Unataka kuunda Bendi? Sehemu ya kwanza

John Kitime

Member
May 25, 2020
7
30
Kuna mambo ambayo kwa uzoefu wangu wa muda mrefu katika tasnia hii, ninaweza kusema yangesaidia sana kuunda bendi bora. Kwanza lazima kuwa na sababu za msingi kwanini unataka kutengeneza bendi. Nimeshakutana na wanamuziki wengi wanataka kuanzisha bendi lakini ukiwauliza nia ya kutengeneza bendi wanakuwa na kigugumizi.

Kuna sababu nyingi ambazo nazifahamu za kutaka kuunda bendi, kuna wanaotaka kuunda bendi ili wapate sifa, wengine huunda ili wakawafanyie maonyesho watalii, wengine huunda bendi ili wapige muziki wa mwanamuziki, kuna wanaounda bendi ili wasafiri nchi mbalimbali duniani, au washiriki matamasha ya kimataifa.

Kuna wanaounda bendi ili watangaze bidhaa au itikadi zao, na kuna wanaounda bendi ili wapate fedha,na kuna wanaounda bendi kwani wanaona wana tungo ziko vichwani mwao ambazo wanadhani zingeweza kuchangia na kukuza makataba ya nyimbo za bendi katika jamii yao. Ni muhimu sana kabla ya kuunda bendi kuwa na lengo lililo wazi kwanini bendi inaundwa.

Kufahamu nia ya kuunda bendi kutasaidia namna ya kujipanga katika yote yatakayofuata. Bendi inaweza kuundwa kwa wanamuziki wenye nia moja kujikusanya na kuanza kutafuta vyombo, na njia nyingine ambayo ni maarufu sana ni mtu mwenye uwezo kununua vyombo kisha kuanza kutafuta wanamuziki.Ila kabla ya kufikia hatua hii ya kununua vvyombo kuna haja ya kujua ni aina gani ya bendi inatotaka kuundwa. Kuna aina nyingi sana za bendi.

Kwa mfano kuna bendi kama Kilimanajaro Band ‘wana njenje’. Bendi hii nyimbo zake nyingi zina tumia magitaa matatu, solo, rhythm na bass, halafu vinanda vitatu, drums na tumba. Kuna bendi zina tumia magitaa matatu hayo, trumpet, saxophone, drums na tumba kama vile Msondo na Sikinde.Kuna nyingine hazina vyombo vya upulizaji, pia kuna bendi zinazotumia magitaa manne gita la nne linakuwa ni second solo. Hivyo ni muhimu kujua aina ipi ya bendi inataka kuundwa.

Kosa kubwa hufanywa na wadau wengi ni kuamua kuingia dukani na kununua vyombo wakitegemea ushauri wa wauzaji wa vyombo hivyo. Kwanza sio siri kuwa kuna vyombo vingi vya muziki vilivyo madukani humu nchini ni ‘feki’. Unakuta chombo kina alama ya YAMAHA, au Mackie majina yenye sifa za vyombo bora kumbe ni feki, si rahisi mtu asiye mzoefu kugundua kuwa anauziwa ‘mafafa’.

Hivyo ni muhimu kusindikizana na ‘fundi wa vyombo’ kununua vyombo vipya na sahihi. Kwa mfano magitaa yako marefu na mafupi, kuna magitaa ya bezi yenye nyuzi nne na mengine yana nyuzi tano na hata zaidi, na pia kuna kamapuni maarufu za kutengeneza magitaa, na hivyo ni muhimu kuwa na mtu mwenye ujuzi wakati wa kutafuta vyombo.

Angalizo, si kila mwanamuziki anafahamu vyombo bora. Unaweza kununua vyombo ‘original’ lakini si sahihi kwa matumizi ya bendi. Matokeo ya makosa ya kuchagua vyombo ni kujikuta vyombo vikiharibika baada ya muda mfupi, au kutokupata sauti nzuri licha ya kuwa na vyombo vipya. Tatizo jingine la kununua vyombo bila ushauri sahihi ni kujikuta unatumia fedha nyingi kununua vyombo visivyo sahihi.

Kwa mfano mara nyingine unaweza ukakuta bendi ambayo kazi yake ni kupiga katika kumbi za bar inanunua vyombo vyenye uwezo wa kupiga kwenye uwanja wa stadium. Huko ni kupoteza fedha, na mbaya zaidi unaweza kukuta bendi inataka kutumia vyombo hivyo kwenye kumbi ndogo na hivyo kuwa kero kwa wasikilizaji na majirani kwani bendi inakuwa na kelele mno. Mara nyingi bendi ambazo zimeanzishwa na mtu mmoja ambaye ni mwanamuziki aliye na picha ya aina ya muziki ambao anataka kuupiga mara nyingi ndizo hudumu muda mrefu zaidi.

Lakini bendi ambazo wanamuziki wake hutokana na uteuzi wa kamati, au kundi la marafiki au wapenzi wa muziki, maisha yake huwa mafupi sana, bahati mbaya njia hii hupendelewa sana na wadau ambao wana uwezo wa kununua vyombo. Mara nyingi watu hawa huamini kuwa wakichagua wanamuziki maarufu au wanamuziki bora na bendi watakazounda zitakuwa na ubora. Kamati au maseneta wa bendi hukutana na kuanza kupanga wanamuziki ambao wangefaa kwa bendi yao.

Majina ya wanamuziki wazuri na maarufu huchaguliwa na kutafutwa bei yoyote ili kuunda bendi, tatizo ni kuwa wanamuziki hawa pamoja na ubora wao wanaweza kuwa na mitizamo tofauti kimuziki, na hiyo ndio mbegu ya kwanza ya kuhakikisha bendi haitadumu. Ushauri kwa wale ambao wanataka kuwa na bendi, tafuta mwanamuziki mmoja unaeona anafaa na umkabidhi kazi ya kukusanya wanamuziki ambao anadhani watamfaa. Usiingize chaguo lako, hiyo ni kupanda mbegu ya kuja kuvunja bendi.

32267126_10216105112959494_9221846034974507008_n.jpg




Soma sehemu ya Pili hapa

Unataka kuunda BENDI? Sehemu ya Pili - JamiiForums
 
Na mfano wa bendi au kikundi cha muziki lilichokamilika kila idara ni hiki chenye makao yake Bagamoyo, Tanzania




Source : msafiri zawose
 
Hongera sana Mzee Baba kwa bandiko lako zuri na lenye mafundisho mengi kwa Wanamuziki wenzako. Mungu aendelee kukujalia afya na uzima tele.

Huwa ninakuona mara nyingi kwenye interview mbalimbali! Umejaliwa moyo usio na chembe ya ubinafsi kwenye utoaji wa Elimu ya maasuala ya Muziki kwa Wanamuziki wachanga.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom