini sana, basi usiufanye umasikini wako ni ulemavu wako, na kinga yako. Ama sababu ya kuonewa huruma na mtawala. Iwe ni Mungu au mtawala aliyebinadamu. Kwa maana hakuna mtawala amuoneaye huruma masikini. Kama vile watu masikini waivyompenda mtawala masikini ndivyo watawala wasivyowapenda masikini. Masikini hapendeki hata na masikini wenzake. Umasikini sio sifa hivyo popote pale kamwe usijtambulishe kama masikini usijeukachukiwa ghalfa.

Kama utakuwa na utajiri au uwezo kidogo basi wafanya watawala rafiki zako. Usipigane na watawala, na wala usitafute sababu ya kuungana na watawaliwa isipokuwa kwenye biashara tuu. Masikini asikufanye ugombane na watawala kwa sababu utakapoanza kupata shida masikini watakukimbia. Jitenge na visa na mikasa ya kisiasa hata kama maslahi yako yanaguswa, zaidi tafuta watawala ujenge nao shauri la mapatano baina yako na wao, nawe utaishi kwa amani.

Usitetee chama chochote cha siasa kiasi cha kutaka kutoa uhai wako ikiwa chama hiko hukikianzisha wewe. Tumia hekima kupambanua mambo yako zaidi kuliko mambo ya chama au ya mtu mwingine. Hakuna mtu anayekufa kwa ajili ya mwingine bali mtu hufa kwa upumbavu wake au kwa mapenzi ya Mungu. Basi usijekufa kwa upumbavu kwa kutetea chama kuliko maisha yako mwenyewe. Maisha ni yako na wala sio ya mtu mwingine.

Mwanangu, usikubali kuwa chambo katika ulimwengu wa siasa, hata kama yapo manufaa watakayokuambia kuwa yatakuja baadaye. Epuka kadiri ya uwezo wako kuwa chambo. Kwenye siasa mtu anayetolewa chambo ni yule ambaye hana umuhimu hivyo usikubali kwa namna yoyote ile ukadanganywa. Ukiwa chambo jua thamani yako ni ndogo ukilinganishwa na hiko kinachotafutwa.

Ukiwa mtawaliwa usikubali kwenda kwenye mikutano ya wanasiasa ikiwa hupati hata nusu ya faida ya huyo unayenda kumuona. Usikubali kwenda kumsikiliza mwanasaisa, kwa maana siku akishapa utawala yeye mwenyewe hata kusikiliza. Hivyo usiende kumsikiliza kama yeye ambavyo hatakusikiliza.

Usilie kwenye misiba ya watawala wala usifurahie kwenye sherehe zao. Kwa maana wao nao hawatalia siku ukifiwa wala hawatafurahi siku ukiwa na sherehe. Walakini kama unaukaribu na mtawala basi lia naye pindi aliapo, cheka naye pindi achekapo. Usijipendekeze kwa mtu ambaye hajipendekezi kwako. Huko ni kujidhalilisha.

Usiyaamini maneno ya wanasiasa watawala kwani wao hujivunia kuongea uongo mbele ya wale wanaowatawala. Hujisifu na kujivunia pale wanapowadanganya. Wao uongo ndio ngao ya kusuluhisha matatizo hasa yanayotokea kwa upesi. Uongo kwao ndio huona sehemu ya kutatua changamoto.

Mwanasiasa mtawala akikuambia ingai barabarani upigane usiingie wala usipigane kwa akili ya mtawala. Kwa sababu yeye hapigani kwa sababu yako bali kwa sababu ya maslahi yake mwenyewe na familia yake.

Wanasiasa wakigombana usiingilie mechi zao, kwa maana wao hugombana wenyewe na kuwaagiza ninyi mpigane, muuane na kutiana vilema. Lakini siku wakipatana hawatawaagiza ninyi mfurahie pamoja nao iwe kwa kuwapa chochote chenye maslahi na ninyi. Mtakuwa mmepoteza nguvu, mmeuana na kuwekana vilema wenyewe kwa wenyewe yaani ninyi watawaliwa wakati watawala wakila raha na wake zao

Usiende kwenye msiba wa mtawala, usijesikia sifa njema pekee hata kama alikuumiza au kuidhuru jamii yake mwenyewe.

Kwenye ulimwengu wa siasa chunga sana ulimi wako na kugusa maslahi ya watawala, utaishi kwa raha mustarehe. Kwa watawala hawatakuwa na habari na wewe.

Na siku ukiwa Mtawala
Kama utabahatika kuwa mtawala basi haya ndiyo mausia yangu.
Usiwe na huruma yoyote kwa kile unachokisikia au kukiona ukakitolea maamuzi pasipo kufikiri kwa kina. Usijeingizwa kingi na wajanja wa mjini. Kwani wengi wamefanyiwa hila na njama kwa namna hiyo.

Ukiwa mtawala fanya uwezavyo usiwape uhuru watawaliwa wasije wakakudhuru pale watakapojiweza. Uhuru wa kifikra na uhuru wa kiuchumi hasa, huu usiwape, unaweza wapa uhuru wa kijamii na kiutamaduni au kiteknolojia na kisayansi.

Kwa jinsi unavyowaumiza watawaliwa ndivyo nafasi yako ya kutawala nivyo inavyozidi kuthibitika lakini kadiri unavyowaponya vidonda vyao watawaliwa ndivyo nafasi yako ya kutawala inavyozidi kubatilishwa. Kwa maana kila mwanadamu hupenda kutawala na kila mwanadamu huitafuta siku ya kutawala ila kinachozuia ni nafasi na uwezo. Hivyo ukiwa mtawala usiwape watawaliwa nafasi wala uwezo wa kukukaribia au kukujaribu. Utaangamia.

Ukiwa mtawala usimuamini yeyote hata kama ni Mama yako. Kuwa na msimamo wako wala usiwe mtu wa kuyumbishwa. Ukiwa mtawala usiipende sana Demokrasia ila hakikisha unaowatawala wanapenda hiyo demokrasaia.

Kwenye siasa ni bora utuhumiwe unapenda udikteta kuliko usifiwe kuwa unapenda demokrasia. Ni heri mtawala awe dikteta kuliko mtawaliwa ndio awe dikteta kwani huko lazima kutokeee machafuko

Niishie hapa kwa leo

Ulikuwa nami;

Robert Heriel
Taikon wa fasihi
0693322300
Kwa sasa Dar es salaam
 
Back
Top Bottom