Undani waliodai kupigwa na askari wilayani Mbarali

peno hasegawa

JF-Expert Member
Feb 24, 2016
12,830
21,460
Wakati Serikali ikikanusha madai ya wananchi kuteswa na askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) katika Kijiji cha Mwanavala, Mbarali mkoani Mbeya, wananchi hao wameibuka upya wakifafanua madai yao.

Mei 11 mwaka huu, Mbunge wa Mbarali (CCM), Francis Mtega aliomba Bunge liahirishe shughuli zake ili kujadili tukio la askari wa Tanapa la kudaiwa kuumiza wananchi, kuua mifugo na kupora mifugo katika jimbo lake.

Alisema askari hao wa jeshi usu waliwashambulia na kuwajeruhi wananchi kwa madai ya kuingilia mipaka ya hifadhi.

Madai ya mbunge huyo yalimfanya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kumwagiza Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa kwenda Mbarali kufuatilia suala hilo na kumpelekea taarifa.

Hatimaye Mei 12 Waziri Mchengerwa akiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Zuberi Homera na viongozi mbalimbali wa CCM walifika katika kijiji hicho.

Baada ya Waziri Mchengerwa kutembelea eneo hilo akiambatana na uongozi wa Tanapa, alitoa taarifa ya kukanusha madai ya unyanyasaji ulioibuliwa na mbunge.
“Nimesikitishwa sana na kauli za mbunge na baadhi ya malalamiko na shutuma zake dhidi ya Serikali zimeleta taharuki kubwa ambayo sijaikuta katika eneo hili.

“Wananchi wamekiri kuingia ndani ya eneo hili na wameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa kuwatafutia maeneo ya kuishi,” alinukuliwa Mchengerwa katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Hata hivyo, kiongozi huyo alikiri kuwa mbwa walipigwa risasi kwa sababu walikuwa wanawatishia askari waliokuwa wanatimiza wajibu wao.

Kilio cha wananchi

Baada ya kauli hiyo ya Waziri Mchengerwa, mwandishi wa habari hizi alifika katika kijiji hicho na kuwasikiliza wananchi wanaodai kupigwa, kushambuliwa wakisimulia tukio lilivyokuwa.

“Maisha yetu yapo hatarini, tunaishi kwa hofu,” alisema Golyama Chimya anayedai kuathiriwa na tukio hilo.

Chimya alisema Mei 6 asubuhi akiwa maeneo ya nyumbani kwake akitafuta ng’ombe wake, aliona helikopta inayofanya kazi kwenye hifadhi ikitua karibu yake na kuanza kuswaga mifugo yake.

“Waliposhindwa wakanifuata na kunipiga kwa rungu katika maeneo mbalimbali ya mwili,” alisema Chimya huku akionyesha majeraha ya kutandikwa, hasa maeneo ya mgongo na kwenye mbavu.

Kwa mujibu wa Chimya, licha ya kuwaomba wamuache au wampeleke kwenye vyombo vya sheria iwapo ana makosa, askari hao waliokuwa wawili hawakumsikiliza.

“Walinitesa sana, ikiwemo kunichoma kwa panga la moto katika makalio na sehemu nyingine za mwili.

“Nilikwenda hospitali nikatibiwa na daktari akaniambia kama hali yangu itazidi kuwa mbaya nirudi kwa matibabu zaidi, lakini hadi sasa bado afya yangu si nzuri, siwezi kufanya kazi yoyote wala kutembea umbali mrefu,” alisimulia Chimya akisema hata hivyo hajarudi hospitali kutokana na kukosa fedha.

Aliendelea kueleza kuwa vitu vyake vyote vilichomwa moto na alishangazwa na viongozi waliofika kuwajulia hali kupindisha ukweli kuhusu walichokiona.

Alifafanua kuwa kutokana na mateso aliyopata, aliwaomba wamuue moja kwa moja kuliko kumuacha na ulemavu wa kudumu lakini haikuwa hivyo.

Alisema kwa sasa wanaishi kwa hofu na wasiwasi katika kijiji hicho.
Mfugaji mwingine, Mage Ntalamila alisema siku ya tukio hilo alikwenda kumsaidia mwenzake kutafuta ng’ombe aliyetoroka zizini baada ya kuzaa, alikwenda hadi mashambani.

