Uongozi Wetu Na Swali La Kifalsafa- Niweje?

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Uongozi Wetu Na Swali La Kifalsafa:
- Niweje?

HATA kama ni mara chache sana nachangia maoni yangu, nimekuwa ni mmoja wa
wanaofuatilia mijadala mingi kwenye majukwaa mbalimbali mtandaoni. Ni darasa
zuri, kuna mengi ya kujifunza. Miye ni wale wa ‘Kizazi Cha Azimio’. Hutokea
mara kadhaa kuona jinsi kizazi na makuzi yanavyochangia tofauti za kimaono
na kimtazamo.

Nilikuwa bado mtoto mdogo sana wakati Azimio la Arusha linazaliwa, 1967.
Hata hivyo, nimekulia katika vuguvugu la Azimio. Miaka kumi baada ya Azimio
la Arusha nilikuwa sijatimiza miaka kumi ingawa nilikuwa na akili timamu
kulishuhudia na kulielewa tukio kubwa la kwanza la kisiasa nililopata
kulishuhudia katika historia ya nchi yetu Tanzania; KUZALIWA KWA CHAMA CHA
MAPINDUZI, CCM, tarehe 5.2.1977.

Nilikuwa mmoja wa watoto waliokaa chini pale Ofisi ya TANU Ilala Bomani,
kandokando ya barabara ya Uhuru. Nilikwenda pale na watoto wenzangu kutoka
Mtaa wa Iringa, Ilala. Tulikwenda kushuhudia bendera ya TANU ikishushwa, ya
CCM ikipandishwa. Barabara ile ilifungwa na watu walifurika. Kulikuwa na
gwaride la Chipukizi, ngoma na kwaya ( Kwaya ya Marehemu Mzee Makongoro).

Kaka yangu, Grey, alikuwapo pia kucheza halaiki na kikundi chao cha ‘
Manyanda’. Alisoma Shule ya Msingi Boma. Pale Ilala Bomani niliona nyuso za
watu wazima zilizojaa imani. Ni imani kwa viongozi wao na imani kwa taifa
Tanzania. Imani ile iliambukizwa kwetu tuliokuwa watoto enzi hizo, tulijawa
imani na matumaini.

Naam. Ilihusu imani. Siasa ni jambo zuri na siasa ni imani. Siasa ndio
inayoendesha nchi. Hivyo basi, kuna umuhimu mkubwa wa uwapo wa imani ya
wananchi kwa siasa ya nchi, kwa wanasiasa na viongozi wao. Katika hali ile
ya utoto, nilitamani sana nikue nije kuwa kiongozi wa kisiasa, ikiwamo siasa
za majukwaani pia. Kwa wakati huu sina ndoto za siasa za majukwaani hadi
hapo mazingira yatakaponiridhisha. Maana, enzi hizi si zile za Katibu Tarafa
kusimama jukwaani akajieleza na kupata ubunge kwa kumshinda Profesa wa Chuo
Kikuu. Hii leo, mtu akitangaza kuwa ana dhamira ya kugombea udiwani, achilia
mbali ubunge, kuna watakaomtazama kwa kumtilia mashaka. Watajiuliza ni wapi
ameyatoa mamilioni ya shilingi ili agharamie kampeni zake ikiwamo kuwahonga
wapiga kura. Si wote wenye kugombea nafasi za siasa siku hizi wanaolazimika
kuhonga wapiga kura lakini kuna wengi wanaofanya hivyo. Nimejifunza, kuna
njia nyingine pia za kufanya kazi za siasa bila kusimama majukwaani, ni
nyingi.

Nchi yetu sasa ina viongozi wengi vijana wanaochipukia, ni jambo jema
kabisa. Wengi wao wamezaliwa miaka ya 70. Wana mapya mengi ikiwamo mitazamo
pia. Mwongo mmoja ujao ( Miaka kumi ijayo) Watanzania wa kizazi changu na
kile cha miaka ya 70 na 80 ndio watakaoshika nafasi nyingi za uongozi wa
nchi.

Mwanafalsafa Frank Fanon anasema; kuwa kila kizazi kina wajibu wa kulitambua
jukumu lake na kulichukua. Lakini inakuwaje kama kizazi husika hakijitambui?
Kutambua jukumu na kuchukua wajibu kuanze na kujitambua.

Naam. Swali la msingi ni niweje? Ni swali la kifalsafa,. Inahusu virtue, kwa
maana ya maadili na kutenda yalo ya haki. Kutenda yalo mema. Mtu mwenye
maadili mema utamwamini, ndivyo pia wasemavyo WaNgereza; a virtuous person
is someone you can trust.

Mzazi anapaswa kuwa a virtuous person, kiongozi wa kisiasa anapaswa kuwa a
virtuous person, kiongozi wa kidini anapaswa kuwa a virtuous person,
Mwandishi wa habari anapaswa kuwa a virtuous person, vivyo hivyo mwalimu.
Kwa hilo la mwisho, mahusiano ya Mwalimu-Mwanafunzi kati ya Mwanafalsafa
Socrates na mwanafunzi wake Plato yasingepata umaarufu ulionao sasa kama
Plato angebaki kuwa ‘ mwanafunzi’ tu- kivuli cha Mwalimu. Socrates
alitambua, kuwa jukumu la mwalimu ni sawa na la mkunga. Mwalimu ni mkunga.

Katika mijadala ya siku hizi tunaona hata wale wanaojiona ni viongozi wasivyo
tayari kukosolewa. Wasivyo tayari kuyaona mapungufu yao. Inasikitisha kuona
baadhi ya viongozi hawa ni vijana sana. Wamekuwa wabinafsi zaidi huku
wakijiita ni viongozi. Wanajiita viongozi ilhali, kwa namna nyingi,
hawawatendei haki wanaowaongoza, wanatanguliza zaidi tama ya mali na
mamlaka. Yamkini, kiongozi mtenda maovu kwa watu wake ni ama mjinga au
mgonjwa. Kama ataambiwa bayana kuwa anatenda maovu, au ana mapungufu ya
kiutendaji, basi, huenda tutamsaidia kujirekebisha. Lakini kamwe usishangae,
kama kiongozi huyo atatingisha mabega na kucheka tu, kutushangaa siye
tunaomkosoa. Naendelea kutafakari…
Maggid,
Iringa, Januari 12, 2010

http:// mjengwa.blogspot.com, http://www.kwanzajamii.com,
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom