Mimi ni mwanakijiji,ingawa pia ni mfanyakazi wa serikali.Vijiji vingi vina kasoro nyingi za wazi za kiungozi,kwa kweli there is much to be desired.Kuna uonevu wa wazi wa wanakijiji.Siku moja katika hali ya kusikitisha nilishuhudia wanakijiji katika kijiji changu cha Dakawa ambao walishindwa kulipa mchango wa mradi wa maji wakifungiwa kwenye darasa la shule ya msingi kwa masaa kadhaa, eti mpaka walipe mchango huo!Wanakiji walio wengi wa kijiji hiki ni maskini wa kutupwa,na kumwambia alipe Sh.3,500 ni sawa na kuomba jamvi msibani.Tabia hizi zimekuwa za kawaida kabisa katika kijiji hiki,bila hata kujali hali halisi za wanakijiji hawa.Vitisho kwa wanakijiji ni vingi ikiwa pamoja na kutishiwa kwamba watafungwa ikiwa hawakutoa mchango huu au ule,sijui kwa kutumia sheria zipi!Lakini unapochunguza hasa kwanini mambo yanakuwa hivi, unagundua kwamba fujo zote hizo zinafanywa ili kupata fedha kwa ajili ya kushibisha matumbo ya viongozi,na wala sio kwa sababu ya maendeleo ya wanachi.Ninalojua ni kwamba michango yote ni hiari, na wananchi wanatakiwa wahamasishwe katika uchangiaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo yao na sio kulazimishwa.
Katika hali nyingine isiyokuwa ya kawaida,wanachi waliambiwa waandikishe majina ili hatimaye wapate mbolea ya ruzuku.Wananchi kwa kujua kwamba kwa vile ndugu yangu Waziri wa Kilimo alikuwa ameongelea swala hili kwa uzito sana,na kwamba vile pia alishasema mbinu ya wakati huu ya kutumia coupon itafanikiwa,walijiandikisha kwa wingi, huku wakijua kwa hakika kwamba watapata mbolea.Kilichitokea hata hivyo ni tofauti kabisa.Wanachi walio wengi waliojiandikisha hawakupata mbolea,eti kwa vile wao wana uwezo wa kununua mbolea isiyo ya ruzuku.Sina hakika kama mbolea ya ruzuku ni ya watu wa kipato fulani tu.Na wale waliopata walikwenda kuchukua mbolea kwa kutumia vyeti vya kupigia kura badala ya coupon kama ilivyo ahidiwa,hali inayotoa mwanya wa wazi wa kuuza isivyo halali mbolea ya ruzuku.Kwa ujumla zoezi zima lilikumbwa na mizengwe ambayo inaashiria ufisadi!
Ushauri wangu kwa serikali ni kwamba kama kweli ina nia ya kusaidia wakulima wake, ni bora mbolea yote inayotumika nchini ikawa ya ruzuku,hasa kwa vile mbolea yote inayoingizwa nchini inatumika kwa shughuli za uzalishaji wa kilimo,vinginevyo matatitizo haya hayatakwisha.Watu wasio waaminifu watatumia mbinu zozote zile kujinufaisha kwa kutumia mianya iliyopo.Sina shaka kabisa kwamba kama serikali ikijipanga vizuri,uwezo huo inao.Ni vema pia serikali ikawa karibu zaidi na vijiji, ili wananchi wasionewe,na kukatishwa tamaa katika kujiletea maendeleo yao.Nina hakika kwamba matukio haya sio isolated kwa Dakawa peke yake lakini yamesambaa nchi nzima.