“Wakati naendelea kutafuta nikaona helikopita kama inanifuata huku ikinitimulia nyasi machoni, nikadondoka kwenye kichaka. Ghafla ikatua chini, nikawaona askari wawili wakishuka na kuniuliza natafuta nini kwenye hifadhi.

“Nikawajibu pale si hifadhini bali ni makazi ya watu, ndipo mmojawapo akamwambia mwenzake ‘piga huyo’. Katika jitihada za kumkwepa nilidondokewa na gogo, wakaniamsha wakanifunga mikono kwenye kiota cha moto na kuendelea kunipiga, huku wakiwa wamenivua nguo zote,” alidai Ntalamila.

Ntamila alisema katika helikopta kulikuwa na rubani mwanamke ambaye aliona huruma kwa namna alivyokuwa akitendewa na askari hao.

Alisema rubani huyo alisogea katika eneo hilo na kuwaongelesha kwa Kiingereza, ndipo askari hao wakaacha kumtesa.

Kwa upande wake Rehema Milakoni alisema akiwa na wenzake wakichuma mboga shambani, alikamatwa na askari hao waliomhoji shughuli anazozifanya katika eneo la hifadhi.

“Walituuliza kwa nini tunachuma mboga eneo lile, tukawajibu huwa tunachuma, wakaanza kutupiga mapanga, baadaye akashuka rubani akasema waache,” alisema Milakoni.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwanavala, Chesco Kapunga alisema tukio hilo lilitokea kweli na ni watu watano walioathirika kwa kipigo.

Alazwa siku mbili

Daktari Deogratias Gama alisema Chimya alifika kituoni Mei 6 na kulazwa, kisha kuruhusiwa Mei 8 kutokana na maumivu aliyosema yametokana na kipigo.

“Alikuwa na ganzi mguuni hawezi kutembea na kichwani akiwa amechanika kidogo na makovu mgongoni na pajani na katika maelezo yake alidai kupigwa na panga, hali iliyomsababishia maumivu hayo.
“Alikuja Jumamosi Mei 6 na kuruhusiwa Mei 8, sisi tulitoa huduma kadiri ilivyowezekana hadi kuruhusiwa,” alisema Dk Gama.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera alipoulizwa alisema tukio hilo ni la kweli na watu watano walijeruhiwa na wanaume wawili waliumia zaidi.

Alisema wanawake watatu walikuwa na maumivu ya kawaida ya hapa na pale na kwamba aliamuru ndani ya saa 24 askari waliohusika wakamatwe.

“Askari watatu walikamatwa na uchunguzi unaendelea kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria kwa sababu hakuna Serikali iliyomtuma askari wake kumpiga mwananchi.”

“Lakini hata wale majeruhi wawili nilitoa maagizo watibiwe na Serikali na walitibiwa hadi kupona na kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa alifika eneo la tukio na kutoa pole.

“Waziri alisema hakuna mwananchi aliyeporwa mifugo, aliyebakwa wala kutaka kujinyonga, kwa sababu yule mbunge alisema kuna mifugo 170 imeporwa kumbe hakuna,” alisema Homera.

Juhudi za kumpata Waziri Mchengerwa kuzungumzia malalamiko ya wananchi hazikufanikiwa, kwani simu yake imekuwa ikiita bila kupokewa na hata ujumbe aliotumiwa haukujibiwa.

Homera alisema baada ya kupata taarifa hizo, alifika eneo la tukio kijiji cha Mwanavala akiambatana na kamati ya ulinzi usalama na walijiridhisha kwamba wananchi hao wamevamia eneo la hifadhi na ametoa wito waache kuvamia hifadhi hiyo.

Hata hivyo, Mgaluli Chimya, kaka wa Golamya Chimya anasema bado hali ya mdogo wake haijawa vizuri na anafikiria kumpeleka Hospitali ya Iponda iliyopo Makete mkoani Njombe kwa uchunguzi na matibabu zaidi.

Kuhusu gharama za matibabu kulipwa na Serikali, Chimya alisema hawajapewa utaratibu wowote na yeye ndiye anahusika kwa kila kitu.

“Gharama zote nahusika mimi, ile siku ya tukio ndiyo mkuu wa wilaya aliwapeleka wale wengine watatu hospitali ya Wilaya Mbarali, lakini mdogo wangu tulimpeleka Mission ambayo ni binafsi na gharama zote ni mimi,” amesema Chimya.

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom