Urais Zanzibar: Dk. Salmin atua Dodoma kutia `ubani | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Urais Zanzibar: Dk. Salmin atua Dodoma kutia `ubani

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by MziziMkavu, Jul 9, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Jul 9, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,613
  Trophy Points: 280
  [​IMG] Aondoka ndege moja na Nahodha
  [​IMG] Aonekana mwenye bashasha nyingi
  [​IMG] Ameadimika vikaoni muda mrefu  [​IMG]
  Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein.  Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi CCM kesho itakutana mjini Dodoma kuwajadili na kuchuja majina ya wanachama 11 waliojitokeza kuomba uteuzi wa kugombea urais wa Zanzibar.
  Miongoni mwa viongozi wa kitaifa wanaotarajiwa kuhudhuria kikao hicho ni Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, ambaye kwa miaka kadhaa hajaonekana kati ka shughuli za kitaifa na katika vikao vya CCM vilivyokuwa vikifanyika Tanzania Bara na Zanzibar, kutokana na matatizo ya macho.
  Dk. Salmin ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Mstaafu, aliondoka mjini Zanzibar jana mchana kuelekea mjini Dodoma.
  Dk. Salmin alionekana mchangamfu wakati akiondoka katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar wakati wa kuingia katika ndege ya Serikali ambayo pia ilimchukua Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, ambaye pia ni miongoni mwa wagombea.
  Dk. Salmin hakuhudhuria kikao cha Kamati Maalum cha Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar Jumamosi iliyopita mjini Zanzibar ambacho kilipendekeza majina ya wagombea watano kuwa wanafaa kuteuliwa kushika nafasi hiyo. Kikao hicho kiliongozwa na Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar.
  Wagombea waliopendekezwa ni Waziri Kiongozi Mstaafu; Dk. Mohammed Gharib Bilal; Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha; Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamuhuna; Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Haroun Ali Suleiman na Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein.
  Wagombea wote watano waliopendekezwa waliwasili Dodoma jana kwa nyakati tofauti, wa kwanza akiwa Suleiman, ambaye aliondoka saa 1:00 za asubuhi kwa ndege ya Kampuni ya ZAN AIR akiwa amefuatana na mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mama Fatma Karume, na kufuatiwa na Shamuhuna, Dk. Bilal, Nahodha na Dk. Shein.
  “Usione Dk. Salmin kaamua kwenda katika kikao, Zanzibar inapita katika wakati mgumu wa kisiasa na ndio maana ameamua kwenda kuokoa jahazi,” alisema mjumbe mmoja wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutoka Zanzibar ambaye aliomba jina lake lisitajwe.
  Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz, alisema Kamati Maalum ya CCM NEC Zanzibar tayari imeshakamilisha wajibu wake wa kupokea majina, kuyapitia na kukabidhi CC ambayo itayapitia na kupendekeza majina matatu ambayo yatapigiwa kura na kikao cha NEC kesho.
  “Shughuli zote kwa sasa tumemkabidhi Katibu Mkuu wa Chama chetu, kwa upande wetu Zanzibar kazi tumemaliza tunasubiri maamuzi ya mwisho ya vikao,” alisema Ferouz.
  Wakati huo huo, jana Mohammed Raza aliandika barua ya malalamiko kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, kutokana na kutopokea barua ya mwaliko wa kuhudhuria vikao vya Dodoma.
  Kwa mujibu wa barua hiyo yenye kumbukumbu namba 786/7/7/10 ya Julai 7, mwaka huu, Raza alisema baada ya kuhojiwa na Kikao cha Kamati Maalum ya CCM Zanzibar, Mwenyekiti wa kikao hicho, Rais Karume aliwaeleza kuwa wagombea wote watapewa taarifa juu ya kitakachofuatia, baada ya kujieleza na kujadiliwa.
  Hata hivyo, alisema tangu kumalizika kwa kikao hicho, hakuna mawasiliano yoyote kati ya wagombea na chama wakati shughuli zote za uchukuaji fomu na urejeshaji zilifanyika kwa taarifa maalumu ya barua, kutoka kwenye chama.
  Raza alimueleza Rais Kikwete kuwa baada ya kuona kimya kizito, aliamua kufika Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar na kutakiwa kwenda Masjala kupata mwongozo na kuelezwa kuwa hakuna maelekezo yoyote kuhusiana na suala la wagombea kuhudhuria vikao.
  “Kutokana na hali hiyo, nakupa taarifa rasmi kuwa sijajitoa kwenye kinyang’anyiro cha kugombea urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, isije ikaonekana kuwa nimedharau kutokuja Dodoma kwenye vikao vinavyoendelea, ilieleza sehemu ya barua ya Raza kwenda kwa Mwenyekiti Kikwete.
  Hata hivyo, Raza alisema ataendelea kuwa mwanachama muaminifu wa chama hicho na yuko tayari kupokea maamuzi yoyote yatakayofikiwa na CC.
  Naye Balozi Ali Karume alisema hadi jana alikuwa hajapokea wito au mwaliko wa kuhudhuria vikao hivyo.
  Alisema kwa kuwa yeye si mjumbe wa NEC atalazimika kuhudhuria kama mshangiliaji kwa vile hadi anawasili Dodoma hakukuwepo na mwongozo wowote uliotolewa kwa wagombea wanaowania nafasi hiyo.
  Katika hatua nyingine, kikao cha bajeti cha Baraza la Wawakilishi kimeahirishwa hadi Julai 14, mwaka huu, ili kuwapa nafasi wajumbe wa CC na NEC kushiriki katika vikao vya CCM mjini Dodoma.
  Kikao hicho kimeahirishwa baada ya kutolewa hoja na wajumbe wengi kuunga mkono ambapo Spika wa Baraza hilo, Pandu Ameir Kificho, alitangaza kuwa kikao hicho kitaendelea wiki ijayo.
  Mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM anatarajiwa kujulikana kesho baada ya wajumbe wa NEC kupigia kura majina matatu yatakayopelekwa na CC.
  Tayari wanachama wa CCM wameanza kupamba maskani ikiwemo kupaka rangi kama matayarisho ya kumpokea mgombea atakayepitishwa huku mjadala ukitaja zaidi majina ya Dk. Bilal, Shamuhuna na Dk. Shein.
  Habari kutoka Dodoma zinaeleza kuwa wapambe wa wagombea kutoka Zanzibar wamejaa katika nyumba mbalimbali za wageni wakisubiri hatma ya vikao vya leo na kesho.
  Jana, ndege ya Shirika la Ndege la Precision ilikuwa ikitua mara kwa mara na kuondoka huku ikiwa imewabeba wajumbe na wapambe.
  Katika ofisi za Makao Makuu ya CCM vijana wengi wa chama hicho jana walikuwa wamekusanyika wakiwa wamevaa sare za chama.
  Wagombea ambao Nipashe iliwaona mjini Dodoma jana ni Nahodha, Shamhuna huku majina ya Dk. Shein na Dk. Bilal yakitajwa zaidi na wanachama wa CCM.
  Wajumbe wa Sekretarieti walikuwa wakikutana jana kuanzia mchana kwa ajili ya kuandaa ajenda za Mkutano Mkuu unaotarajia kufanyika Jumamosi na Jumapili.
  CHANZO: NIPASHE
   
Loading...