jiamini360
Member
- Jan 26, 2016
- 35
- 19
Uongozi ni mamlaka au karama ya kuonyesha njia kwa vitendo.
Kipimo cha uongozi ni jinsi gani kiongozi anaweza kuleta ushawishi kwa watu na kufikia maendeleo yaliyotarajiwa. Kiongozi bora hana muda wa kulalamika bali anatafuta ufumbuzi wa matatizo ya watu, yaani wananchi au watu walio chini yake. Kiongozi wa kweli akiongea, watu husikiliza.
Maana ya uongozi
Uongozi ni dhana, taaluma inayompa mhusika madaraka na uwezo wa kuwawezesha wale wanaongozwa naye kuunganisha nguvu, stadi na vipaji vyao na kuvitumia ili kufikia malengo yao. Kuongoza ni kujua lengo la wale wanaoongozwa na njia ya kufikia lengo lao.
Sifa za kiongozi bora
i. Awe na ufahamu. Kiongozi ni lazima awe na ufahamu mkubwa juu ya taasisi anayoiongoza, malengo yake, mazingira na matatizo yake.
ii. Awe mwaminifu. Kila taasisi inalenga kufikia shabaha fulani. Ni wajibu wa kiongozi kuwaongoza wanataasisi ili wafikie malengo yao. Kwa hiyo kiongozi ni lazima aweze kubuni mikakati na mbinu zitakazoiwezesha taasisi anayoongoza kufikia malengo yake.
iii. Mwenye Maadili mema. Kiongozi ni lazima akubalike katika jamii na taasisi anayoiongoza. Ili akubalike ana budi kuzingatia maadili ya msingi ya jamii na taasisi yake. Kiongozi mwongo, mlevi, mvivu, asiye mwaminifu n.k. hawezi kuwa kiongozi mzuri.
iv. Amche Mungu.
UTAWALA BORA
Utawala bora ni matumizi ya uwezo (mamlaka) wa kiserikali katika jitihada za kuongeza na kutumia rasilimali hizo ili kuboresha maisha ya wananchi
MISINGI YA UTAWALA BORA
- Utawala wa kidemokrasia
- Ushirikishwaji wa umma
- Utawala wa kisheria
- Haki na usawa kwa watu wote
- Uwazi katika kuendesha shughuli za maendeleo
- Uwajibikaji katika utendaji
- Uadilifu
Ili utawala bora uwe na sifa za kupendeza na kupendwa na wananchi lazima uzingatie Misingi ya utawala bora.
Utawala wa Kifalme
ni mfumo wa uongozi unaompa mamlaka ya dola na ya serikali Mfalme. Katika mfumo huu madaraka hurithiwa na mtu wa familia ya kifalme.
Utawala wa Kiimla
ni mfumo wa uongozi unaotoa madaraka yasiyo na mipaka kwa kiongozi. Katika utawala huu watu binafsi hawana haki na uhuru katika maamuzi.
Utawala finyu
ni mfumo unaowapa wachache nguvu za maamuzi katika dola na serikali. Nafasi ya wachache hawa hutokana na haiba na uwezo wao kiuchumi, kijamii, kijeshi au kutokana na mafanikio yao katika nyanja mbalimbali za maisha. Mfumo huu ni nadra sana siku za hivi karibuni. Pia waweza kuitwa utawala wa makabaila.
Utawala wa Umma
ni utawala unaotokana na jamii kuamua misingi ya kujiongoza. Mfumo huu wa utawala hujulikana kama Utawala wa Kidemokrasia na umegawanyika katika sehemu nne.
Demokrasia Baguzi
ni aina ya Demokrasia inayojikita katika kulinda nguvu za kiuchumi zaidi.
Demokrasia Duni
ni aina ya demokrasia inayotokana na makundi ya watu na kisha kupitia makundi hayo watu kuunda serikali mfano: chama - serikali.
Demokrasia Endelevu
ni aina ya demokrasia inayotoa fursa ya usawa na kupinga matabaka katika jamii.
Demokrasia Shirikishi
katika aina hii ya Demokrasia wachache hupewa dhamana na wengi katika uwakilishi wa jamii katika maamuzi.
Wachache huchaguliwa na wengi kwa njia ya Demokrasia huru na haki kwa kufuata Katiba ya nchi hiyo. Mfano: Wabunge uwakilisha wananchi wao katika kuleta maendeleo na kuishauri serikali juu ya maendeleo ya nchi.
Demokrasia
ni mfumo unatoa fursa ya madaraka kwa umma moja kwa moja au kutokana na kuwakilishwa.