Upambe huu haumsaidii rais wala taifa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Upambe huu haumsaidii rais wala taifa

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Josh Michael, Oct 4, 2009.

 1. Josh Michael

  Josh Michael JF-Expert Member

  #1
  Oct 4, 2009
  Joined: Jun 12, 2009
  Messages: 2,525
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Deus Bugaywa


  INAWEZEKANA kuwa ni kiburi au jeuri ya madaraka au tu hulka inachukua mkondo wake; wahenga walisema sikio la kufa halisikii dawa. Hii ni kweli kwani kitu kikianza kuoza hakiozi nusunusu kitaendelea hivyo mpaka kimemalizika kabisa.
  Vyovyote vile iwavyo, ni wazi wapo watendaji tena wenye nguvu na ushawishi mkubwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameamua, ama kwa makusudi au kwa kutokujua wanachokifanya, kukiandalia anguko kuu la uharibifu chama chao.
  Nimekuwa nikiyatafakari majibu ya mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Amos Makalla, aliyotoa kwa vyombo vya habari na yale ya Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Propaganda wa chama hicho, Tambwe Hiza, juu ya kauli ya Jaji Joseph Warioba na za wastaafu wengine kuhusu hali ya mwenendo wa siasa nchini, nikaishia kupata mashaka juu ya aina ya viongozi wa taifa hili tulio nao leo na mustakabali wake.
  Katika taarifa yake iliyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari Makalla anasema, ninanukuu, “Msingi wa umoja, amani na mshikamano kwa Watanzania ni mambo muhimu kwa ustawi wa nchi yetu ambavyo kwa kauli ya Warioba anataka kuvunja misingi hiyo. Nawataka Watanzania kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya CCM na Rais wao kipenzi Jakaya Kikwete.” Mwisho wa kunukuu.
  Anaendelea kumlauma Jaji Warioba kuwa hajawahi kuisifia serikali ya awamu ya nne wakati yako mengi tu iliyoyafanya, kwamba matamshi yake yamekuwa yakilenga kuilaumu serikali ya Rais Kikwete.
  Hiza akizungumza kama mgeni katika kipindi cha Tuongee Asubuhi cha Star TV, Ijumaa iliyopita, alisema wanaotoa kauli za kuilaumu serikali ya Rais Kikwete ni wale waliokuwa ama wagombea wa nafasi ya urais mwaka 2005 ambao walishindwa na Kikwete au walikuwa wanaunga mkono kambi iliyoshindwa, na hivyo wana kinyongo na Rais na wanaendeleza makundi ya 2005.
  Ukisoma katikati ya mistari ya kauli za waheshimiwa hawa utaona kuna mambo mawili ambayo yanajitokeza, la kwanza ni kuwa wakosoaji wanaokosoa hali ya mambo inavyokwenda nchini wana kisa au kisasi na Rais Kikwete binafsi au unaweza ukayatafsiri kwamba wanauonea wivu urais wa Kikwete.
  Lakini kitu cha pili kinachojitokeza hapa ni kwamba wale ambao walikuwa kinyume na Kikwete wakati wa mchakato wa kura za maoni kupata mgombea urais wa CCM (ambao hawakuwa wanamtandao) hawana haki na wala hawapaswi kumkosoa kwa kuwa aliwashinda. Hii ndiyo tafsiri unayoweza kuzipa kauli hizi za utetezi dhidi ya kauli za viongozi wastaafu na wengine ambao wamekuwa wakiikosoa serikali ya Kikwete.
  Nakubalina na Makalla kwamba “msingi wa umoja, amani na mshikamano kwa Watanzania ni mambo muhimu kwa ustawi wa nchi yetu” lakini sikubalini naye kwamba “kauli ya Warioba ni ya kuvunja misingi hiyo” badala yake utetezi wao unaoongozwa na ulinzi wa maslahi ya watu wachache ndani ya chama na kutaka kuonekana wazuri kwa Rais hata kama hayo hayaendani na maslahi ya umma wa Watanzania ndio utakaovunja misingi ya hiyo anayoisema.
  Tuangalie kwa mfano Jaji Warioba amezungumzia habari za tofauti kubwa ya kipato miongoni mwa Watanzania, kwamba linajengwa tabaka la wenye nacho na wasiokuwa nacho, tena kwa mfumo rasmi kabisa wa hata mishahara ya watumishi wa serikalini, tofauti kati ya kima cha chini na kipato cha mtu wa juu kabisa haielezeki ni kama ya mbingu na ardhi. Ukishakuwa na tabaka la namna hii unategemea nchi hiyo itaendelea kuwa na amani na utulivu? Katika hali ya kawaida mwenye njaa anaweza kuendelea kuishi kwa amani upendo na furaha na jirani yake anayekula na kusaza kila siku kwa muda tu, lakini kadri siku zinavyokwenda hawezi kuvumilia.
  Leo hii katika Tanzania wako mbwa wa baadhi ya Watanzania wanakula vizuri na kutunzwa vyema kwa tiba na malazi kuliko binadamu wa Kitanzania, kati ya mwenye mbwa huyu na jirani yake anayekula kwa kubahatisha unaweza kweli ukawaita ni watu wanaoweza kuwa na maelewano ya dhati?
  Mtu anayesimama na kusema tunakokwenda siyo kuzuri na kunahatarisha mustakabali wetu hata kama watawala hawatapenda hayo anayosema ndiye atakayevunja amani na mshikamano au yule ambaye anaona hali hiyo lakini hataki kuikubali ili tu amfurahishe Rais?
  Ziko kashfa za Deep Green na Meremeta ambazo pamoja na serikali kukataa kutolea ufafanuzi lakini jamii kubwa ya Watanzania na dunia yote wameelezwa na wanajua nini kilichojificha ndani ya Meremeta, hata kama serikali itasema siyo taarifa rasmi au haina ukweli lakini yenyewe haijatoa ufafanuzi wowote, kile wanachokijua wananchi ndicho watakachokitambua kama ukweli.
  Hata kama hali ni kimya lakini liko mioyoni na kwenye nafsi ya mtu, siku moja linaweza kulipuka ili kuepusha hili serikali yoyote makini lazima ije isimame mbele iseme kipi ndicho kipi na itoe ufafanuzi wa tuhuma hizo, kuendelea kukaa kimya hakutakuwa na manufaa kwa taifa hili. Kuishauri serikali kuhusu hili haimaanishi mtu anaonea wivu urais wa Rais Kikwete au ana chuki na serikali.
  Anayesifia kila kitu hata mahali ambapo panaonekana hapafai huyo hawezi kuwa muungwana na wala haitendei haki nafsi yake, achilia mbali taifa lake, Jaji Warioba analalamikiwa kwa kuilaumu serikali ya Kikwete wakati imefanya mambo mengi mazuri, lakini walalamikaji hawa watambue kufanya mambo mazuri kwanza ni wajibu wa serikali wa msingi, viongozi waliomba kura na kuahidi kuyafanya hayo, kwa hiyo hiyo siyo hisani wanalipa deni lao kwa wananchi, lakini wanaposhindwa kufanya tunayoyatarajia ni wajibu wa kila muungwana kuwakumbusha.
  Lakini pia siyo kweli kwamba serikali ya awamu ya nne haina mapungufu, sina hakika ni lini Makalla na watu wa aina yake wameikosoa serikali ya awamu ya nne, Je wao hatuwezi kuwalaumu kwamba wamekuwa watetezi wa serikali hii bila kujali makosa na mapungufu yake, au wanataka kutuambia kwamba Rais Kikwete ni kiongozi mkamilifu ambaye hawezi kufanya makosa?
  Kama wao pamoja na kwamba serikali hii ina mapungufu lakini hawaoni hayo, wanaisifia na kuiimbia nyimbo za sifa na kutukuza basi wasiwashangae wala kuwalaumu wenzao wanaoona upande wa pili ambao wao hawauoni au wanaona lakini wanaupuuza kwa sababu zilizo wazi, wajipime kwa kipimo kilekile wanachowapimia wengine.
  Viongozi wa ngazi ya juu kwa kiwango cha ujumbe wa Kamati Kuu ya CCM kimsingi ndio wanaoedeleza makundi na kuwagawa wanachama wao wanapowatafsiri kwa hisia binafsi zaidi kauli wanazozitoa kuliko kuongozwa na hoja zilizomo ndani ya kauli hizo.
  Kilio cha uongozi kuwa karibu mno na matajiri siyo cha leo wala jana, na hili linaonekana wazi wazi katika ngazi zote za utendaji na ni dalili mbaya kwa hatma ya nchi, kwa sababu wananchi wengi wakiamini kwamba serikali iko kwa ajili ya kundi la watu wachache wenye fedha, au inawasikiliza wao zaidi kuliko wananchi wa kawaida maskini, hii haiwezi kuwa ni dalili njema kwa uhai wa taifa hili. Kutolisema hili ili kuwakumbusha viongozi kwamba kuna hatari ni dhambi mbaya zaidi, wastaafu wanachojaribu kusema ni kuisaidia nchi hii na hasa viongozi wake ili waweze kuona ni namna gani taifa linakoelekea katika uchaguzi mkuu na wa serikali za mitaa wanaliepusha taifa na balaa. Kama wana CCM hawa wanadhani wanampenda Rais Kikwete na wanakitakia kheri chama chao na kama wanaitakia heri Tanzania na Watanzania wote basi wafike mahali wawe waungwana, wamwambie mfalme ukweli kama yuko uchi wamshauri avae nguo, siyo kila anayechungulia anakuja na jibu la mfalme kapendeza wakati hali sivyo ilivyo.
  Mungu ibariki Tanzania.
   
Loading...